Israel Mwenda kutua Yanga lilikuwa suala la muda tu

ZIKIWA zimesalia siku nne kabla ya dirisha dogo la usajili kufunguliwa Desemba 15 mwaka huu, Yanga imemtambulisha beki wa kulia, Israel Mwenda kuwa usajili wao wa kwanza.

Mwenda mwenye uwezo pia wa kucheza beki wa kushoto na winga, anatua Yanga kwa mkopo hadi mwisho wa msimu huu akitokea Singida Black Stars ambayo alijiunga nayo dirisha kubwa la usajili msimu huu.

Inaelezwa kwamba, nyota huyo aliyewahi kuichezea Alliance FC na KMC, kwa muda mrefu alikuwa akihitajika na Yanga tangu akiwa anaitumikia Simba kabla ya kutua Singida Black Stars katika dirisha kubwa la msimu huu.

Mtu wa karibu na mchezaji huyo, ameliambia Mwanaspoti kwamba, Mwenda ambaye aliitumikia Simba kwa misimu mitatu, alihitajika na Yanga mwanzoni mwa msimu huu lakini ugumu uliokuwepo ukalifanya dili hilo kutofanyika

“Ni kama Yanga imefanikisha kile ilichokuwa inakitaka kwa muda mrefu katika usajili huu wa Mwenda ambaye ilipata ugumu wa kumchukua pindi alipokuwa Simba,” amesema mtoa taarifa huyo na kuongeza.

“Baada ya Yanga kuona ugumu huo, ikasubiri Mwenda aondoke Simba kwenda timu yoyote ili imsajili kutokea huko ndipo akatua Singida ambapo unaona imekuwa rahisi kwake kukamilisha huo usajili kipindi hiki.”

Miaka mitatu ya Mwenda ndani ya Simba, ilikuwa na changamoto kwake ya kupata namba mbele ya Shomari Kapombe upande wa beki wa kulia.

Licha ya kupata changamoto hiyo ya namba, lakini kila alipopewa nafasi alionyesha uwezo mkubwa ambao leo hii umewafanya Yanga kumsajili.

Ikumbukwe kwamba, Mwenda ndani ya Singida Black Stars, pia hakuwa na wakati mzuri kwani nafasi ya beki wa kulia alikutana na changamoto ya namba mbele ya Ande Koffi Cirille.

Lakini pia upande wa kushoto ambapo Mwenda anaweza kucheza, kuna Ibrahim Imoro, hivyo kuifanya nafasi yake ya kucheza kuwa finyu chini ya Kocha Patrick Aussems ambaye ameondolewa Novemba 29, mwaka huu.

Mwenda ambaye ni usajili wa kwanza kwa Kocha Sead Ramovic, inaelezwa anakwenda Yanga kuwa mbadala wa Yao Kouassi mwenye changamoto ya majeraha ya mara kwa mara tangu kuanza kwa msimu huu.

Lakini pia nyota huyo ana uwezo wa kucheza beki wa kushoto hivyo katika kikosi cha Yanga anaweza kucheza pindi akikosekana Chadrack Boka.

Related Posts