Dodoma. Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango amelitaka Shirika la Watumishi Housing Investiment (WHI) kuhakikisha nyumba zinazojengwa zinazingatia ubora na viwango stahiki ili kuendana na thamani ya fedha na hivyo kuwaepushia wanunuzi gharama za marekebisho na maboresho.
Mbali na hilo, Dk Mpango ameonya watumishi wenye uwezo kutowatumia wale wa kawaida katika kupata nyumba hizo.
Dk Mpango ameyasema hayo leo wakati akizindua Mpango wa Makazi kwa Watumishi wa Umma unaotekelezwa na WHI ambapo nyumba 2100 zitajengwa hadi kufikia mwaka 2027 kwa gharama ya Sh169 bilioni.
Akizungumza amesema ili mpango huu uweze kufikia malengo yake na kuwa na manufaa kwa watumishi, ni muhimu vigezo na masharti ya upatikanaji wa nyumba kwa watumishi wa umma viheshimiwe na kuzingatiwa.
Amesema upokeaji, uchambuzi wa maombi na uthamini wa nyumba hizo vifanyike kwa haki na kuzingatia uhalisia.
“Juhudi za makusudi zifanyike ili watumishi wa ngazi za chini na kati wapewe kipaumbele katika upatikanaji wa nyumba hizo na watumishi wenye uwezo wasiwatumie watumishi wa kawaida kupata nyumba hizo,” amesema makamu huyo wa Rais.
Amesema anatambua changamoto kubwa ya upatikanaji wa viwanja vya kutosha katika maeneo mengi, hususan maeneo ya mijini.
Ili kuufanya mpango huo kuwa endelevu, Dk Mpango ameshauri Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma kwa kushirikiana na Wizara ya Ardhi na Halmashauri husika kufanyia kazi suala la changamoto ya viwanja kwa ili kuhakikisha upatikanaji wa maeneo ya ujenzi wa nyumba za watumishi yaliyo karibu zaidi na sehemu za kazi.
Amesema maeneo hayo yazingatie mahitaji ya msingi ya watumishi na familia zao, hivi sasa na kwa wakati ujao.
“Napenda kusisitiza kuwa nyumba zinazojengwa na Watumishi Housing Investments, lazima zizingatie ubora na viwango stahiki ili kuendana na thamani ya fedha na kuwaepushia wanunuzi wa nyumba hizo gharama za marekebisho na maboresho zaidi,” amesema.
Aidha, Dk Mpango ametoa rai kwa watumishi na wananchi ambao watapata nafasi ya kununua nyumba hizo kuzitunza ili zibaki katika hali ya ubora kadri inavyowezekana.
Amewataka pia kuangalia uwezekano wa kushirikisha taasisi au watu binafsi wenye utaalam wa kupendezesha makazi.
Dk Mpango amesema Hospitali ya Benjamin Mkapa ambayo iko jirani na Njedengwa ina uhaba wa nyumba za makazi kwa ajili ya madaktari na wauguzi na kuwaelekeza Watumishi Housing Investments, kutoa kipaumbele kwa watumishi wa hospitali wataonyesha nia ya kuzinunua zile zitakazoendelea kujengwa Dodoma.
Amesema kwa kuwa mahitaji ya nyumba nchini bado ni makubwa, ameielekeza Ofisi ya Rais-Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora sambamba na Watumishi Housing Investments kutafuta vyanzo vingine vya fedha kwa ajili ya upanuzi wa mradi huo.
Awali, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene alisema mpaka sasa WHI imetumia takribani Sh87.97 bilioni kwa ajili ya kujenga nyumba 1,006 katika mikoa 19.
Amesema mpango wa sasa ni kujenga nyumba 5,000 nchi zima lengo likiwa ni kuhakikisha watumishi wa umma wanapata makazi kwa bei nafuu.
Aidha, Simbachawene ameshauri WHI kufanya mazungumzo na kuingia makubaliano na Ofisi ya Rais-Tamisemi kuangalia namna ya kujenga nyumba katika shule na vituo vya kutolea huduma za afya.
Mwenyekiti wa Bodi ya WHI, Abdul-Razaq Badru alisema Shirika hilo linakabiliwa na changamoto ya mtaji ambao utawezesha kujenga nyumba nyingi za bei nafuu kwa watumishi wa umma.
Ameomba Serikali kuiruhusu kukopa katika masoko ya ndani na nje ambayo inatoa mikopo yenye riba nafuu na ambayo inalipwa kwa muda mrefu.
“Kwa sasa Watumishi Housing Invetment haina deni, hivyo itakuwa na nafasi nzuri ya kukopa, tunaiomba Serikali ituruhusu tuweze kukopa kwenye masoko yenye riba ndogo na itakayoripwa kwa muda mrefu ili tuongeze kasi ya kujenga nyumba kwa watumishi wa umma na wazipate kwa bei nafuu,” amesema.
Naye Mkurugenzi wa Watumishi Housing Investiment, Dk Fred Msemwa amesema tangu kuanzishwa kwa shirika hilo mwaka 2014 tayari zaidi ya familia 1,000 za watumishi wa umma zimepata makazi katika mikoa 19.
Amesema pia kati ya mwaka 2015 hadi 2020, WHI ilijenga nyumba za walimu katika shule za kata 186 zilizoko katika wilaya 31 na kusisitiza kuwa bei ya nyumba wanazojenga ni kati ya asilimia 10 na 30 ikilinganishwa na bei za soko.