Scholz ameongeza kuwa Rais wa Urusi Vladimir Putin hajatimiza hata lengo moja la nchi yake katika vita vinavyoendelea kati ya Ukraine na Urusi.
Katika hotuba aliyoitoa kwenye kongamano la kibiashara kati ya Ujerumani na Ukraine lililofanyika mji mkuu wa Ujerumani Berlin, Scholz amesema uwekezaji nchini Ukraine leo na katika miaka ijayo ni sawa na kuwekeza kwa mwanachama ajaye wa Umoja wa Ulaya.
Kiongozi huyo wa Ujerumani ameongeza kuwa baada ya vita, dunia itaona ukuaji na fursa za maendeleo zitakazojitokeza nchini Ukraine, akilinganisha uwezo wa kiuchumi wa nchi hiyo na ule wa mataifa ya Ulaya Mashariki yaliyojiunga na Umoja wa Ulaya baada ya kuanguka kwa Umoja wa Kisovieti.
Amesema biashara kati ya Ujerumani na Ukraine imeongezeka kutoka euro bilioni nane mnamo mwaka 2021 hadi karibu euro bilioni 10 mwaka wa 2023. Kwa sasa, Ujerumani ina takriban kampuni 2,000 zinazohudumu nchini Ukraine, huku zikijihusisha zaidi na biashara katika sekta ya usalama na ulinzi, bidhaa za kemikali na sekta nyengine muhimu.
Miundo mbinu muhimu ya Ukraine yaharibiwa
Kansela huyo wa Ujerumani ameongeza kuwa anataraji ushirikiano wa kibiashara utaongezeka hasa katika sekta ya nishati kutokana na ukweli kwamba, miundombinu ya nishati nchini Ukraine imeharibiwa baada ya kushambuliwa mara kwa mara na jeshi la Urusi.
Kulingana na ofisi ya takwimu, Ujerumani inaagiza zaidi bidhaa za kilimo, chakula na sehemu za magari kutoka Ukraine.
Akizungumza katika jukwaa hilo hilo, Waziri Mkuu wa Ukraine Denys Shmygal amesisitiza umuhimu wa uwekezaji wa kampuni binafsi katika mchakato wa kuijenga upya nchi hiyo.
Shmygal amesema kila sarafu moja ya euro inayowekezwa ndani ya Ukraine ina mchango mkubwa kwa mustakabali sio tu wa nchi hiyo bali pia ndani ya Umoja wa Ulaya.
Kando na suala la ushirikiano wa kibiashara kati ya Berlin na Kyiv, Scholz ameliambia kongamano hilo la mjini Berlin kuwa Ujerumani inaiunga mkono Ukraine katika azma yake ya kutafuta kile alichokiita “amani ya haki” na kuvimaliza kabisa vita vilivyoanzishwa na uvamizi wa Urusi.