Waomba huduma ya msaada wa kisheria bure iwe endelevu

Musoma. Wakazi wa Manispaa ya Musoma mkoani Mara wameiomba Serikali kuweka utaratibu maalumu utakaowezesha wananchi kupata huduma za kisheria wakati wote, hasa kwa wale wenye kipato cha chini.

Maombi ya wananchi hao  yamekuja siku moja kabla ya kuanza kwa utoaji huduma za msaada wa kisheria kupitia kampeni maalumu ya ‘Mama Samia legal aid’ unaotarajiwa kuanza kesho mkoani Mara.

Wakizungumza mjini Musoma leo Desemba 10,2024 wakazi hao wamesema kupatikana kwa huduma hizo katika mazingira rafiki kwa wananchi wenye kipato cha chini, kutasaidia kwa kiwango kikubwa kumaliza changamoto zao hasa suala la migogoro ya ardhi.

“Tumeshuhudia migogoro mingi katika jamii mfano inayohusu masuala ya ardhi na ukichunguza vizuri utabaini wengi wanaoathiriwa nayo ni wasiokuwa na  uwezo wa kupata huduma za kisheria, kutokana na sababu mbalimbali kubwa ikiwa ni ukosefu wa fedha kwa ajili ya kuwalipa wanasheria,” amesema Joab Magori.

Magori amesema ipo haja ya Serikali kuangalia namna ya kuwawezesha wananchi kupata huduma hizo za kisheria kwa gharama nafuu, hatua ambayo anaamini itakuwa na mchango chanya katika kutatua migogoro mingi kwenye jamii.

“Hii kampeni ni nzuri lakini sio suluhisho la kudumu juu ya uhitaji wa huduma za kisheria kwa wananchi kwani inatolewa mara moja, wakati wananchi wana uhitaji wa huduma hizo kila siku hivyo naomba ikiwezekana kuwe na  kitengo cha wanasheria katika ofisi za kata hata vijiji ili kuwasaidia wananchi hukohuko katika maeneo yao,” amesema Anna Makilagi.

Makilagi amependekeza Serikali kuanza kuajiri wataalamu wa sheria ngazi za kata na vijiji ili iwe rahisi kutoa huduma kwa wananchi, tofauti na ilivyo sasa huduma hizo mara nyingi hutolewa kwa gharama kubwa kupitia wanasheria wa ofisi binafsi.

Akitoa taarifa kwa waandishi wa habari juu ya kuanza kwa kampeni hiyo mkoani Mara, Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara, Gerald Kusaya amesema wakazi wa vijiji na mitaa 270 katika kata 90 mkoani Mara wanatarajiwa kupata huduma hizo za msaada wa kisheria.

Kusaya amesema kampeni hiyo inatarajiwa kuanza katika mkoa wa Mara Desemba 11 hadi 20 mwaka huu, huku akiwataka wananchi kutumia fursa hiyo kupata msaada wa kisheria ambao utatolewa bila malipo na wataalamu hao katika kipindi hicho.

Amesema wakazi wa mkoa wa Mara wana uhitaji mkubwa wa masuala ya kisheria hivyo ujio wa wataalamu hao utakuwa sehemu ya suluhisho la changamoto hiyo.

“Mkuu wa Mkoa wa Mara, Evans Mtambi ameanzisha utaratibu wa kusikiliza kero za wananchi kila Jumanne na Ijumaa, na tumebaini kuwa asilimia kubwa ya wananchi wanaokuja kuonana na kiongozi huyo wana uhitaji wa msaada wa kisheria.

“Hii inatokana na sababu nyingi ikiwepo kutokuwa na elimu ya kutosha juu ya masuala ya kisheria pamoja na kukosa namna ya kuwafikia wanasheria kwa maana ya gharama na mambo mengine,” amesema Kusaya

Kusaya amesema utekelezaji wa kampeni hiyo ni sehemu ya utimizaji wa wajibu wa Serikali kwa wananchi.

Mratibu wa kampeni hiyo kutoka Wizara ya Sheria na Katiba, Laurent Burilo amesema kampeni hiyo iliyoanza Machi mwaka jana hadi sasa imefika katika mikoa saba nchini. Amesema katika mikoa hiyo zaidi ya wananchi 490,000 wamefikiwa ambapo migogoro 670 kati ya 5,000 iliyowasilishwa na wananchi hao ilitatuliwa papo hapo.

“Kampeni hii inalenga kutoa huduma za msaada wa kisheria katika masuala mbalimbali ikiwepo migogoro ya ardhi, ukatili wa kijinsia, mirathi, ndoa, jinai madai na mambo mengine, mengi huku walengwa zaidi wakiwa ni wananchi wa kipato cha chini,”amesema

Wakili wa Serikali kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Joyce Mushi amesema mbali na huduma za msaada wa kisheria kampeni hiyo pia itahusika na utoaji wa elimu kwa viongozi hasa wa serikali za mitaa kuhusu suala la uongozi na utawala bora pamoja na uraia.

Related Posts