TANESCO tunathamini wadau wa maendeleo – Mha. Nyamo-Hanga

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Mha. Gissima Nyamo-Hanga amesema kuwa TANESCO inathamini michango inayotolewa na wadau wa maendeleo katika kuimarisha sekta ya nishati nchini.

Mha. Nyamo-Hanga ameyasema hayo Mombasa nchini Kenya wakati akitoa wasilisho kuhusu Sekta ya Umeme Tanzania katika mkutano uliowakutanisha nchi Wanachama wa Mashariki mwa Afirka (EAPP) na wadau mbalimbali katika sekta ya umeme.

“Tunatambua ushiriki wa wadau wa Maendeleo katika kuongeza biashara ya umeme nchini Tanzania kwa kufadhili miundombinu ya mfumo wa umeme katika maeneo ya uzalishaji wa umeme na mifumo ya Usambazaji wa umeme.” Amesema Mha. Nyamo-Hanga.

Kuhusu wawekezaji binafsi katika sekta ya umeme, Mha. Nyamo-Hanga amesema kwa upande wa uzalishaji umeme wapo wawekezaji na kutanabaisha kuwa kwa sasa hakuna wawekezaji binafsi kwa upande wa usambazaji wa umeme na kwa upande wa mfumo wa usafirishaji wa umeme unaendeshwa na Serikali kupitia TANESCO.

Mha. Nyamo-Hanga ameongeza kuwa, Serikali inaendelea kuangalia njia bora ya kushirikisha sekta binafsi katika ujenzi na uendeshaji wa mifumo ya usafirishaji wa umeme bila kuathiri uthabiti wa mifumo hiyo.

Akielezea faida zitakazopatikana kutokana na Tanzania kushiriki soko la Kanda la biashara ya umeme kwa kuingia katika muunganiko wa kuuziana na kununua umeme kwa upande wa Mashariki (EAPP) na Kusini mwa Afrika (SAPP), Mha. Nyamo-Hanga amesema nchi itafaidika kwa kuuza umeme kutokana na uwekezaji mkubwa Serikali inaoufanya katika eneo la uzalishaji wa umeme.

Amesema Kijiografia Tanzania ipo katikati Nchi zilizo upande wa Kaskazini mwa Afirika zitakapo hitaji kufanya biashara ya umeme na Nchi zilizo Kusini mwa Afrika na zitahitajika kuupitisha umeme katika miundombinu ya kusafirishia umeme ya Tanzania hivyo Nchi itafaidika kwa kupata fedha za kigeni.

Amesema pia kwa upande mwingine kutakuwa utulivu wa gridi kupitia kuunganishwa kwa gridi ya Kanda kwa karibu. Gridi ya kanda inayounganishwa itatoa fursa ya kuingiza nishati mbadala kutokana na akiba ya pamoja ya mifumo, kuongezeka kwa usalama wa ugavi wa umeme na fursa za kuuza/kununua umeme wa bei nafuu kutoka soko la kanda

    

 

Related Posts