Ligi Kuu Bara namba zinaongea

LIGI Kuu Bara inatarajiwa kuendelea leo Jumatano kwa kuchezwa mechi mbili ikiwa ni raundi ya 14 tukielekea kuugawa msimu. Baada ya kumalizika kwa raundi hii, tunabakiwa na moja ambayo imekuwa na ushindani mkubwa sana.

Hadi sasa, rekodi zinaonyesha hakuna hat trick iliyopatikana, hiyo inadhihirisha wazi hivi sasa suala la mchezaji kufunga inabidi afanye kazi ya ziada.

Ukiachana na hat trick kuna ishu ya kuongoza kwa mabao, kinara ni Seleman Mwalimu wa Fountain Gate mwenye sita akifuatiwa na Jean Charles Ahoua wa Simba (5).

Ahoua ambaye amejiunga na Simba msimu huu, ameonekana kuwa na mchango mkubwa wa mabao kikosini hapo, wakati timu hiyo ikifunga 22 yeye amehusika kwenye mabao tisa kutokana na asisti nne na mabao matano.

Kinara wa mabao msimu uliopita, Stephane Aziz Ki wa Yanga, hadi sasa amefunga moja na asisti zake mbili wakati aliyeshika namba mbili, Feisal Salum akifunga manne na kuongoza kwa asisti akifikisha tano.

Ufalme wa kulinda lango, unashikiliwa na Moussa Camara wa Simba ambaye ana clean sheet tisa ukiwa ni usajili mpya msimu huu. Kipa ambaye msimu uliopita aliibuka kinara wa clean sheet, Ley Matampi, hajafua dafu kwani hadi jana Coastal Union inatangaza kufikia makubaliano ya kusitisha mkataba wake, alikuwa na clean sheet moja pekee. Camara anafuatiwa na Djigui Diarra wa Yanga mwenye clean sheet saba.

Ugumu na ushindi uliopo katika ligi umemuibua Kocha Abdallah Mohamed ‘Bares’ wa Mashujaa ambaye amesema hiyo inatokana na kila timu kuendelea kujiimarisha na kuzifukuzia nafasi za kushiriki michuano ya kimataifa.

“Ushindani ni mkubwa sana, leo hii unaweza kuona timu inapata matokeo mazuri katika uwanja wowote ule haijalishi nyumbani au ugenini, hiyo inatoa picha halisi kuna mabadiliko makubwa.

“Hatua hii inazidi kuifanya ligi yetu kuzidi kuwa bora kitu ambacho kinatakiwa kuonekana,” alisema kocha huyo ambaye ndiye pekee amesalia katika timu aliyoanza nayo msimu uliopita 2023-2024 hadi sasa 2024-2025 huku zingine zote zikifanya mabadiliko ya benchi la ufundi.

Kwa upande wa Kocha Mkuu wa Namungo, Juma Mgunda, amesema ugumu uliopo kwenye ligi unaiweka katika hatari timu yake hivyo ameamua kufanya kazi ya ziada kukabiliana na jambo hilo.

β€œNafasi tuliyopo sio nzuri, mimi kwa kushirikiana na wenzangu tumekaa na wachezaji kujua shida iliyopo na kuanza kuifanyia kazi, tunafahamu msimu huu ligi ni ngumu hivyo lazima tujipange mapema kabla mambo hayajawa magumu sana,” alibainisha Mgunda.

Kuna mengi yamejiri ndani ya Ligi Kuu Bara ambayo inaendelea kwa sasa na Mwanaspoti linakubainishia baadhi yake kwa mfumo wa namba.

Idadi ya mechi za Ligi Kuu Bara zilizochezwa msimu huu wakati leo tukiingia raundi ya 14.

KenGold ni timu pekee iliyopata ushindi wa mechi chache zaidi (1), huku pia timu za Azam na Simba zikipoteza mechi chache zaidi (1).

Wakati Simba ikijivunia kufunga mabao mengi zaidi (22) katika ligi, KenGold imeruhusu mabao mengi zaidi (22).

Kati ya mabao 195 yaliyofungwa katika mechi 99, wazawa wanakimbiza kwa kufunga 112, huku wageni wakiwa nayo 78. Katika mabao hayo, kuna matano ya kujifunga.

Dodoma Jiji ndiyo timu iliyojifunga mabao mengi (2) katika ligi msimu huu. Zingine zilizojifunga ni KMC, Azam na Simba.

Ni idadi ya kadi nyekundi zilizoonyeshwa mpaka sasa kwa wachezaji Cheikh Sidibe (Azam), Saleh Masoud (Pamba Jiji), Victor Sochima (Tabora United), Ibrahim Elias (KMC), Denis Richard (JKT Tanzania), Ibrahim Hamad ‘Bacca’ (Yanga), Abalkassim Suleiman (Fountain Gate) na Ramadhan Chobwedo (KenGold).

Katika mikwaju 31 ya penalti iliyopigwa mpaka sasa, sita wapigaji wamekosa huku 25 ikijaa nyavuni.

Ni timu tatu pekee bado hazijafaidika na mkwaju wa penalti ambazo ni KMC, Kagera Sugar na Pamba Jiji, huku Tabora United ikiongoza kwa kupata penalti tano ikifuatiwa na Simba (4). Timu iliyopigiwa penalti nyingi ni Kagera Sugar (4) wakati Simba na Yanga ndiyo pekee hazijapigiwa mkwaju huo.

Imeshuhudiwa mechi 12 pekee kati ya 99 zimemalizika bila ya nyavu za timu yoyote kutikiswa.

Idadi ya makocha wakuu walioondolewa kwenye timu hadi sasa kwa sababu tofauti ikiwa ni raundi 13 pekee zimechezwa. Msimu uliopita hadi unamalizika yalifanyika mabadiliko ya makocha 18.

Related Posts