Katiba ya Zanzibar inavyokinzana na ya JMT

Kimataifa, Tanzania ni nchi moja inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye ni mkuu wa nchi, mkuu wa Serikali na Amiri Jeshi Mkuu.

Lakini kitaifa, Tanzania ni nchi moja yenye Katiba mbili, Katiba ya Jamhuri ya Muungano Tanzania na Katiba ya Zanzibar, yenye marais wawili, Rais wa JMT na Rais wa Zanzibar, yenye mabunge mawili, Bunge la JMT na Baraza la Wawakilishi, yenye Mahakama mbili, Mahakama Kuu ya JMT, na Mahakama Kuu ya Zanzibar.

Japo muungano wetu adhimu na adimu ni muungano wenye nchi mbili zenye haki sawa na hadhi sawa ndani ya muungano, licha ya ukubwa wa eneo la mshirika mmoja Tanzania Bara na udogo wa eneo la mshirika mwingine, Zanzibar, Katiba ya JMT, ndiyo Katiba mama na inaitambua Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984.

Katiba hiyo ya Zanzibar ilifanyiwa marekebisho makubwa na kutoa toleo la mwaka 2010, lakini mpaka hivi leo ninapoandika hapa, Katiba ya JMT, imegoma katakata kuyatambua marekebisho hayo ya Katiba ya Zanzibar na mpaka hii leo, bado Katiba yetu hailitambui toleo la mwaka 2010 la Katiba ya Zanzibar iliyounda Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) kutokana na baadhi ya vipengele vya Katiba ya Zanzibar kukinzana na Katiba ya JMT.

Ibara ya kwanza ya Katiba ya JMT inasema: “Tanzania ni nchi moja na ni Jamhuri ya Muungano.”

Ibara ya pili inasema: (1) Eneo la Jamhuri ya Muungano ni eneo lote la Tanzania Bara na eneo lote la Tanzania Zanzibar, na ni pamoja na sehemu yake ya bahari ambayo Tanzania inapakana nayo.

Ibara kwanza ya Katiba ya Zanzibar inasema: “Zanzibar ni nchi ambayo eneo la mipaka yake ni eneo lote la Visiwa vya Unguja na Pemba pamoja na Visiwa vidogo vilivyoizunguka na bahari yake ambayo kabla ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ikiitwa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar.”

Ibara ya pili inasema: “Zanzibar ni miongoni mwa nchi mbili zinazounda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Hizi ibara mbili tu za kwanza, siyo tu zimevunja Katiba ya JMT, bali zimefanya kosa kubwa la uhaini kuivunja JMT ndani ya nchi mbili. Kabla ya muungano wetu adhimu, tulikuwa na nchi mbili za Tanganyika na Zanzibar, muungano wetu ni muungano wa “union”, kwa nchi mbili kuungana na kuwa nchi moja. Nchi ya Zanzibar na nchi ya Tanganyika, zote zilikufa na kuunda nchi moja ya JMT.

Kitendo cha Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 inatamka kwamba Zanzibar ni nchi na inatamka mipaka ya eneo lake Katika Ibara ya kwanza inayosema: “Zanzibar ni nchi ambayo eneo la mipaka yake ni eneo lote la Visiwa vya Unguja na Pemba pamoja na Visiwa vidogo vilivyoizunguka na bahari yake ambayo kabla ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ikiitwa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar.”

Wakati Katiba ya JMT imeitangaza Tanzania ni nchi moja ya JMT na kutaja eneo la JMT ni eneo lote la Tanzania Bara na eneo lote la Tanzania Zanzibar, na ni pamoja na sehemu yake ya bahari ambayo Tanzania inapakana nayo. Huu ni mkanganyiko.

Hapa Zanzibar imejitangaza kama nchi, tangazo hili ni kama kuvunja muungano.

Wakati haya yakifanyika, nchi ilikuwa chini ya Rais Jakaya Kikwete, mtu rahimu sana, aliamua kunyamaza kimya bila kuingilia kwa hoja kuwa hayo ni mambo ya ndani ya Zanzibar, kilichofanyika ni kwa Katiba ya JMT, kuyapuuza mabadiliko hayo ya Katiba ya Zanzibar kwa Katiba ya JMT kutofanyiwa mabadiliko, hivyo mpaka leo Katiba ya Zanzibar haitambuliwi na Katiba ya JMT, huku Katiba ya JMT ikiendelea kuitambua Katiba ambayo imefutwa.

Katiba ya Zanzibar katika Ibara ya 26, inatamka kwamba Rais wa Zanzibar ni mkuu wa nchi ya Zanzibar. Katiba ya Jamhuri ya Muungano katika Ibara ya 33(2) inatamka: “Rais wa Jamhuri ya Muungano ndiye mkuu wa nchi, kiongozi wa Serikali na Amiri Jeshi Mkuu.”

Hapa ni mwendelezo wa Zanzibar kujitangaza kuwa nchi na kumtangaza Rais wa Zanzibar kama mkuu wa nchi, wakati ukweli ni kwamba Tanzania ni nchi moja, Zanzibar siyo nchi, bali ni sehemu ya JMT, yenye utawala wake wa ndani.

Mikanganyiko hiyo haikuishia hapo, kuna vifungu vimepoka mamlaka ya Bunge kutunga sheria za muungano, kuna vifungu vimepoka mamlaka ya Mahakama ya Rufaa Tanzania kuifanya Mahakama Kuu ya Zanzibar ndio kuu kuliko Mahakama ya Rufaa ya JMT.

Ukiondoa hiyo mikanganyiko ya Katiba ya Zanzibar na Katiba ya JMT, mabadiliko hayo ya Katiba ya Zanzibar pia yameleta mambo mazuri, Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK), hili ni jambo kubwa, zuri la heri, japo kiprotokali, Serikali ya JMT inaitambua SUK na viongozi wake wanapewa protokali stahiki kitaifa na kimataifa.

Sasa ni muda mwafaka kwa Katiba ya JMT, ama iitambue rasmi Katiba ya Zanzibar, kwa kuifanyia marekebisho Katiba ya JMT na kuuingiza SUK au Zanzibar ilazimishwe kuuondoa huo utata wa Katiba ya Zanzibar kupoka mamlaka ya JMT, Rais, Bunge na Mahakama.

Related Posts