Njombe. Ili kumuenzi hayati Jackson Makweta, jamii mkoani hapa imetakiwa kutumia elimu, teknolojia na kukubali mabadiliko ya matumizi ya mifumo ya fedha ili kuleta matokeo chanya nchini.
Hayo yalibainishwa jana Desemba 9, 2024 wakati wa kumbukizi ya mwanazuoni, Jackson Makweta katika miaka 63 ya uhuru wa Tanzania Bara, iliyofanyika mkoani hapa kwa kushirikisha wadau mbalimbali.
Hayati Makweta aliwahi kuwa mwanazuoni na Mbunge wa Mkoa huo kwa miaka 35, tangu 1975 hadi 2010 na kuongoza katika nyadhifa mbalimbali nchini.
Mdahalo huo ulihusisha wanazuoni, viongozi mbalimbali na wananchi wa mkoa huo chini ya umoja unaoitwa Luhala, ambapo mijadala imejikita kwenye masuala ya elimu, uchumi na historia ya mkoa huo.
Alatanga Nyagawa amesema ili mkoa huo uweze kutambulika ni lazima watu wake wawe na elimu.
Amesema miongoni mwa maandiko makubwa yaliyoandikwa na watu wa mkoa huo ni pamoja na yale yaliyoandikwa na Hayati Makweta ambaye mpaka anafariki dunia, 2012 amefanikiwa kuandika zaidi ya vitabu 15 vilivyoleta mabadiliko chanya.
“Tukisema huyu siyo mtu wa kawaida kama wangekuwa Wazungu wangesema wanakaa vikao na wanamuita mtakatifu au kumjengea sanamu mahali fulani’ amesema Alatanga akielezea historia fupi na Makweta.
Amesema waliamua kuungana Watanzania wanaotoka Mkoa wa Njombe lengo ikiwa ni kutafuta watu ambao wamefanya makubwa kutoka mkoani humo kabla ya uhuru, ambapo walipata majina machache likiwemo la Makweta.
“Tangu 1961 hadi sasa kwa ngazi za Taifa za utawala kama watu wapo 100 tafiti ya kawaida iliyofanyika na Luhala kati ya makabila zaidi ya 120 ya Tanzania watu 30 au 40 watakuwa wanatoka Njombe” amesema Alatanga.
Giliad Ngewe amesema wameamua kufanya mdahalo kutokana na mkoa huo kuwa na hali ya hewa nzuri, uwepo wa madini, miundombinu mizuri na watu wake kuwa wachapa kazi licha ya kasoro ndogondogo.
Amesema kwa sasa Watanzania wengi hawana ajira na hata wanaojishughulisha na kilimo, mvua imekuwa si ya kutosha hali inayowafanya baadhi yao kushindwa kumudu gharama za maisha.
Alfred Luvanda amesema kuelekea mabadiliko ya uchumi maoni ya Hayati Makweta yalikuwa ‘uongozi madhubuti na ushirikishwaji ndiyo msingi wa maendeleo katika awamu sita’.