Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Dkt. John Jingu, amewataka wadau wa Kemikali kuzingatia matumizi salama na sahihi ya kemikali ili kuchochea maendeleo katika nchi yetu kwani kemikali ikitumika vizuri kwa kuzingatia miongozo ina faida kubwa tofauti na pale inapotumika vibaya.
Dkt. Jingu amesema hayo leo wakati akifungua mafunzo ya siku tatu ya usimamizi na udhibiti wa kemikali na bidhaa zake kwa wasimamizi wa kemikali yaliyoandaliwa na Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kupitia Ofisi ya Kanda ya Mashariki na kufanyika jijini Dodoma Desemba 11, 2024
“Shughuli za kiuchumi na maisha ya kila siku ya mwanadamu, zinategemea uwepo wa kemikali, mafunzo haya yana tija kubwa sana kwa sababu yatatusaidia kuwa na matumizi salama na sahihi ya kemikali, hivyo yatachochea maendeleo kwa sababu kemikali ina faida kubwa pale tu inapotumika vizuri, lakini ikitumika vibaya madhara yake ni makubwa sana mfano Vifo na athari za kiafya na mazingira” alisema Dkt. Jingu.
Katika hatua nyingine Katibu Mkuu ameipongeza Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kwa kaulimbiu ya mafunzo hayo inayosema “Mafunzo yanaendelea” kwani elimu haina mwisho na kwenye Nyanja ya kemikali mambo mengi yanaibuka kila siku hivyo elimu ndio silaha kuu ya kuwezesha matumizi salama na sahihi ya kemikali kwa lengo la kulinda afya za binadamu na mazingira ambayo kemikali hizo hutumika.
Kwa upande wake Mkemia Mkuu wa Serikali, Dkt. Fidelice Mafumiko, amesema Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali inaendelea kutimiza majukumu yake ya kisheria ikiwemo kutoa elimu na kufanya usajili na ukaguzi wa kemikali ili kuiwezesha Serikali kufahamu ni kemikali ipi imeingizwa na nani kwa ajili ya matumizi gani na je inaruhusiwa kisheria ili kulinda afya na mazingira.
“hadi kufikia jana Desemba 10, 2024 jumla ya wadau 5933 wanaojihusisha na kemikali wamesajiliwa rasmi baada ya jitihada za Mamlaka ambapo ukirejea mwaka 2012 wakati utekelezaji wa Sheria ya usimamizi na udhibititi wa kemikali za viwandani na majumbani sura ya 182 unaanza jumla ya wadau 12 tu walisajiliwa rasmi” alisema Dkt. Mafumiko.
Berina Valence na Jimmy Mkongwe ni washiriki wa Mafunzo hayo wamesema wamepata elimu kubwa ambayo itawasaidia kuondokana na usimamizi wa mazoea wa kemikali kwenye maeneo yao ya kazi kwani ni hatari kwa afya za wafanyakazi na mazingira
“Mafunzo haya yana tija kubwa sana kwa sababu kuna baadhi ya mambo tumezoea kufanya kimazoea lakini hapa tunapata shule inayotuamsha na kuturudisha kwenye muelekeo sahihi” walimaliza.
Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Dkt, John Jingu, akiongea wakati akifungua mafunzo ya siku tatu ya usimamizi na udhibiti wa kemikali na bidhaa zake kwa wasimamizi wa kemikali (hawapo pichani) mafunzo yaliyoandaliwa na Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kupitia Ofisi ya Kanda ya Mashariki, yaliyofanyika katika ukumbi wa Dkt. Mafumiko jijini Dodoma, Desemba 11, 2024.
Mkurugenzi wa Huduma za Udhibiti wa Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Daniel Ndiyo (aliyesimama) akiwasilisha mada juu ya Mwongozo wa udhibiti wa kemikali aina ya Sulphur na Ammonium Nitrate katika mafunzo ya usimamizi na udhibiti wa kemikali na bidhaa zake kwa wasimamizi wa kemikali (waliokaa) mafunzo yaliyoandaliwa na Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kupitia Ofisi ya Kanda ya Mashariki yaliyofanyika katika ukumbi wa Dkt. Mafumiko jijini Dodoma, Desemba 11, 2024.
Meneja wa Mamlaka, Kanda ya Mashariki, Danstan Mkapa (kulia) akiwa na Meneja wa Kanda ya Kati (kushoto) wakiwa katika ufunguzi wa mafunzo ya siku tatu ya usimamizi na udhibiti wa kemikali na bidhaa zake kwa wasimamizi wa kemikali (hawapo pichani) wakati wa mafunzo yaliyoandaliwa na Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kupitia Ofisi ya Kanda ya Mashariki yaliyofanyika katika ukumbi wa Dkt. Mafumiko jijini Dodoma, Desemba 11, 2024.
Baadhi ya Wasimamizi wa Kemikali wakifuatilia mafunzo ya usimamizi na udhibiti wa kemikali na bidhaa zake kwenye mafunzo yaliyoandaliwa na Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kupitia Ofisi ya Kanda ya Mashariki yaliyofanyika katika ukumbi wa Dkt. Mafumiko jijini Dodoma, Desemba 11, 2024Wasimamizi wa Kemikali wakiuliza maswali kwenye mafunzo ya usimamizi na udhibiti wa kemikali na bidhaa zake, mafunzo yaliyoandaliwa na Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kupitia Ofisi ya Kanda ya Mashariki, yaliyofanyika katika ukumbi wa Dkt. Mafumiko jijini Dodoma, Desemba 11, 2024 .