Iran yazishutumu Israel, Marekani kwa anguko la Assad – DW – 11.12.2024

Ayatullah Khamenei, ambaye ndiye mwenye nguvu kubwa kisiasa nchini Iran, alisema siku ya Jumatano (Disemba 11) kwamba nchi yake ina ushahidi unaothibitisha kwamba kupinduliwa kwa Rais Assad wa Syria ulikuwa mpango wa Israel, Marekani na jirani mmoja wa Syria, ambaye hakumtaja. 

Wachambuzi wanasema nchi hiyo huenda ikawa ni Uturuki, ambayo imekuwa ikipambana na wale inaowaita magaidi kwenye mpaka wake na Syria kwa miaka mingi sasa.

Soma zaidi: Mohammed al-Bashir kiongozi wa mpito Syria

Iran, ambayo ilikuwa mshirika mkubwa wa utawala wa Assad, inatajwa kuwa mmoja wapo wa waathirika wakubwa wa kuporomoshwa kwa utawala huo, hasa kupitia kile kiitwacho Muungano wa Mapambano, ambao unaongozwa na taifa hilo la Ghuba ya Uajemi na ukizijumuisha Yemen, Syria, makundi ya Hizbullah nchini Lebanon na Hamas katika Ukanda wa Gaza.

“Anayedhani kuwa kudhoofika kwa Muungano wa Mapambano kutaidhoofisha Iran, atakuwa hajajuwa kabisa maana ya mapambano.” Alisema kiongozi huyo wa Iran.

Marekani, Uturuki kuzungumzia Syria

Kwa upande mwengine, Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Marekani, Antony Blinken, anatazamiwa kuwasili nchini Uturuki kukutana na mwenzake wa Ankara, Hakan Fidan, siku ya Ijumaa (Disemba 13). 

Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Marekani, Antony Blinken.
Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Marekani, Antony Blinken.Picha: Florion Goga/REUTERS

Chanzo kimoja kutoka wizara ya mambo ya kigeni ya Uturuki kilisema hivi leo kwamba lengo la ziara ya Blinken ni kuzungumzia hali ya Syria baada ya kupinduliwa kwa Assad. 

Soma zaidi: Vikosi vya Israel vyakaribia mji mkuu wa Syria, Damascus

Chanzo hicho hakikueleza undani wa mazungumzo kati ya pande hizo mbili, lakini kauli za awali kutoka utawala wa Rais Joe Biden unaomaliza muda wake zinaashiria kuwa Washington inataka kuhakikisha utawala mpya wa Syria hautakuwa na mafungamano wa maadui wa Marekani na Israel kwenye eneo hilo la Mashariki ya Kati. 

Israel yaishambulia Syria

Israel yenyewe ilitangaza kufanya mashambulizi ya anga dhidi ya vituo vya kijeshi vya Syria, ambavyo wanajeshi wake walivikimbia kufuatia kusonga mbele kwa waasi wiki mbili zilizopita.

Muhammad al-Bashir
Muhammad al-Bashir, kiongozi wa waasi aliyegeuka kuwa waziri mkuu wa mpito wa Syria.Picha: AL ARABIYA TV/Handout/REUTERS

Jeshi la Israel lilisema limeshambulia maghala ya kimkakati ya silaha ndani ya masaa 48 yaliyopita. 

Soma zaidi: Israel yashambulia maeneo 350 ya kijeshi nchini Syria

Waziri wake wa ulinzi, Israel Katz, amesema mashambulizi yao yanadhamiria kuanzisha eneo la kujilinda kusini mwa Syria ambalo litasimamiwa bila kuwapo wanajeshi wa kudumu kwenye ardhi ya Syria.

Verdi yaonya dhidi ya kuwarejesha Wasyria kwao

Hayo yakiendelea, umoja wa vyama vya wafanyakazi nchini Ujerumani, Verdi, umeonya dhidi ya hatua ya kuwarejesha nyumbani maelfu ya Wasyria kufuatia kupinduliwa kwa Bashar al-Assad.

Syria | Israel Latakia
Mashambulizi ya Israel kwenye bandari ya Latakia nchini SyriaPicha: BILAL ALHAMMOUD/Middle East Images/AFP/Getty Images

Kupitia mahojiano yake na shirika la habari la Ujerumani (dpa), mkuu wa umoja huo, Frank Werneke, amesema kwamba kuwafukuza Wasyria ni kinyume na maslahi yao na pia kinyume na maslahi ya soko la ajira ndani ya Ujerumani yenyewe.

Soma zaidi: Majadiliano ya kukabidhiana madaraka yaanza Syria

Badala yake, mkuu huyo wa wafanyakazi ameitaka serikali ya Ujerumani na za Umoja wa Ulaya kwa ujumla kuchukuwa tahadhari kutokana na kile kinachoonekana kuwa ni wimbi la hatua dhidi ya wahamiaji kutoka Syria.

Vyanzo: dpa, AFP, AP

Related Posts