Musoma. Mfanyakazi wa ndani aliyefahamika kwa jina moja la Modesta (17), amefariki dunia baada ya kudaiwa kujinyonga, huku chanzo cha tukio hilo kikihusishwa na msongo wa mawazo.
Tukio hilo limetokea jana Desemba 10, 2024 katika mtaa wa Zanzibar katika Manispaa ya Musoma majira ya saa 5 asubuhi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Pius Lutumo amesema leo Desemba 11, 2024 kuwa mwili wa binti huyo ulikutwa ukiwa unaning’inia kwenye kenchi la paa ya chumba alimokuwa akilala binti huyo enzi za uhai wake.
“Huyu binti alikutwa amefariki kwa kujinyonga kwa kutumia kamba ya kufungia mbuzi na mwili wake ulikutwa ukiwa umening’inia kwenye kenchi la paa ya chumba chake,” amesema Kamanda Lutumo.
Amesema Jeshi la Polisi limeanza kufanya uchunguzi juu ya chanzo cha tukio hilo huku uchunguzi wa awali ukionyesha chanzo cha tukio hilo ni msongo wa mawazo ingawa hakutoa ufafanuzi zaidi na kutoa wito kwa jamii kuacha kujichukulia hatua mkononi badala yake kuwa huru na kushirikisha wengine hasa katika changamoto za msongo wa mawazo.
Akisimulia namna tukio lilivyotokea, shuhuda wa tukio hilo ambaye pia ni mtoto wa bosi wa marehemu, Goodluck Kahaya amesema muda mfupi kabla ya tukio hilo alikuwa nyumbani yeye pamoja na binti huyo na hapakuwa na ugomvi na kwamba binti huyo alikuwa katika hali ya kawaida kama ilivyokuwa siku zote.
“Niliondoka kwenda kukatia mifugo majani nikamuacha dada akiwa anaosha vyombo baada ya kumaliza kukata majani, nikarudi nyumbani ila nikashangaa kukuta mlango umefungwa kwa ndani. Nilipojaribu kugonga pakawa kimya nikasubiri kwa muda bila mafanikio nilipoona hivyo nikatafuta msumari nilioingiza kwenye tundu la ufunguo na ufunguo ukadondoka nikauvuta nikafungua mlango,” amesimulia.
Amefafanua baada ya kufanikiwa kufungua mlango na kuingia ndani hakumkuta dada na kumuita bila mafanikio ndipo alipoamua kuingia chumbani kwake na kukuta mwili wake ukiwa unaning’inia huku akiwa tayari amefariki.
Bosi wa binti huyo, Mary Urono amesema ameishi na binti kwa muda wa mwaka mmoja kama mfanyakazi wake wa ndani na kwamba mwezi Novemba mwaka huu binti huyo aliomba ruhusa ya kwenda nyumbani kwao Katoro mkoani Geita kwaajili ya kusalimia wazazi.
“Tangu amerudi kutoka likizo ana wiki mbili sasa na toka nimeishi naye na hata alipotoka kwao hakuwahi kuniambia kama kuna changamoto yoyote, alikuwa binti mzuri alikuwa mtiifu sana ukimwambia kitu anafanya kwa wakati bila shida yoyote alikuwa kama mwanangu, nashangaa leo hii ameniacha katika mazingira ya kutatanisha,” amesema Marry.
Amesema siku ya tukio akiwa anajiandaa kwenda kazini, binti huyo alimsihi asiondoke bila kupata kifungua kinywa kwa sababu alikuwa amechelewa na alipokataa, binti alimsisitiza kuwa lazima amuandalie na akafanikiwa kumuandalia kifungua kinywa baadaye ndipo alipoondoka kwenda kazini kabla ya kupigiwa simu saa 7 mchana kujulishwa kuhusu tukio hilo.
Annasatazia Athumani ambaye alikuwa rafiki wa binti huyo amesema binti huyo aliwahi kumwambia kuwa anaweza kufa siku yoyote kutokana na changamoto za nyumbani kwao huko Katoro.
“Huyu binti alikuwa rafiki yangu na tulikuwa tukisali pamoja, ila mara nyingi alikuwa akilalamika kuhusu pesa zake za mshahara kwani alikuwa akipokea mshahara wake yeye alikuwa akituma nyumbani kwao ila anadai mama yake badala ya kutunza zile fedha alikuwa anazitumia kunywea pombe kwakweli hilo jambo lilikuwa likimsumbua sana lakini nilikuwa namshauri asifikie hatua ya kujiua,” amesema.