Mido ya boli yatua Namungo

KIUNGO wa Singida Black Stars, Najim Mussa anakaribia kujiunga kwa mkopo Namungo baada ya makubaliano ya pande mbili baina ya nyota huyo na klabu.

Nyota huyo aliyejiunga na Singida msimu huu akitokea Tabora United baada ya kuonyesha uwezo mzuri na kutabiriwa makubwa, mambo yamekuwa tofauti kwake kwani hadi sasa ameanzia benchi michezo miwili tu kati ya 12 ambayo kikosi hicho kimecheza.

Akizungumza na Mwanaspoti, Najim alisema kwa sasa anachotaka ni kuhakikisha anapata nafasi ya kucheza kikosi cha kwanza baada ya kuanza vibaya maisha yake ndani ya klabu hiyo, yanayosababisha kuanza kusahaulika licha ya kiwango chake bora.

“Hakuna maamuzi yaliyofanyika hadi sasa lakini shauku yangu kubwa ni kupata muda mwingi wa kucheza iwe hapa Singida au timu nyingine, siwezi kusema nataka kukimbia ushindani uliopo bali nitapambana kadri ya uwezo wangu ambao umezoeleka.”

Mmoja wa viongozi wa Singida ambaye aliomba kuhifadhiwa jina alisema, tayari viongozi wamefanya makubaliano ya kumpeleka nyota huyo Namungo, wakiamini itakuwa timu itakayompa nafasi ya kucheza ili kulinda kiwango chake kisiweze kuporomoka.

“Makubaliano yamefikiwa kwa kuangalia mustakabali wa mchezaji mwenyewe kutokana na kushindwa kupata nafasi ya kucheza kikosi cha kwanza, sio yeye pekee bali wapo wengine tutakaowatoa pia ili kulinda vipaji vyao,” kilisema chanzo hicho.

Najim ameshindwa kupenya kutokana na viungo wakiwemo, Emmanuel Keyekeh aliyetokea FC Samartex ya kwao Ghana, Josaphat Arthur Bada aliyetokea ASEC Mimosas ya Ivory Coast, huku mwingine akiwa ni Mohamed Damaro aliyetoka Hafia FC ya Guinea.

Nyota hao kiujumla wamechangia mabao 10 kati ya 16 yaliyofungwa msimu huu, ambapo Keyekeh amefunga mawili na kuasisti mawili, huku Josaphat akitupia kambani mawili na kuasisti matatu, wakati kwa Damaro amefunga bao moja tu.

Related Posts