Na Imani Mtumwa. Maelezo 10.12.2024
Waziri Mkuu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe, Kassim Majaliwa Majaliwa amesema Mpango wa kitaifa wa maendeleo wa 2050 ni jambo kubwa na nimuhimu kwa taifa letu kutokana na wakati unavyoweza kukua.
Ameyasema hayo katika Uzinduzi wa Rasimu ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 katika Ukumbi wa Golden Tulip Uwanja wa Ndege nje kidogo ya mji wa Zanzibar.
Aidha Majaliwa alizishukuru Tume za mipango zote mbili ya Tanzania bara na Zanzibar pamoja na kuishukuru kamati ya ukusanyaji wa maoni na walioshiriki utoaji wa maoni hayo kwani imekuwa ni rahisi kupatikana na kuundwa kwa rasimu hiyo.
Majaliwa ameongeza kuwa katika utekelezaji wa majukumu hayo kamati imefanya kazi ya kuielemisha jamii juu ya mpango wa dira ili kuendeleza mpango wa dira hiyo
Hata hivyo amesema kamati itaendelea kusimamia na kuratibu mpango wa kitaifa wa kimaendeleo kwa kuengeza yale yote ambayo hayakuwemo ama hayajaingizwa katika rasimu ya kwaza
Aidha amezitaka Tume za Mipango zote mbili kama ni Sekretarieti zihakikishe zinaratibu zoezi la uhakiki wa Dira kwa ufanisi wa hali ya juu pamoja na kuzitaka kusambaza Rasimu hiyo katika vyombo mbalimbali na kuweka mfumo rahisi wa kupokea maoni ya wadau wote na jamii kwa ujumla.
Akisoma taarifa fupi Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji Prof.Kitali A Mkumbo amesema kufuatia kwa Utekelezaji wa mpango huo ni maagizo ya Mhe Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan kuitaka tume ya mipango kuandaa na kuandika dira nyengine ya mpango wa maendeleo nchini.
Hata hivyo amesema mchakato huo ulijumuisha kwa kiasi kikubwa wadau wa maendeleo na maoni yao yalikua ya uhuru na yalisaidia kuunda rasimu ya dira ya kitaifa ya maendeleo 2050
Nae Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Fedha na Mipango Saada Mkuya Salum amesema katika kutaarisha mpango huo hatua mbali mbali zimechukuliwa katika ukusanyaji wa maoni kupitia kamati ya kitaifa.
Vile vile amesema katika ukusanyaji wa maoni washiriki wengi waliotoa maoni ni kinamama kwani ndio ambao wanapata changamoto nyingi katika jamii na kuitaka Serikali kingamuzi kwa sasa vishuke bei.
Pia ameeleza ni namna gani wataweka pesa za kuendeleza Rasimu hiyo ili watendaji waweze kufanya kazi hiyo kwa wepesi na kwa weledi.
Hatahivyo amesema kupitia wizara yake itahakikisha inasimamia kukusanya maoni katika jamii ili kuendeleza dira ya mwaka 2050
Hafla ya Uzinduzi wa Rasimu ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 umehudhuriwa na viongozi mbali mbali wa serikali wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na wa serikali ya mapinduzi ya Zanzibar wadau wa maendeleo taasisi binafsi na wananchi ambapo mpango huo umezinduliwa ramsi na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt Hussein Ali Mwinyi.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Hussein Ali Mwinyi akionesha Kitabu cha Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 baada ya Kuizindua hafla iliofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Golden Tulip Uwanja wa Ndege Zanzibar.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Hussein Ali Mwinyi (katikati)akiwa katika Picha ya Pamoja na Viongozi mbalimbali katika hafla ya Uzinduzi wa Rasimu ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050- hafla iliofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Golden Tulip Uwanja wa Ndege Zanzibar.
PICHA NA YUSSUF SIMAI,MAELEZO ZANZIBAR.11/12/2024.