TANZANIA imeandika historia kubwa baada ya wanafunzi wa Shule ya Sekondari Arusha Science kushinda tuzo nne za heshima katika mashindano ya kimataifa ya Ufanisi kwa Vijana (Junior Achievement) yaliyofanyika nchini Mauritius, yakihusisha mataifa 11 kutoka barani Afrika. Anaripoti Mwandishi Wetu, Port Louis, Mauritius … (endelea).
Wanafunzi hao wa Kidato cha Sita, kupitia kampuni yao ya BLOOMTECH, wamebuni programu inayosaidia wakulima kupata suluhisho la changamoto mbalimbali zinazokabili mazao yao.
Ubunifu huu uliiwezesha Tanzania kushinda Tuzo ya Umahiri wa Ujasiriamali Tuzo ya Matumizi Bora ya Usimamizi wa Miradi
Tuzo ya Uongozi wa Wasichana (Girl LEAD Award)Tuzo Kuu – Mshindi wa Kwanza.
Vijana watatu waliowakilisha Tanzania, Yvonne Lyaruu, Baraka Kileo, na Angel Mtakwa, walionyesha uongozi wa kipekee na ushindani wa hali ya juu, wakitangaza ushindi huo kuwa si wao tu bali ni wa taifa zima.
Akizungumza baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro, Yvonne alisema: “Tulipata changamoto kubwa kwa sababu washiriki wote walikuwa wamejiandaa vizuri. Hata hivyo, tuliamini kuwa tunaweza kushinda, na tumefanikiwa kwa juhudi zetu na imani thabiti.”
Baraka Kileo aliongeza: “Mashindano haya yalihusisha nchi 11 za Afrika, na kupitia kampuni yetu ya BLOOMTECH, tumeibuka kuwa kampuni ya mwaka barani Afrika. Ushindi huu ni wa kipekee na umetufungulia njia kushiriki mashindano ya kidunia nchini Brazili mwaka 2025.”
Angel Mtakwa alisema kuwa ushindi huo pia umeonyesha uwezo wa wasichana kwenye uongozi, hasa baada ya kushinda Tuzo ya Girl LEAD Award, ambayo imewapa nafasi ya kuiwakilisha Tanzania nchini Ghana mwaka 2025.
Ushindi wa Kihistoria
Mkurugenzi wa Shule ya Sekondari Arusha Science, Prof. Nuhu Hatibu, alisema matokeo haya yametokana na utekelezaji wa sera ya taifa ya elimu ya amali, akihimiza serikali kuwekeza zaidi katika eneo hili.
“Arusha Science tumejikita katika kuhakikisha elimu ya vitendo inatekelezwa kikamilifu. Ushindi huu ni uthibitisho wa uwezo wa Tanzania kushindana kimataifa,” alisema Prof. Hatibu.
Harun Kidungu, mratibu wa mashindano kutoka taasisi ya The Foundation for Tomorrow, aliyeambatana na wanafunzi hao, alisema: “Mashindano haya yanalenga kuwasaidia vijana kujitegemea kupitia ubunifu. Suluhisho walilobuni linaonyesha njia mpya ya kupunguza tatizo la ajira kwa vijana, ambalo ni changamoto kubwa duniani.”
Wazazi wapongeza mafanikio
Dororosa Dankani, mzazi wa mmoja wa wanafunzi, aliwataka wazazi wenzake kuwaruhusu watoto wao kutumia vipaji vyao badala ya kuwalazimisha masomo yasiyoendana nao.
“Kwa mfano huu, ni dhahiri kuwa talanta za watoto wetu zinaweza kuwafanikisha zaidi. Hebu tuwaunge mkono,” alisema Dororosa.
Ushindi wa wanafunzi wa Arusha Science sio tu umeitangaza Tanzania, bali pia umeyapiku mataifa makubwa kama Afrika Kusini, Nigeria, na Kenya. BLOOMTECH sasa inaandaa mikakati ya kushiriki mashindano ya kidunia nchini Brazili mwaka 2025, hatua ambayo inazidi kuiweka Tanzania katika ramani ya ubunifu wa kimataifa.