Mollel ainusa Dubai, Lina Tour zamu ya Dar

MCHEZA gofu ya kulipwa kutoka Arusha, Nuru Mollel ana asilimia kubwa ya kwenda Dubai endapo ataibuka mshindi wa jumla kwenye michuano ya Lina PG Tour, inayotarajiwa kuanza wiki ijayo, jijini Dar es Salaam.

Michuano hiyo inatarajiwa kupigwa kwenye viwanja vya Dar es Salaam Gymkhana kuanzia Desemba 19 hadi 22 mwaka huu.

Road to Dubai ndiyo kauli ya mbiu ya Lina PG Tour na mshindi wa jumla atakata tiketi ya kucheza mashindano yenye hadhi ya kidunia Dubai, Falme za Kiarabu.

Mollel ambaye hadi sasa ameshinda raundi tatu kati ya tano za Lina PG Tour, ndiye mwenye nafasi nzuri ya kumaliza mshindi wa jumla, hata asiposhinda raundi ya mwisho.

Kwa sasa Mollel anaendelea na mazoezi katika viwanja vya Arusha Gymkhana na alisema yuko tayari kwa ajili ya raundi ya tano licha ya kuuona upinzani mkali kutoka kwa wachezaji kama Fadhil Nkya na Isaack Wanyeche wanaomfuatia kwa wingi wa pointi.

Hadi kutamatika kwa raundi ya nne mjini Moshi mwishoni mwa mwezi Oktoba, Mollel alikuwa mbele ya wapinzani wake wa karibu kwa tofauti ya pointi 18, akiwa tayari amejikusanyia jumla ya pointi 76 kwa ushindi wa 1-3-1-1 katika raundi zote nne.

Kwa kushinda raundi tatu za Lina PG Tour pekee, Mollel amejihakikishia Sh20 milioni na mshindi wa kwanza wa kila raundi kwa upande wa gofu ya kulipwa huzawadiwa Sh6.8 milioni kutoka kwa waandaji wa mashindano hayo.

Wanaomfuatia Mollel ni Nkya na Wanyeche kila mmoja akiwa na pointi 58, huku Hassan Kadio wa Dar es Salaam akishika nafasi ya nne na pointi 50 na wa tano ni Frank Mwinuka pia wa Dar es Salaam aliyevuna pointi 49.

Raundi hizo nne zilifanyika katika viwanja vya mikoa ya Kilimanjaro, Morogoro na Arusha.

Related Posts