Manula afichua siri nzito Simba akimtaja Camara

NI suala la kawaida kwa binadamu yeyote aliye hai maisha yake kuwa na hali ya kupanda na kushuka, inaweza kukutokea kazini, masomoni, kwenye uhusiano au sehemu nyinginezo.

Sio rahisi sana kupitia kipindi kigumu kwenye maisha halafu ukarudi katika hali ya mwanzo, kwa sababu kwenye hii muda hautusubiri ila unapopata changamoto lazima mbadala wako upatikane haraka ili mambo yasikwame.

Hiki ndicho kilichomkuta kipa namba moja Tanzania, Aishi Manula kutoka kucheza mechi zote muhimu na kuwa tegemeo la klabu ya Simba na timu ya taifa, Taifa Stars hadi kukaa benchini.

Unaweza ukaelewa kibinadamu ni ngumu kiasi gani kuipokea hali ya watu kusahau kila kitu ulichofanya katika kuibeba timu, kuipa mataji na hata kuiokoa katika mechi ngumu huko nyuma.

Manula anakutana na Mwanaspoti baada ya mazoezi mazito aliyoyafanya huku hali ya hewa ikiwa ni ya mvua na anaweka wazi kuwa alishawahi kutamani kuchezea timu nyingine ila mkataba ndio uliomfunga, huku akielezea namna alivyokuwa akijihisi kama binadamu alipokuwa nje ya gemu.

NILITAMANI KUONDOKA SIMBA

Mwishoni mwa msimu uliopita Manula alijikuta nafasi yake haipo kama hapo awali na aliachwa benchini.

Kipa huyo aliyekuwa nguzo muhimu wakati Simba ikishinda ubingwa wa Ligi Kuu Bara mara nne mfululizo, anafunguka sababu zake za kutamani kutimka katika klabu hiyo aliyoitumikia kwa misimu saba:

“Ndio niliwahi kutamani kuondoka na ilitokana na msukumo wa ndani kuhusu kupata nafasi ulionifanya nione hivyo, kama ningepata hiyo nafasi ya kuondoka ningefanya hivyo, Lakini sijapata kwa hiyo nimeendelea kubaki kwenye timu.

“Nipo naendelea kufanya kazi kwa ari kubwa ili kufikia malengo ambayo klabu imejiwekea kwani hicho ndicho kinanifanya niwe hapa mpaka leo.

“Mimi sio mwepesi wa kukata tamaa, kama ingelikuwa hivyo basi usingaliniona hapa nilipo hadi leo, kwa sababu kitu kikubwa ni kufanya mazoezi kwa bidii, kocha ndio anajua nani amtumie na siku zote mwalimu hawezi kumuweka benchi mchezaji mzuri na ambaye anaamini atampa matokeo.

“Imani ya kocha ni kwamba yule anayempa nafasi atamsaidia kupata matokeo mazuri na hiyo ndio kazi yake kubwa.”

Manula alipata changamoto ya kusumbuliwa na nyonga akiwa katika mechi jambo lililomfanya kutomaliza dakika 90 na baadaye taarifa kutolewa kuwa atakuwa nje msimu mzima  au miezi sita.

Lakini alirejea katika Dabi ya Kariakoo ya kwanza ya msimu 2023-24 katika Ligi Kuu kuikabili Yanga ambayo Wekundu wa Msimbazi wakiwa chini ya kocha Mbrazili Roberto Oliveira ‘Robertinho’. walilala 5-1 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa Novemba 5, 2023

“Kwenye maisha yetu ya mpira wa miguu majeraha ni sehemu ya changamoto na unapopitia huwa ni hali kubwa sana ya kumuomba Mungu akuvushe salama, lakini pia ni muda unaotakiwa uzingatie zaidi matibabu.

“Kwa sababu ndio yanayoweza kukufanya urudi uwanjani au usirudi, nadhani nimefanya kazi vizuri na jopo la madaktari, ulikuwa wakati mbaya kwa sababu unaona wenzako wanacheza na unatamani kuwa nao lakini haiwezekani.

“Inauma unaona timu inasafiri, inacheza na wachezaji wanaitwa timu ya Taifa na kama mchezaji ambaye umeshiriki hayo matukio lazima upate simanzi ila unagundua ni sehemu ya maisha ya mchezo na unakuwa na imani, kama sasa hivi Neymar mchezaji mkubwa lakini hayuko sawa.”

“Sikupata presha yoyote kuwa sitacheza tena kwa sababu nilijua tatizo ni nini na nitakaa nje muda gani huo ulikuwa wakati mzuri,” anaongeza Manula. 

Kipa huyo aliyeifanikisha Stars kutinga fainali za Afcon 2025 anaweka wazi kuwa, wakati yuko nje kutokana na majeraha klabu hiyo haikumtupa.

“Binafsi klabu ilinilipia matibabu nje ya nchi kuanzia upasuaji na ilifanya majukumu yak. Mimi pia kwa upande wangu niliyatimiza.”

“Ushindani upo mkubwa na klabu iko tayari kurudisha mataji yale tuliyokuwa nayo mwanzo na mwalimu tuliyenaye (Fadlu Davids) ukiachilia ubora wake ni kijana pia mwenye mbinu za kisasa anayehitaji wachezaji wafanye kazi kubwa.

“Pia timu ina wachezaji vijana wenye uchu wa mafanikio. Timu lazima itengeneze picha yake kwani ina watu wanaojua ukubwa wa Simba hata wageni nao wanaona hii ni nafasi nzuri ya kutengeneza sehemu yao ya maisha.

Eneo la makipa kwa upande wa Simba sasa liko na wachezaji watano ambao wote wana viwango bora kama Ayoub Lakred, Aishi Manula, Moussa Camara, Ali Salim na Hussein Abel.

Aliyesajiliwa msimu huu ni Camara ambaye ndiye anayecheza sana kwa sasa, lakini baada ya majeraha ya Manula aliyekuwa langoni alikuwa Ayoub na Ali Salim.

Anasema aliporudi akakuta wachezaji wameongezeka na uwezekano wa kupata namba ulikuwa mgumu.

“Camara ni kipa mzuri ndio maana anapata nafasi za kucheza na sisi kwa sasa tuko nyuma yake tukiendelea kushirikiana naye kwa kile kikubwa anachofanya na kama wachezaji tunajiandaa vizuri ili pale ambapo mwalimu atahitaji tumsadie basi na sisi tufanye vizuri.”

Kipa huyo namba moja wa Simba tangu msimu wa 2017/18 anaweka wazi kuwa ndani ya misimu sita alikuwa akicheza sana ila ujio wa Mcameroon Camara kwake hauchukulii vibaya.

“Kwa sababu malengo ya timu ni kuhakikisha tunarejesha makombe tuliyoyapoteza, Lakini pia tunafika kwenye hatua za juu katika mashindano ya kimataifa, uzuri kwenye nafasi yetu tunafanya makubwa, kwa sababu kufanya vizuri kwa Camara ni kama tumefanya sisi. Namtakia kheri.”

Related Posts