UDOM YAJA NA KOZI MAALUM YA KUKABILIANA NA CHANGAMOTO YA UCHELEWESHAJI WA MIRADI

 


Makamu Mkuu wa Chuo Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Prof. Lughano Kusiluka akizungumza kwenye uzinduzi wa kozi fupi ya Ufuatiliaji na Tathmini ya miradi mbalimbali leo Disemba 10,2024 uliofanyika chuoni hapo.

Na Gideon Gregory, Dodoma.

Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), kimezindua kozi fupi ya Ufuatiliaji na Tathmini ya miradi mbalimbali yenye lengo la kuisaidia Serikali kukabiliana na changamoto ya ucheleweshwaji wa kukamilisha miradi kwa wakati.

Akizungumza leo Disemba 10,2024 Jijini Dodoma mara baada ya kufungua mafunzo ya muda mfupi kwa wataalamu kutoka sekta mbalimbali toka mikoa mbalimbali ya Tanzania Bara na Zanzibar, Makamu Mkuu wa Chuo hicho Prof. Lughano Kusiluka, amesema mafunzo hayo ni muhimu katika kuhakikisha miradi inatekelezeka kwa wakati.

“Eneo la Ufuatiliaji na Tathmini ya miradi ni eneo nyeti na muhimu kuanzia hatua ya kuanza kuandika mradi hadi utekelezaji wake, ikiwemo miradi ya ujenzi wa miundombinu au utafiti”. Amesema, bila kuweka utaratibu mzuri wa usimamizi na tathmini mradi hauwezi kutekelezeka na ni hasara kwa Taifa na ndiyo sababu ya miradi mingi kushindwa kukamilika kwa wakati.

Aidha, Prof. Kusiluka amewakaribisha wasimamizi wanaokabidhiwa miradi kujiunga na kozi hiyo inatolewa na UDOM, ili kujua namna ya kukabiliana na changamoto ya usimamizi na ufuatiliaji wa miradi na kujiandaa na mbinu za kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazojitokeza wakati wa uendeshaji, ili kuwa na miradi inayotekelezeka.

“Mojawapo ya eneo linalofundishwa hapa ni kuwaangalia mradi wa aina gani, ulikuwa unahitaji kutekelezwa kwa kiasi gani na mambo gani yanatakiwa kufanyika lini na wapi ili wasimamizi wa miradi waweze kuwa na matokeo yanayotarajiwa,”amesema.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Taasisi ya Taaluma za Maendeleo UDOM Dkt. Ajali Mustafa, amesema matarajio yao kupitia kozi hiyo ni kwenda kuwatengeneza wasimamizi walio bora na watakoongoza miradi ya Serikali.

Amesema lengo la kozi hiyo ni kupeleka maarifa kwa watumishi wa taasisi za umma na binafsi huku akiongeza kuwa msukumo uliowapelekea kuanzisha kozi hiyo ni uhitaji mkubwa wa wataalamu wenye ujuzi wa usimamizi wa miradi na kwakuwa UDOM ina wataaalamu wabobevu kwenye sekta hiyo imekuwa vema kuanzisha kozi fupi ili kuwafikia walengwa.

“Hii tunaichukulia kama sehemu ya kutoa ushauri na maarifa yanayohusiana na utathmini ili kuweza kutekeleza majukumu ya taasisi mbalimbali zinazotekelezeka miradi ya maendeleo nchini,’amesema.

Naye Afisa usimamizi wa milki kutoka Shirika la Nyumba Zanzibar Bw. Juma Hassan, amesema kupitia kozi hiyo itaenda kusaidia miradi mbalimbali kukamilika kwa wakati huku akibainisha matarajio yao.

Amesema matarajio yao ni kuwa baada ya kozi hiyo washiriki wataweza kutatua changamoto nyingi zinazotokana na masuala ya Ufuatiliaji na Tathmini na hivyo kutoa ufumbuzi kwa masuala mbalimbali yanayohusu usimamizi wa miradi hususani ile ya Serikali.

Makamu Mkuu wa Chuo Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Prof. Lughano Kusiluka akizungumza kwenye uzinduzi wa kozi fupi ya Ufuatiliaji na Tathmini ya miradi mbalimbali leo Disemba 10,2024 uliofanyika chuoni hapo.

Mkurugenzi wa Taasisi ya Taaluma za Maendeleo
Chuo Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Dkt. Ajali Mustafa akimkaribisha Makamu Mkuu wa UDOM Prof. Lughano Kusiluka kwaajili ya kuzindua kozi fupi ya Ufuatiliaji na Tathmini ya miradi mbalimbali leo Disemba 10,2024 uliofanyika chuoni hapo.

Baadhi ya wataalamu kutoka katika sekta mbalimbali toka mikoa mbalimbali ya Tanzania Bara na Zanzibar walioshiriki kwenye uzinduzi wa kozi fupi ya Ufuatiliaji na Tathmini ya miradi mbalimbali leo Disemba 10,2024 yaliyofanyika katika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM).

Picha ya pamoja ya wataalamu kutoka katika sekta mbalimbali za Tanzania Bara na Zanzibar pamoja na wanafunzi walioshiriki kwenye uzinduzi wa kozi fupi ya Ufuatiliaji na Tathmini ya miradi mbalimbali leo Disemba 10,2024 uliofanyika katika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM).

Related Posts