Tuondoe changamoto hizi katika lugha ya Kiswahili

Jambo au kitu chochote kinachopiga hatua moja kwenda nyingine, ambapo hatua inayopigwa inakuwa bora zaidi kuliko ile ya awali, aghalabu jambo au kitu hiko hakikosi changamoto.

Muda mwingine changamoto hizo ni moja ya viashiria muhimu kudhihirisha ukuaji na ustawi wa kitu husika.

Tukijiegemeza katika muktadha wa lugha ya Kiswahili, hadi kufikia hapa ilipo leo, ama kwa hakika ni hatua kubwa imepigwa ukilinganisha na wakati wa nyuma.

Hivi leo kukua kwake, imefikia hatua ya kuwa lugha ya kidunia na kuwa ndio lugha pekee kutoka Afrika, iliyopewa heshima kutoka Umoja wa Mataifa, kuwa na siku yake maalum ya kuadhimishwa.

Mbali na mafanikio hayo, lugha ya Kiswahili inakabiliwa na changamoto mbalimbali, licha ya kwamba changamoto hizo ni moja ya viashiria muhimu vya ukuaji wa lugha hii. Aidha, changamoto hizo zinajenga ukomavu wa ujasiri katika kukua na kuenea kwa Kiswahili ulimwenguni.

“Jicho la Kiswahili”, linaona kuwa changamoto hizo muda mwingine ni kikwazo kikinachokwamisha juhudi za maendeleo ya Kiswahili.

Miongoni mwa changamoto ni kasumba kutoka kwa wasomi na wanajamii. Bado kuna fikra na mitazamo hasi kuhusiana na Kiswahili, wapo wasomi na baadhi ya wanajamii wanaoamini Kiswahili ni lugha duni pia ni lugha ya watu wa daraja la chini.

Changamoto nyingine ni ujitokezaji wa ubadilishaji na uchanganyaji msimbo wakati wa mazungumzo. Kumekuwa na desturi kwa wazungumzaji wa Kiswahili, kuchanganya maneno ya Kiswahili na maneno ya lugha za kigeni hasa Kiingereza.

Mathalani, mtu anasema, ‘Ok sawa nitacomment baadaye’. Wanaofanya hivi, kwao wanaona ndio umahiri wa lugha kwani anaonekana ana uwezo wa kutumia lugha mbili wakati mmoja, bila kujua ya kwamba anakweza lugha ya kigeni na kuitweza lugha yake mama.

Changamoto nyingine ni kukosekana kwa sera au mwongozo wa matumizi ya Kiswahili katika tasnia mbalimbali ikiwemo tasnia ya habari na mawasiliano na sanaa (muziki,filamu).

 Licha ya kwamba tasnia hizi ni muhimu katika ukuzaji wa lugha, bado kuna matumizi yasiyo sahihi ya Kiswahili.

“Jicho la Kiswahili”, linapendekeza yafuatayo ili kuondokana na changamoto hizo:

Mosi, kuendelee kufanyika kwa juhudi za ukuzaji na uenezaji wa Kiswahili kwa kasi kubwa ikiwemo kutolewe kwa elimu kuhusu matumizi na maendeleo ya Kiswahili

Ninaamini hi itakuwa ni mbinu mojawapo ya kuondoa mitazamo hasi ( katika Kiswahili.

Pili, wadau wote wa Kiswahili tuondokane na utamaduni wa kutumia Kiswahili hapohapo na lugha nyingine wakati wa mazungumzo. Tusome machapisho mbalimbali ya Kiswahili ili kuwa na umilisi wa matumizi ya Kiswahili ili tusipungukiwe na maneno ya Kiswahili kiasi kwamba tukajikuta tunatumia maneno kutoka lugha za kigeni.

Tatu, kuundwe kwa sera madhubuti ya matumizi ya Kiswahili katika tasnia mbalimbali ikiwemo tasnia ya habari na mawasiliano pamoja na tasnia ya sanaa. Tasnia hizi ni muhimu katika kuunadi msamiati wa Kiswahili, ila kulingana ubanangaji wa Kiswahili unaojitokeza katika tasnia hizi, ni muhimu kuundwe kwa mwongozo kimatumizi wa Kiswahili katika tasnia hizi.

Related Posts