Radi yaua ng’ombe 22 Sumbawanga

Sumbawanga. Mvua zinazoendelea katika maeneo mbalimbali nchini zimeleta madhara ambapo ng’ombe 22 wamekufa baada ya kupigwa na radi.

Tukio hilo lilitokea jana Desemba 9, 2024  katika Kijiji cha Songambele Azimio, Kata ya Msanda Muungano wilayani Sumbawanga mkoani Rukwa.

Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo leo Jumanne, Desemba 10, 2024, Katibu Tawala wa wilayani hiyo, Gabriel Masinga amesema ng’ombe hao ni mali ya Fale Keleja mkazi wa kijiji hicho.

Amesema mvua iliyonyesha jana, iliambatana  na upepo mkali na radi.

“Taarifa nilizozipata, mvua hiyo iliambatana na radi nyingi na upepo mkali sana, na ng’ombe waliokufa wote ni wa mwananchi mmoja,” amesema Masinga.

Hata hivyo, amesema hakuna madhara yaliyotokea kwa binadamu na amewataka wakulima na wafugaji katika wilaya hiyo kuendelea kuchukua tahadhari katika kipindi hiki cha mvua, ili kujiepusha na majanga kama hayo.

“Mtu akiona dalili ya mvua asiende shambani wala kupeleka mifugo malishoni,” amesema.

Amewasisitiza wananchi kuacha mila potofu kuwa wanyama hao wamekufa kwa imani za kishirikina badala yake wachukue tahadhari.

Mmoja wa wananchi wilayani humo, Exavery Nkisi amesema tukio hilo si la kwanza kutokea, akieleza kuwa ni maumivu kwa wafugaji na wananchi kwa ujumla.

“Tukio kama hili lilitokea hata mwaka jana,” amesema Nkisi.

Related Posts