Mkama Sharp ni jina linaloleta kumbukumbu ya askari polisi maarufu jijini Dar es Salaam miaka ya 1980 hadi 1990.
Umaarufu wake haukuwa kwenye utekelezaji wa majukumu yake pekee, bali hata kwa mwonekano wake, ubunifu na uchapakazi wake.
Ni askari polisi aliyeipenda kazi yake na nadhifu wa mavazi, huku akitembea na vitendea kazi muhimu.
Ungekutana naye, kiunoni ungemuona kaweka bastola, rungu, pingu na kifuani alining’iniza kipaza sauti alichokitumia kutoa maelekezo.
Ndiye aliyebuni utaratibu wa abiria kuingia kwenye Uda kwa kupanga mstari baada ya kushamiri wizi wa maungoni kama wizi wa saa na kuchomoa pesa mifukoni.
Mkama Sharp, kiboko ya vibaka alikuwa mwembamba mrefu na mwenye sura isiyo na woga au sura ya kutisha, lakini alikuwa mtu rahimu sana anapokuwa kwenye mavazi ya kiraia.
Alikuwa askari polisi wa kituo cha Msimbazi Kariakoo, aliweza kudhibiti magenge ya vibaka, wahuni na masela katika Soko la Kariakoo.
Si vibaka, wahuni na masela, pia alisimamia utulivu kwa kuzuia vurugu kwenye maeneo ya michezo, hasa uwanja wa Taifa zinapocheza timu kongwe na watani wa jadi yaani Simba na Yanga.
Alizunguka kwa mbwembwe huku akiwa ameinua mabega na kutangaza hataki vurugu, na watu walitii. Na kwa nini usitii labda hujitaki!
Pia, kwenye mchezo wa ngumi za kulipwa pale Railway Gerezani na hasa panapokuwa na masumbwi ya mabondia nyota Stanley Mabesi ‘Ninja’ na Joseph Marwa, Rashid Matumla ‘Snake Boy na bondia nyota wa Zambia Charles Libondo (Mawe ), nako alisimamia utulivu ili waliolipa fedha zao kupata burudani ya masumbwi wafurahie.
Mkama Sharp pia alikuwa kiboko cha makondakta na madereva jeuri na sugu wa daladala. Kuna siku mwanafunzi alisukumwa na kondakta asiingie kwenye daladala kwa kuwa wanafunzi walikuwa wakilipa nauli ndogo huku wakubwa wakilipa nauli ya Sh5, ambayo zamani iliitwa ‘dala’ na ndio mwanzo wa jina daladala. Unajua alichofanya? Alishusha abiria wote na kuamuru waingie wanafunzi pekee.
Ni askari aliyejipenda viatu vyake vya kazi vilipigwa rangi na kung’aa, sare za kazi zilikuwa safi na zimepigwa pasi huku akitembea kwa madaha licha ya umbo lake la ‘mbavu nne’ kwa maana ya wembamba.
Sharp ambaye anaelezwa alifariki dunia mwaka 2007 na kuzikwa kwao mkoani Mara, aliishi maeneo jirani na Jangwani kwenye makazi ya raia wa kawaida, aliogopwa na vibaka lakini alipendwa na watu.
Alikuwa na uwezo wa kwenda kukamata kundi la vibaka hata 20 na wote akawafunga mashati na kuwapeleka mpaka polisi. Alikuwa akisema sitaki vurugu watu walitii na kutulia kama wamemwagiwa maji.
Masela walikuwa wanapiga magoti na wanajisalimisha kwake na ama bangi walizokuwa nazo na vitu vya wizi walivyoiba na walikuwa wakiongoza wenyewe kituoni Polisi.
Kuna wakati aliwakuta wanafunzi wa Shule ya Sekondari Minaki wakiwa wamekaa eneo la DDC Kariakoo wakiwa wameachwa na usafiri na wana njaa, aliwachukua hadi hotelini na kuamuru mwenye hoteli awape wanafunzi hao chakula na alitii.
Umaarufu wake ulianzia alipokuwa na cheo cha koplo miaka ya 1988. Alipandishwa cheo na kuwa sajenti mwaka 1990 na aliyekua Mkuu wa Jeshi la Polisi wakati huo IGP Harun Mahundi, kutokana na utendaji wake mzuri wa kazi za polisi.
Umaarufu wa Sharp ulitokana na ubunifu wake wakati ulipozuka wizi wa maungoni kwa abiria wa usafiri wa umma maarufu kama Uda.
Abiria wengi walilalamika kuibiwa fedha na saa za mikononi, wakati wa kugombania kupanda mabasi hayo kutokana na wingi wa abiria kwenye vituo vya Uda.
Sharp wakati huo akiwa PC yaani ‘Police constable’ alianzisha mtindo wa kusimamia upakiaji wa abiria akiwataka wasimame mstari ili wapande basi kwa utaratibu na kila abiria akijua mtu aliyopo nyuma yake na hivyo ikawa sio rahisi watu kuibiana.
Alipewa jina ‘Sharp’ kutokana na uimara wake kwenye kupanga na kusimamia kile anachokiamini akijua kitaleta tija.
Pia, alikua akitembea kwa miguu umbali mrefu kutoka Msimbazi hadi Posta ama Stesheni, Magomeni Mapipa na Keko Magurumbasi kwa ajili hiyohiyo ya kusimamia upandaji wa mabasi, hasa kwa nyakati za jioni watu wakitoka kazini kurudi makwao.
Mbali na vitendea kazi kama kirungu, bastola, pingu na kipaza sauti alichokinunua mwenyewe, pia alibeba fimbo aliyoitumia kutoa maelekezo.
Basi la Uda likifika kituoni, Sharp anakua wa kwanza kusimama mlangoni na kuupa mgongo mlango wa basi kisha hunyoosha fimbo yake ikiwa ni ishara ya kunyoosha mstari.
Pia, Sharp alijielekeza kwenye kusimamia ugawaji wa bidhaa adimu kwenye maduka ya RTC na Ugawaji. Kote huko alielekeza watu wapange mstari kwa ajili ya kupata mahitaji yaliyokua adimu enzi hizo.
Omar Mahita alipoteuliwa kwenye nafasi ya IGP, Sharp alipandishwa cheo kutoka sajenti hadi kuwa mkuu wa kituo (Staff Sergeant /Station Sergeant) na baadaye alipandishwa na kuwa Mkaguzi Msaidizi wa Polisi cheo ambacho alistaafu nacho.
Nidhamu ya vikao vya kazi
Pia, Sharp alikua hakosi kikao chochote cha kazi kiwe cha mkuu wa kituo (OCS), mkuu wa polisi wa wilaya (OCD), kamanda wa polisi mkoa (RPC) ama Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP).
Ilikuwa lazima ahudhurie kusikiliza taarifa na miongozo mbalimbali inayotolewa, lakini pia kusimamia nidhamu kwa askari waliopo chini yake, ambao nao walikua wakimheshimu sana.
Karibu vyeo vyake vyote vya Polisi, Sharp alikuwa akipewa na wakuu wa Jeshi la Polisi wenyewe kwenye mikutano ya viongozi kuanzia kwa sababu ya kuwa askari wa mfano.
Kila mkutano, kiongozi mwenye mkutano, wakiwamo wakuu wa jeshi hilo, lazima auliziwe kama yupo na ikionekana yupo kiongozi aliridhika na kuendelea na kikao.
Viongozi mbalimbali wa polisi hasa ma-IGP kila walipomuona Sharp kwenye vikao vyao, walimtolea mfano mzuri wa askari polisi mwenye ubunifu na hodari kwenye kazi.