Sukuk, inayojulikana pia kama hati fungani za Kiislamu, imekuwa mbadala maarufu wa uwekezaji katika masoko ya hisa na mitaji duniani.
Uwekezaji huo unasimamiwa kwa mujibu wa Shariah, ambayo ni kanuni za kifedha za Kiislamu, na inatoa fursa ya kuwekeza katika miradi mbalimbali kwa kufuata misingi ya kuepuka riba na miamala isiyokubalika kisharia.
Tofauti na hati fungani za kawaida ambapo mwekezaji huwa mdai (creditor) wa kampuni au serikali, na hupokea riba ya kudumu hadi hati hiyo inapoiva, Sukuk inatoa hadhi ya umiliki katika mali au miradi ya uwekezaji. Hii inamaanisha kuwa wawekezaji wana haki ya kupokea moja kwa moja mapato yanayotokana na umiliki wa mali au uendeshaji wa miradi hiyo.
Kwa mfano, Serikali au kampuni inaweza kutoa Sukuk ili kukusanya fedha kwa ajili ya miradi ya miundombinu, ujenzi wa majengo, au uzalishaji wa nishati.
Mapato yanayopatikana kutokana na mali hizo, kama kodi za majengo au mapato ya biashara, hugawanywa kwa wawekezaji kama faida kwa muda maalumu, hadi pale amana zote zitakaporudishwa na umiliki wa mradi kubaki kwa mtoaji wa Sukuk.
Msingi huu muhimu unajenga dhana muhimu katika Sukuk, ambayo ni kuepuka riba kwa kuzingatia usawa na uadilifu. Pia, fedha zinazokusanywa kwa njia hii zinaweza kuelekezwa kwenye miradi ya kijamii na kiuchumi inayoonekana kuwa halali kwa mujibu wa Shariah.
Vilevile, faida za wawekezaji wa Sukuk hubadilika kulingana na ufanisi wa mradi husika. Kwa mfano, katika mradi wa ujenzi wa majumba ya makazi, mapato kutokana na kodi za upangishaji yanaweza kuongezeka au kupungua, kulingana na hali ya soko.
Hii inamaanisha wawekezaji wanakubali hatari za kibiashara (profit and risk sharing), tofauti na mifumo ya riba anayopokea mdai wa hati fungani (fixed coupon rate).
Kwa mtazamo wa Shariah, dhana hii huondoa mazingira ya riba na kuleta uwiano wa haki katika miamala ya kibiashara. Kwa misingi hiyo, Sukuk iwe ni njia bora ya uwekezaji inayohimiza uadilifu, uwazi, na uwajibikaji wa pamoja kati ya wahusika wote kwa kuzingatia mabadiliko ya biashara au uwekezaji uliofanyika.
Sukuk inaweza kuwa kwa aina mbalimbali, kwa mfano, Sukuk Ijarah, ambapo wawekezaji hupata mapato ya kodi kutoka kwa mali inayokodishwa. Sukuk Mudarabah, ambapo faida zinazozalishwa na mradi hugawanywa kati ya pande zinazohusika kulingana na makubaliano.
Muundo mwingine ni Sukuk Musharakah, ambapo pande zote zinachangia mtaji na kugawana faida na hasara, huku Murabaha ikihusiana na mauzo ya gharama za ziada na Istisna ikihusisha ufadhili wa ujenzi.
Kulingana na Benki ya Dunia, utoaji wa Sukuk umeongezeka kwa asilimia 164 kutoka 2010 hadi 2020, ikiwa ni ishara ya ukuaji. Malaysia, Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu ni miongoni mwa nchi viranja katika matumizi ya mtindo huo wa kukusanya mtaji kwa ajili ya uwekezaji.
Katika nchi nyingine kuna umuhimu wa kuendelea kuboresha masoko ya mitaji, kanuni na sheria mpya zinazoweza kutoa mwongozo na kutoa fursa kujumuisha mtindo mbadala wa kifedha kwa lengo la kuchagiza kasi ya maendeleo ya kiuchumi kupitia uwekezaji.