Rais Macron aahidi kumtangaza Waziri Mkuu Mpya – DW – 11.12.2024

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron alikutana kwa mazungumzo Jumanne jioni katika Ikulu ya Elysée na viongozi wa vyama mbalimbali vya siasa ili kujaribu kumaliza mkwamo wa kisiasa kufuatia kuondolewa madarakani kwa Waziri Mkuu Michel Barnier.

Macron amesema katika miaka hii miwili ya kukamilisha muhula wake unaomalizika mwaka 2027, hatarajii kulivunja tena Bunge kama alivyofanya mwezi Juni baada ya chama cha siasa kali za mrengo wa kulia kupata ushindi katika uchaguzi wa Bunge la Ulaya.

Soma pia: Macron autuhumu upinzani “kuihujumu” jamhuri

Rais huyo wa Ufaransa aliwaalika kwa mazungumzo wakuu wa vyama vyote vya siasa ispokuwa viongozi vyama vya siasa kali za mrengo wa kulia wa National Rally (RN) Marine Le Pen na yule wa chama cha siasa kali za mrengo wa kushoto wa (LFI) Jean-Luc Mélenchon ambao hadi sasa ndio wenye wabunge wengi.

Bi Le Pen alijisifu kwa msimamo wake na kusema kutoalikwa na Macron ni sawa na kutunukiwa “medali ya upinzani” wakati vyama vikuu vya siasa vikikusanyika katika kile alichokiita “karamu ya kugawana madaraka serikalini”. Kwa upande wake Mélenchon amewaonya washirika wake wa mrengo wa kushoto kwamba wangekabiliwa na matokeo mabaya ikiwa watajitenga.

Wito wa vyama vya siasa za mrengo wa kushoto

Mwenyekiti wa chama cha kisoshalisti nchini Ufaransa Olivier Faure
Mwenyekiti wa chama cha kisoshalisti nchini Ufaransa Olivier FaurePicha: Julien Mattia / Le Pictorium/IMAGO

Mwenyekiti wa chama cha kisoshalisti nchini Ufaransa amesisitiza msimamo wa chama chake cha mrengo wa kushoto kwamba kitaacha mara moja kuendelea kushiriki kwenye mazungumzo ya kuunda serikali ya muungano iwapo Rais Macron atamteua waziri mkuu mwingine kutoka upande unaoelemea mrengo wa kulia.

Katika barua kwa Rais Emmanuel Macron, iliyochapishwa pia kwenye mtandao wa kijamii wa X, mwenyekiti wa chama cha Kisoshalisti Olivier Faure amesisitiza kwamba angelijiondoa mara moja kwenye mazungumzo na Macron ikiwa atamteua waziri mkuu mwingine kutoka chama cha siasa za mrengo wa kulia.

Soma pia: Wanasiasa wa Ufaransa wanakutana kujadili serikali mpya

Olivier Faure ambaye alihudhuria amesema mkutano huo ulikuwa muhimu lakini haukuwa jumuishi na kusema kuwa kwa sasa uamuzi wa mwisho anao Macron ili kumaliza mzozo huu wa kisiasa kwa kumteua waziri mkuu kutoka chama cha siasa za mrengo wa kushoto.

” Tunataka waziri mkuu wa mrengo wa kushoto. Rais anapaswa kutueleza kwa nini angemchagua waziri mkuu wa mrengo wa kulia kama alivyofanya mara ya kwanza na matokeo yake sote tunayajua. Kwa kuwa tayari amejaribu upande wa mrengo wa kulia, lazima sasa ajaribu Kushoto na kuhakikisha kuwa Wafaransa wanahisi kuwakilishwa, wamejumuishwa, jambo ambalo hawajalihisi kwa miezi kadhaa sasa.”

Sheria maalum ya bajeti kuwasilishwa Jumatano

Hatua ya Macron inajiri wakati mawaziri wake wakiendelea kutoa ufafanuzi kwa umma kuhusu bajeti ya Ufaransa ya mwaka ujao wa 2025. Ofisi ya Macron imesema sheria maalum ya bajeti ili kuruhusu serikali ya Ufaransa kuendelea kufanya kazi itawasilishwa hii leo Jumatano. Wabunge watajadili mswada huo mnamo Desemba 16, huku pande nyingi zikisema zitauunga mkono ili kudumisha hali ya utulivu wa kiuchumi.

Waziri Mkuu wa Ufaransa aliyeondolewa madarakani Michel Barnier
Waziri Mkuu wa Ufaransa aliyeondolewa madarakani Michel BarnierPicha: Sarah Meyssonnier/REUTERS

Sheria hiyo inahusu kuidhinisha serikali kuendelea kukusanya ushuru hadi bajeti mpya ipitishwe na bunge na pia kuiruhusu serikali na mfuko wa hifadhi ya jamii kuendelea kukopa kwenye masoko ya fedha ili kuepuka usumbufu wowote wa malipo yaliyo muhimu.

Yote haya yanajiri baada ya uongozi wa  Waziri Mkuu Michel Barnier kuangushwa na Bunge kutokana na rasimu yake ya bajeti ambayo ilidhamiria kubana matumizi kwenye mfuko unaoshughulikia gharama za kijamii.

Barnier aliungwa mkono na chama cha kihafidhina pamoja na muungano wa vyama vya siasa za mrengo wa kati wa Macron. Lakini muungano huo ulishindwa kupata wingi wa wabunge unaohitajika na hatimae kuuangushwa na muungano wa vyama vya siasa kali za mrengo wa kushoto na kulia.

Soma pia: Macron aapa kusalia madarakani baada ya serikali kuporomoka

Haikuwa wazi ni vyama gani vitakavyomuunga mkono rais Macron ili aweze kuunda serikali mpya. Mmoja wa washauri wa rais amesema kuwa katika mkutano wa jana Jumanne, Macron alielezea umuhimu wa kuunda umoja wa kisiasa ili kujikwamua na utegemezi kwa chama cha RN.

Kiongozi wa chama cha kijani Marine Tondelier alisema alipokuwa akiondoka kwenye mkutano huo kwamba kambi ya rais Macron haiko tayari kwa maelewano au makubaliano yoyote, lakini  akasisitiza haja ya rais Macron ya kutokitegemea tena chama cha RN cha Lepen ili kuunda serikali.

Vyanzo: (AP, RTR, AFP)

 

Related Posts