Dar es Salaam. Baada ya Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe kuvunja ukimya kuhusu msimamo wake wa kugombea au kutogombea nafasi hiyo, makada wa chama hicho wametoa mitazamo tofauti.
Wapo wanaosema kauli ya Mbowe ni sahihi kwamba hakuna mwanachama wa Chadema anayezuiwa kuwania nafasi hiyo, huku wengine wakitaka usubiriwe wakati wa viongozi na wanachama kuamua iwapo agombee au asigombee.
Wakati makada wakitoa mitazamo yao, kesho Desemba 12, 2024 Makamu Mwenyekiti wa Chadema (Bara), Tundu Lissu anatarajia kuwa na mkutano na wanahabari jijini Dar es Salaam, kueleza mambo mbalimbali yanayoendelea ndani ya chama hicho ikiwemo kutangaza nia ya kugombea uenyekiti.
Mbowe jana Jumanne Desemba 10, 2024 akijibu swali aliloulizwa na mwanahabari kuhusu kugombea nafasi ya uenyekiti wa chama hicho, alisema uamuzi wa kugombea au kutogombea utatokana na wanachama wa Chadema.
Swali hilo linatokana na vuguvugu la ndani ya chama hicho kuwa, Lissu ameonyesha nia ya kuitaka nafasi hiyo, huku wengine wakidai imetosha kwa Mbowe kuwa mwenyekiti baada ya kuongoza kwa miaka 20.
“Ooh! wengine wanasema Mbowe umekaa sana miaka 20 ni hivi, miaka 20 ni ya kukomaa, hebu wewe jaribu kukomaa kwa miaka 20 fanya kazi uone komaa yako itakavyokuwa, mwingine analinganisha kwamba Nyerere (Julius) alinga’ tuka.
“Nyerere alikuwa mtumishi wa umma, analipwa mshahara, hafungwi wala kushtakiwa, sisi unaona hapa wote tunajitolea. Miaka 20 ya kukomaa,” amesema.
Tayari wafuasi wa Lissu wameshaanza kusambaza bango la taarifa rasmi ya kufanyika kwa mkutano huo, ingawa halikuweka wazi ajenda zitakazozungumzwa.
Mwananchi limedokezwa kuwa, mbunge huyo wa zamani wa Singida Mashariki atatumia mkutano huo kutangaza nia ya kuwania uenyekiti wa Chadema Taifa, katika uchaguzi utakaofanyika mapema mwakani.
Mkutano huo ilikuwa ufanyike wiki iliyopita jijini Dar es Salaam lakini ukahamishiwa Dodoma na sasa umerejeshwa tena Dar es Salaam.
Kushindikana kufanyika kwa mkutano huo kulitokana na kile kilichoelezwa kumpa nafasi Mbowe kutoa msimamo wa Chadema kuhusu maazimio ya Kamati Kuu iliyojadili mchakato wa uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji Novemba 27, 2024.
Akizungumzia hilo, Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa kichama Kinondoni jijini Dar es Salaam, Henry Kileo amesema si dhambi kwa wawili hao kugombea, kufanya hivyo ndivyo demokrasia inatamalaki.
Amesema ikitokea wakagombea wakati wa matokeo, atakayeshindwa anapaswa kukubali kumuunga mkono mshindi na kuwashawishi wafuasi wake waendelee kuwa waaminifu kwa chama.
“Kama wote watagombea ni vyema kwa sababu demokrasia itatamalaki, lakini atakayeshindwa ahakikishe anaendelea kufanya kazi za chama na kuwaunganisha waliokuwa wanamuunga mkono,” amesema.
Kileo amesema kwa sababu wawili hao ni kama majenerali ndani ya jeshi, hatua ya wote kugombea nafasi moja inaweza kuwapa faida wapinzani wao.
“Ni vyema wafanye busara ya kumwachia mmoja, huku mwingine akikubali kuwa msaidizi,” ameshauri.
Amesema bado hakuna taarifa rasmi za yeyote kati ya wawili hao kuwania nafasi hiyo na hadi sasa mwenyekiti aliye madarakani ni Freeman Mbowe.
Hata hivyo, amesema kwa sababu wawili hao ni viongozi wa ngazi ya juu ndani ya chama hicho ni muhimu wachague baadhi ya mambo na kuyazungumza wenyewe ndani kabla hayajatoka hadharani.
Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Dodoma, Aisha Madoga amesema kwa sababu anajua siasa za mageuzi zinawagharimu kiasi gani na wanakijua wanachokihitaji hawako tayari kushinikizwa.
Kwa sababu katiba ya chama hicho haijaweka ukomo wa madaraka, Aisha amesema haoni tatizo iwapo Mbowe atawania tena nafasi hiyo ya uenyekiti.
Kwa mujibu wa Madoga, hakuna sababu ya kumshinikiza kiongozi huyo asigombee au astaafu uenyekiti kwa kuwa ana haki zote za msingi za kugombea na kuongoza kwa awamu nyingine.
“Najua watu wengi wanamsema mwenyekiti baada ya kuamua kuingia kwenye maridhiano, lakini ile ilikuwa moja ya mbinu za kutafuta njia mbadala ya kutatua changamoto zilizopo,” amesema.
“Baada ya kushindwa kwa njia ya maandamano kupambana na mfumo, mwenyekiti alitafuta njia mbadala na ndipo alipoingia kwenye maridhiano. Na kusema ukweli yamesaidia kuna watu walifungwa, wakatolewa,” amesema.
Katibu wa Chadema wa Jimbo la Ubungo, Dar es Salaam, Moses Odinga amesema Mbowe ameeleza wazi kwamba katiba ya chama hicho haijamzuia mtu asigombee nafasi yoyote ndiyo maana kuna uchaguzi.
“Chadema kimejengwa kwa misingi ya kwamba tunaishi kama familia, kwa asilimia kubwa tunafahamiana. Kwa mfano katika uchaguzi wa mwaka 2019, Mbowe tumlichukulia sisi vijana fomu, tulimuomba kwa sababu alisema kwa muda huo vijana ndio wanatosha, lakini tukasema hapana tunahitaji huduma yake.
“Ingawa wakati hajasema lolote kuhusu kugombea au kutogombea, lakini amesema Chadema hakijamzuia mtu kugombea na kukaa kimya haimzuii mtu kugombea, kila mtu yupo huru. Baadhi ya wanachama tunatamani tuone Mbowe aendelee kutulea,” amesema.
Hata hivyo, amesema ukifika wakati sahihi Mbowe akifikiria kutangaza kugombea basi wanachama na viongozi ndio watakaoamua kwenda naye au atafutwe mtu mwingine anayefaa zaidi.
Katibu wa Chadema Mkoa wa Kilimanjaro, Basil Lema ameeleza kufurahia hatua ya Mbowe kurejea kauli aliyowahi kuitoa mwaka 2019 kuhusu chama hicho kufungua milango ya watu kugombea.
“Ninaridhika kauli yake hii ni ya dhati, kwa sababu haiwezekani airudie kwa miaka mitano mfululizo ni kitu kipo katika imani yake. Inawezekana jana Jumanne (Desemba 10) hakutaka kusema siri kubwa nyingine, lakini mimi ninayo siri yake nyingine kwamba tangu mwaka 2004 hajawahi kuchukua fomu ya Chadema,” amesema.
“Sasa inawezekana hii imetengeneza imani kubwa ambayo imekuwa ulemavu, kama umefanya kazi ukawaridhisha wanachama basi wataamua ugombee au usigombee. Yupo katika sura kwamba umewaridhisha wanachama, watakuchukulia fomu, watakupigia kura, watakupa ushirikiano kwa miaka mitano,” amesema.