MSHAMBULIAJI wa Azam, Nassor Saadun ameshindwa kujizuia na kumtaja beki wa Tanzania Prisons, Vedastus Mwihambi ni ‘mtu kazi’ kati ya mabeki aliokumbana nao katika mechi za Ligi Kuu Bara hadi sasa, huku akimvulia kofia pia beki anayecheza naye timu moja, Yoro Mamadou Diaby raia wa Mali.
Saadun aliyefunga mabao manne hadi sasa, aliliambia Mwanaspoti Mwihambi anayemiliki bao moja hadi sasa katika ligi hiyo ni mmoja ya mabeki hodari kutokana na umakini wa kuzuia washambuliaji na utulivu wa kuokoa hatari nyingi.
Saadun aliyekuwa akiichezea Geita Gold msimu uliopita, alisema Mwihambi na Diaby wana sifa zinazofanana za utulivu katika kuokoa hatari pindi mpira unapokuwa eneo lao, pia wana uwezo wa kutuliza mashambulizi na kuanzisha mipira inayofika kwa wahusika.
“Kwangu mimi ni kati ya mabeki ambao wamefanya kazi nzuri hadi sasa wakati duru la kwanza likiwa linakaribia kumalizika, Mwihambi ni mmoja ya mabeki ambao ni vigumu kumpita kwa utulivu alionao na jinsi anavyotumia akili, lakini kwa Diaby namwona jinsi anavyojituma kuanzia katika mazoezi hadi mechi za ushindani, hana papara anakuwa anajiamini na anachokifanya,” alisema Saadun.
Alisema duru la pili anaamini mabeki hao watafanya makubwa zaidi ya kile walichokionyesha ngwe ya kwanza, kwani unakuwa na ushindani mkubwa, kila timu ikipigania malengo yake.