Hukumu anayedaiwa kuua, kuteketeza mwili wa mkewe Februari mwakani

Dar es Salaam. Wakati Serikali ikiomba kuongezewa muda wa kuwasilisha hoja za mwisho katika kesi ya mauaji dhidi ya mfanyabiashara Hamisi Luwongo, anayedaiwa kumuua mkewe na kisha kuuteketeza mwili wake kwa moto, Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam imepanga kutoa hukumu Februari 26, 2025.

Jaji Hamidu Mwanga anayesikiliza kesi hiyo amepanga tarehe hiyo ya hukumu leo Jumatano Desemba 11, 2024, huku akiridhia maombi ya upande wa mashtaka kuongezewa muda wa kuwasilisha hoja za mwisho baada ya kukamilisha usikilizwaji wa ushahidi wa pande zote.

Novemba 25, 2024 Mahakama iliamuru pande zote kufikia Desemba 10, ziwe zimeshawasilisha majumuisho ya hoja kwa lengo la kuishawishi mahakama kuwa mshtakiwa ana hatia au hana hatia, na ikapanga kesi hiyo itajwe leo Desemba 11 kwa ajili ya kupanga tarehe ya hukumu.

Kesi hiyo ilipoitwa leo, upande wa mashtaka kupitia Wakili wa Serikali, Cuthbert Mbilinyi umeieleza mahakama haukuweza kuwasilisha majumuisho ya hoja kwa kuwa kompyuta iliyokuwa ikitumika ilipata tatizo, akaomba waongezwe muda wa kuwasilisha hoja hizo mpaka Desemba 24.

Wakili wa utetezi, Hilda Mushi ameieleza mahakama wameshawasilisha majumuisho ya hoja zao ndani ya muda uliotolewa na mahakama, akipinga maombi ya upande wa mashtaka kuongezewa muda.

Amesema mahakama ilitoa muda wa siku 14 kwa pande zote kuwasilisha hoja za mwisho na kwamba, upande wa mashtaka haujaieleza mahakama ni lini tatizo la kompyuta lilitokea mpaka wakashindwa kutekeleza amri ya mahakama. Ameiomba mahakama isikubali ombi hilo badala yake ipange tarehe ya hukumu kama ilivyokuwa imeelekeza.

Jaji Mwanga amemuomba Wakili Mushi akubali upande wa mashtaka kuongezewa muda. Amesema hoja hizo zinaweza kuisaidia mahakama na kwa kuwa mahakama inakwenda likizo (kuanzia Desemba 15 mpaka Februari 2025), basi kwa vyovyote hukumu itakuwa baada ya mapumziko ya mahakama.

“Ninakubaliana na maombi ya upande wa mashtaka kuongezewa muda. Kwa hiyo, upande wa mashtaka utawasilisha hoja za mwisho Desemba 24, 2024 na hukumu itakuwa Februari 26, 2025, saa 8.30 mchana,” amesema.

Kabla ya kesi hiyo kuahirishwa, mshtakiwa Hamisi alinyoosha mkono juu akiomba nafasi ya kuzungumza. Aliporuhusiwa ameulaumu upande wa mashtaka kwa kushindwa kuwasilisha hoja kwa wakati akidai umefanya uzembe.

Jaji Mwanga amemkatiza, akimtuliza asiwe na wasiwasi. Amefafanua kuwa, kutokana na asili ya kesi hiyo ni jambo la muhimu kwa upande wa mashtaka kupewa nafasi na hakuna ushahidi mpya utakaowasilishwa.

Katika kesi hiyo ya jinai namba 44/2023, Hamisi, mkazi wa Gezaulole, wilayani Kigamboni, Dar es Salaam anakabiliwa na shtaka la mauaji ya mkewe Naomi Marijani kinyume cha kifungu cha 196 na 197 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, kama ilivyorejewa mwaka 2019.

Anadaiwa alimuua mkewe Mei 15, 2019 nyumbani kwao kisha akauchoma mwili wake kwa moto kwa kutumia magunia mawili ya mkaa ndani ya banda la kuku, baadaye akaenda kuzika masalia ya mwili huo na majivu shambani kwake na kupanda migomba juu yake.

Upande wa mashtaka ulifunga ushahidi Novemba 18, 2024 baada ya kuwaita mashahidi 14 na kuwasilisha vielelezo tisa, huku upande wa utetezi ukiufunga Novemba 19 baada ya kumuita shahidi mmoja ambaye ni mshtakiwa mwenyewe, bila kuwasilisha kielelezo chochote.

Mshtakiwa katika utetezi alikana kumuua mkewe akidai hajafa bali alitoroka na kwamba, taarifa alizowaeleza Polisi kuwa alimuua na kuchoma moto mwili wake akazika majivu na masalia yake shambani hazikuwa za kweli.

Alidai aliwadanganya ili kujinusuru na mateso ya kipigo kutoka kwa askari polisi waliomtaka awaonyeshe iliko maiti ya mkewe.

Mshtakiwa alieleza hata masalia ya mifupa aliyowaonyesha polisi shambani kwake si ya mkewe bali ni ya mzoga alioukuta wakati akisafisa shamba lake na mingine ilisalia kwenye kaburi lililohamishwa kwenye shamba lingine alilonunua eneo la Mwongozo, Kigamboni.

Alidai mifupa iliyofukuliwa na mafundi waliokuwa wakichimba udongo kutengeneza msingi wa nyumba aliyokuwa akiijenga, aliichukua na kwenda nayo shambani akaiweka pamoja na ya mzoga kisha akaichoma pamoja na takataka nyingine.

Alidai ndiyo maana hata uchunguzi wa kisayansi uliofanywa na Mkemia Mkuu wa Serikali matokeo yake hayakutoa uthibisho kuwa ni ya mkewe Naomi.

Upande wa mashtaka baada ya mshtakiwa kumaliza utetezi, uliiomba mahakama iamuru daktari bingwa wa magonjwa ya akili kutoka Hospitali ya Taifa ya Afya ya Akili Mirembe, Dk Sadiki Mandari aitwe.

Dk Mandari ambaye pia ni Mkurugenzi wa Huduma za Tiba ndiye aliyemfanyia mshtakiwa uchunguzi wa afya ya akili kwa amri ya mahakama.

Katika ripoti ya uchunguzi wa afya ya akili ya mshtakiwa iliyowasilishwa mahakamani ilionyesha wakati wa tukio la mauaji anayodaiwa kutenda mshtakiwa alikuwa na tatizo la kiakili.

Upande wa mashtaka uliiomba mahakama daktari huyo aitwe kizimbani kwa ajili ya kumfanyia mahojiano kuhusu ripoti hiyo. Jaji Mwanga alikubali ombi hilo na akuamuru afike mahakamani kuhojiwa Novemba 25.

Alipohojiwa na mawakili wa pande zote kuhusu ripoti hiyo, Dk Mandari aliikana akidai haitambui, akiwasilisha nyingine inayoeleza wakati mshtakiwa akitenda kosa hilo hakuwa na tatizo la kiakili bali alikuwa na akili timamu.

Jaji Mwanga alionyesha kukasirishwa na hilo akahoji kwa nini mtaalamu kama yeye awasilishe mahakamani ripoti mbili tofauti katika kesi nyeti kama hiyo inayohusu maisha ya watu. Mshtakiwa alidai daktari huyo ameiaibisha taasisi yake.

Dk Mandari alipobanwa kwa maswali alisema kuna mmoja wa ndugu wa mshtakiwa alimpigia aende aitetee ripoti iliyoko mahakamani.

Alipoulizwa na Jaji kama alimweleza huyo ndugu wa mshtakiwa kuwa anakwenda na ripoti nyingine alijibu hakumwambia, alipoulizwa iwapo huyo ndugu wa mshtakiwa alijuaje kama anakwenda na ripoti nyingine alijibu hajui.

Related Posts