Moshi. Wanasheria mbalimbali wakiwamo mawakili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, wamependekeza mambo 10 ambayo kama yakifanyika, vitendo vya utekaji nyara, kupoteza watu, kutesa na mauaji vinaweza kutoweka nchini.
Moja ya mapendekezo hayo ni pamoja na kutekelezwa kwa vitendo na siyo kutolewa kwa kauli za kisiasa, kwa mapendekezo yote ya Tume ya Haki Jinai iliyoundwa na Rais Samia Suluhu Hassan na kuongozwa na Jaji Othman Chande.
Wakili mashuhuri nchini, Method Kimomogoro amependekeza kurejeshwa kwa utaratibu wa zamani ambapo Polisi hakuweza kumkamata mtu nyumbani kwake bila kuwepo kwa Balozi wa nyumba kumi kushuhudia ukamataji huo.
Wakili Kimomogoro alienda mbali na kupendekeza kuwa mahakama hapa nchini zifike mahali zisikubali kupokea mshitakiwa pasipo kujiridhisha juu ya ukamataji wake kama ulizingatia sheria na kiongozi wa eneo husika alishirikishwa.
Kauli za wanasheria hao zimekuja baada ya baadhi ya wananchi kuanza kujawa na hofu hususan wanaharakati, viongozi wa kisiasa, wanachama wa vyama vya siasa na wakosoaji kutokana na kuendelea kushamiri kwa vitendo vya utekaji nyaraka.
Hii inakuja siku chache baada ya Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana ya ACT-Wazalendo, Abdul Nondo kutekwa na watu wasiojulikana Desemba mosi, 2024 muda mfupi baada ya kushuka katika basi Kituo cha Mabasi cha Magufuli.
Lakini lilitokea siku chache baada ya uwepo wa tukio la jaribio la kumteka mfanyabiashara wa Jijini Dar es Salaam, Deogratius Tarimo na kushushwa kwenye basi na kuuawa kwa mjumbe wa secretarieti ya Chadema, mzee Ally Kibao.
Si hivyo tu, lakini wanasheria na mawakili hao wamepaza sauti zao miezi kadhaa tangu Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS) kutoa tamko zito, viongozi wa dini, wanaharakati na wananchi wakitaka Serikali na Jeshi la Polisi kudhibiti hali hiyo.
Katika taarifa yake, Tume ya Haki Jinai ilibainisha uwepo wa utitiri wa vyombo vya Haki Jinai vinavyotekeleza majukumu yake kwa taswira ya kijeshi na vikiwa na mamlaka ya kukamata, wakitaka uanzishwaji wa vyombo hivyo usitishwe.
Pia Tume hiyo ilibaini kuwa uwepo wa taasisi nyingi zenye mamlaka ya kukamata washukiwa na vyenye mahabusu umetafsiriwa na jamii kuwa ni sababu mojawapo ya watu waliokamatwa kupotea wakiwa mikononi mwa vyombo vya dola.
Tume ikapendekeza mambo matatu ambayo hayajapatiwa ufumbuzi nayo ni kwa mamlaka ya kukamata waliyonayo mamlaka za usimamizi na taasisi nyingine yatekelezwe kwa kushirikiana na polisi na zitumike mahabusu za polisi pekee.
Lakini tangu kutolewa kwa taarifa ya Tume hiyo, kilio cha wadau wengine wa haki jinai wakiwamo viongozi wa dini ikiwamo kufumuliwa kwa Jeshi la Polisi, bado utekelezaji wa mapendekezo unasuasua huku utekaji nyara watu ukiendelea.
Mapendekezo 10 ya wanasheria
Wakizungumza na gazeti hili kwa masharti kuwa wanatoa maoni binafsi nje ya yaliyotolewa na TLS Agosti 9, 2024 na kutoa orodha ya watu 83 waliotekwa na kupotea au kuuawa, wamedai kunahitajika mjadala wa kitaifa juu ya suala hilo.
Wakili Aloyce Komba ambaye pia ni mwanahabari, alirejea wito uliotolewa na TLS kuwa uchunguzi wa matukio ya utekaji, kupotea kwa watu na mauaji ufanywe na Tume Huru ya Kimahakama (Coroners Court) akihoji kwanini haiundwi hadi sasa.
Kwa upande wake, wakili Kimomogoro wa Jijini Arusha alishauri polisi yeyote asiruhusiwe kumkamata mtuhumiwa bila taaarifa kwa viongozi wa eneo anakoishi na aruhusiwe kuwajulisha wakili wake, ndugu, jamaa au rafiki yake wa karibu.
“Pia Wananchi wahamasishwe kupinga ukamataji wa mwananchi yeyote iwapo mkamataji hajajitambulisha ipasavyo,”alisisitiza wakili huyo akisema hiyo itawafanya askari wa Jeshi la Polisi kuhakikisha wanazingatia sheria ipasavyo.
“Lakini vile vile mahakama isikubali kumpokea mshitakiwa atakayefikishwa mahakamani bila uthibitisho kwamba uongozi wa eneo lake, ndugu na jamaa au wakili wake wana taarifa ya kukamatwa kwake,” alisisitiza wakili huyo.
“Kipindi cha awamu ya kwanza ilikuwa marufuku kwa mtu yeyote wakiwamo polisi kumkamata raia bila kupitia kwa balozi wa nyumba kumi isipokuwa tu kama amekamatwa akitenda kosa la jinai. Turudishe huu utaratibu kuepuka utekaji”.
“Majeshi mengine hayakuruhusiwa kumkamata raia isipokuwa pale alipokutwa ameingia kiuhalifu kwenye eneo la jeshi husika mfano la JWTZ, JKT au Magereza, na afisa mkamataji alilazimika kumkabidhi kwa Kituo au kwa askari polisi.”
“Kwa makosa yasiyo na dhamana, hata polisi alihitaji warrant of arrest (hati ya ukamataji kutoka kwa hakimu au ofisa wa polisi wa cheo fulani. Siku hizi kwa ujio na utapakaaji wa simu za mkononi hakuna sababu ya msingi ya mwananchi yeyote kukamatwa bila kufuata taratibu hizi,”alieleza wakili huyo.
Kwa upande wake, wakili David Shillatu alisema ukamataji ulio wa haki na usioleta tashwishi ya aina yoyote ni ule ambao askari mkamataji atajitambulisha kwa kutoa kitambulisho na kwa kufanya hivyo kumpatia nafasi huyo anayekamatwa kufahamu wazi ni nani anayemkamata na kwa kushukiwa kutenda kosa gani.
“Sasa katika nyakati za leo, utaratibu huo unaoelekezwa na PGO (Kanuni za uendeshaji Jeshi la Polisi nchini) haufuatwi badala yake watu wanakamatwa hovyo na hivyo kufanya utekelezaji wa sheria na PGO kuwa mgumu kwelikweli,”alidai.
“Lakini kusema ukweli bado kuna mapungufu hayo na ndiyo yameongeza matukio haya ya utekwaji kwa kuwa kwa sasa wananchi wanashindwa kuelewa kama anayemkamata ni polisi kweli? Kama ni polisi kweli ni ofisa wa cheo gani?”
“Kimsingi ni maoni yangu kwamba Jeshi la Polisi lilipaswa kuendelea na wajibu wake msingi wa usalama wa raia na mali zao. Idara nyingine yeyote isiruhusiwe kukamata raia, suala hili linapaswa kutunzwa kisheria,” alisisitiza Shillatu.
Wakili Peter Mshikilwa wa jijini Dar es Salaam, alitaka uwajibikaji wa vyombo vya ulinzi na usalama lakini akasema sasa ni wakati mwafaka kuwa na mjadala wa kitaifa kuhusu matukio ya utekaji na kufuata ushauri wa Tume ya Haki Jinai.
“Tume ilishauri tulifanyie mapinduzi makubwa Jeshi la Polisi kutoka katika fikra za upolisi wa kikoloni kuwa jeshi la kisasa linalowajibika kwa Jamii lakini tumen a chombo huru cha kupokea malalamiko dhidi ya Jeshi la Polisi,”alisema.
Mkurugenzi wa Jukwaa la Katiba Tanzania (Jukata), Bob Wangwe alisema kinachopaswa kufanyika ni Jeshi la Polisi kuhakikisha linatokomeza vitendo vya utekaji na wananchi wanakuwa salama bila kujali nao wananyooshewa kidole.
Wangwe ambaye ni mwanasheria, alisema Jeshi la Polisi haliwezi kukwepa kunyooshewa kidole kwani wajibu wa usalama wa raia uko mikononi mwao na kushauri kwa hali ilivyo sasa, wananchi waendelee kujilinda kadri iwezekanavyo.