KOMBAINI ya Dar Kings imeanza kwa kishindo Ligi ya TCA U-17 kwa kuisambaratisha Arusha Kings kwa mikimbio 162 katika viwanja vya UDSM, jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa Msemaji wa Chama cha Kriket nchini (TCA) waandaaji wa ligi hiyo, Ateef Salim, michuano hiyo ambayo inafanyika pia katika viwanja vya Leaders Club, inashirikisha timu za kombaini kutoka mikoa mbalimbali ya Tanzania.
Dar Kings ndio walioshinda kura ya kuanza kubeti na kutengeneza mikimbio 249, huku wakipoteza wiketi nne hadi mwisho wa mizunguko 30 ya mchezo huo, huku Arusha Kings kutolewa wakiwa wamefikisha mikimbio 87 na mizunguko 21 kati ya 30.
Johnson David wa Dar Kings aliyetengeneza mikimbio 110 kutokana na mipira 86, ndiye alikuwa shujaa wa mchezo akisindikizwa na Ayaan Ashik aliyetengeneza mikimbio 77, huku Rehaan Atif akijazia 15.
Licha ya Arusha kupoteza, John Frank alipata wiketi tatu kati ya nne, wakati Daniel Michael alipata wiketi moja.
Mchezo mwingine, Combined Kings iiliishinda Morogoro Kings kwa wiketi sita katika mchezo wa mizunguko 30.
Morogoro Kings ndio waliopata kura ya kuanza kubeti na jitihada zao ziligota kwenye mikimbio 132 baada ya kupoteza wiketi tisa hadi mwisho wa mizunguko 30, huku Combined Kings ikipata mikimbio 133 kwa mizunguko 27 na kupoteza wiketi nne.
“Ni ligi nzuri kwa vijana wetu kwa sababu inawaleta pamoja wachezaji wote wa kriketi kutoka mikoa mbalimbali ya Tanzania,” alisema Ateef Salim huku akiwataka wapenzi wa kriketi nchini kuendelea kuwaunga mkono vijana hawa ili mchezo huo uzidi kusonga mbele.
Katika michuano hiyo, baadhi ya wachezaji walitia fora kwa kuonyesha vipaji na katika viwanja vya UDSM, mpigaji (batsman) kutoka Arusha Kings, John Frank baada ya kuiwezesha timu yake kuifunga United Kings kwa wiketi nne.
Frank alipiga mikimbio sita mara tatu (pigo moja lenye usawa wa mikimbio sira) hivyo kutengeneza mikimbio 18 kwa mapigo matatu tu.
Shaaban Hamisi wa Morogoro Kings aliiwezesha timu yake kuifunga United Kings kwa mikimbio 120 baada ya kutengeneza mikimbio 58 kutokana na mipira 48.
Arafat Abdul wa Gairo Kings aliisaidia timu yake kuifunga Tanga Kings kwa wiketi sita baada ya kutengeneza mikimbio mitatu mara 15 kwa kutumia mipira 33 tu.
Rehaan Atif wa Dar Kings aliyepiga mapigo ya mikimbio mitatu mara 14 kwa kutumia mipira 12 tu, aliiwezesha timu yake kuishinda Combined Kings kwa mikimbio 106, huku akitengeneza hat-trick ya kwanza ya mashindano.
Wengine walioonyesha ujasiri mkubwa ni Zawadi Mahelela wa United Kings aliyepiga mikimbio sita mara 20 kwa kutumia mipira 36 na Joseph Stefano Marusu pia wa United Kings aliyepiga mikimbio mitano mara 18 kwa kutumia mipira 21 katika mechi dhidi ya Arusha Kings.
“Vijana hawa ni tumaini la taifa kwa siku zijazo, hivyo, wanahitaji kusaidiwa zaidi ili wafiker mbali,” alisema Ateef.