Ugonjwa usiojulikana waikumba DRC, WHO yaanza uchunguzi

Congo DRC. Ugonjwa usiojulikana umeikumba nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) huku ukisababisha watu zaidi ya 30 kupoteza maisha hasa watoto walio chini ya miaka mitano.

Shirika la Afya Duniani (WHO) limetuma wataalamu wake nchini humo kusaidia kuchunguza ugonjwa huo mpya usioeleweka ambao una dalili za homa, maumivu ya kichwa, kikohozi, mafua na maumivu ya mwili.

WHO imesema kati ya Oktoba 24 na Desemba 5, 2024, katika eneo la Panzi jimboni Kwango, jumla ya maambukizi 406 ya ugonjwa huo yaliripotiwa huku walioambukizwa wakiripotiwa kuwa na utapiamlo mkali.

Timu za kukabiliana na magonjwa zimetumwa ili kubaini sababu huku zikichukua sampuli kwa ajili ya uchunguzi wa kimaabara kutoa maelezo ya kina zaidi ya kliniki ya kesi zilizogunduliwa, kuchunguza mienendo ya maambukizi.

“Kipaumbele chetu ni kutoa msaada kwa familia na jamii zilizoathirika. Juhudi zote zinafanyika ili kubaini sababu ya ugonjwa huu, kuelewa njia zake za maambukizi haraka iwezekanavyo,” amesema Dk Matshidiso Moeti, Mkurugenzi wa Kanda ya Afrika wa WHO.

Hata hivyo, changamoto ya kufikia eneo hilo la vijijini ni mtandao wa barabara kuwa mgumu, WHO inasema ufikiaji wa eneo athiriwa ni mgumu hasa wakati wa msimu wa mvua kwa sababu ni mbali na mjini.

Kulifikia eneo hilo kutoka mji wa Kinshasa kwa njia ya barabara inaweza kuchukua takriban saa 48. Changamoto hizo pamoja na uchunguzi mdogo uliofanyika zimechelewesha kutambua sababu kuu za ugonjwa huo.

Timu za wataalamu kwa sasa zinakusanya sampuli kwa ajili ya uchunguzi wa kimaabara, kutoa maelezo ya kina zaidi ya kliniki ya maambukizi yanayogundulika, kuchunguza mienendo ya maambukizi na kutafuta kikamilifu iwapo kutakuwa na maambukizi ya ziada, ndani ya vituo vya afya na katika ngazi ya jamii.

Hata hivyo, hii sio mara ya kwanza kwa DRC kukumbwa na maambukizi ya magonjwa sugu. Tangu 1976 nchi hiyo yenye utajiri mkubwa wa rasilimali barani Afrika, imepambana na milipuko 14 ya Ebola.

Mwaka 2024, imeathiriwa na mlipuko wa Homa ya Nyani (Mpox) ambao umeathiri zaidi ya watu 4,900 na zaidi ya 625 kufariki.

Related Posts