Mwenyekiti Baraza la Wazee Yanga afariki dunia kwa ajali, kuzikwa leo

ALIYEKUWA Mwenyekiti wa Baraza la Wazee Yanga, Abdulrahman Mnero aliyefariki dunia jana kwa ajali ya barabarani anatarajiwa kuzikwa saa 10:00 jioni ya leo huko Mbagala Kingugi, jijini Dar es Salaam.

Munelo alipata ajali jana katika eneo la Mbagala Zakhem baada ya bodaboda aliyokuwa amepanda pamoja na abiria mwingine (maarufu mshikaki), kugongwa na lori kabla ya kukumbwa na mauti muda mfupi baadaye, huku dereva wa bodaboda hiyo ikielezwa alifanikiwa kukimbia eneo la tukio.

Mwenyekiti wa Matawi ya Yanga Mkoa wa Dar es Salaam, Shaban Mgonja ‘Uda’ ameithibitishia Mwanaspoti kuhusu tukio hilo na taratibu za mazishi ya kiongozi huyo, huku akiwataka Wanayanga ambao watakuwa na nafasi kwenda kumsindikiza mwenzao.

“Alipata ajali jana Mbagala Zakhem, walipanda watu wawili, dereva alipoona hawezi kukwepa gari akaruka na kukimbia, hivyo ikawakanyaga abiria akiwemo mzee wetu Mnero,” alisema Uda na kuongeza;

“Marehemu alikuwa katika nafasi hiyo tangu uongozi wa Dk Mshindo Msolla hadi kipindi hiki cha Injinia Hersi Said.”

Related Posts