Mama adaiwa kumuua mwanawe kwa panga

Morogoro.  Jeshi la Polisi mkoani Morogoro linamshikilia Teodora Mkunga (39), mkazi wa Lusange, Kata ya Mtombozi, Wilaya ya Morogoro, kwa tuhuma za kumuua mtoto wake Simon Gervas (8) kwa kumkata sehemu mbalimbali za mwili wake kwa panga.

Kamanda wa Polisi mkoani Morogoro, SACP Alex Mkama akizungumza ofisini kwake leo Jumatano Desemba 11, 2024, amesema tukio hilo lilitokea Desemba 8, mwaka huu na chanzo kinadaiwa kuwa matatizo ya akili aliyokuwanayo mwanamke huyo.

“Siku ya tukio, mama huyo alimvamia mtoto wake na kumshambulia kwa kutumia silaha yenye makali sehemu za kichwani na mgongoni, jambo lililosababisha mtoto huyo kupoteza maisha kutokana na kupoteza damu nyingi,” amesema Kamanda Mkama.

Amesema Polisi wanamshikilia mtuhumiwa huyo kwa uchunguzi zaidi kabla ya kufikishwa mahakamani.

Akizungumza na Mwananchi Digital, baba wa mtoto huyo, Gervas Jovin amesema aliambiwa kuwa mtoto huyo alikuwa akicheza na wenzake kabla ya mama yake kumvamia na kuanza kumshambulia kwa panga.

“Nilipofika nyumbani nilikuta mtoto wangu amelala chini na damu nyingi zikimtoka, nilipomtazama zaidi, alikuwa tayari ameshakufa. ila mama yake ana matatizo ya akili, ila tayari alishaanza matibabu na hali yake ilikuwa inaonekana kuwa nzuri, naona hali ya awali imerudi tena upya,” amesimulia baba mtoto huyo.

Mwili wa mtoto huyo tayari umeshafanyiwa uchunguzi wa kidaktari na ulizikwa Desemba 9, 2024, katika makaburi ya Kijiji cha Lusange.

Katika tukio lingine, Kamanda Mkama amesema wanawashikilia watu wengine watano kwa tuhuma tofauti ikiwamo ya kukamatwa na pikipiki za wizi wilayani Kilosa.

“Desemba 8, 2024 tumemkamata Msilvesta Aloyce (38) akiwa na pikipiki MC 765 DDP aina ya Hojue, iliyokuwa imeibiwa Julai 29, 2024,” amesema Mkama.

Wakati huo huo, kamanda huyo amesema  watuhumiwa wengine watatu wanashikiliwa na jeshi hilo kwa tuhuma ya kuhujumu miundombinu ya kilimo.

Kamanda Mukama amesema wanatuhumiwa kukata uzio wa shamba la Taifa la mbegu Msimba wilayani Kilosa na kuingiza kundi kubwa la ng’ombe walioharibu mazao yaliyokuwa ndani ya shamba hilo.

Amesema uchunguzi kuhusu matukio hayo unaendelea na watuhumiwa wote watafikishwa mahakamani uchunguzi utakapokamilika.

Pia, amewaondoa hofu wananchi mkoani humo kuhusu usalama katika kipindi hiki cha sikukuu za mwishoni mwa mwaka.

“Niwasihi wanannchi waendelee kuwa watulivu, na Jeshi la Polisi linaendelea kuimarisha ulinzi kuelekea msimu huu wa sikukuu,” amesema kamanda huyo.

Related Posts