Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Umoja wa Ulaya zimesaini Tamko la Pamoja kama alama ya makubaliano ya kuendelea kuunga mkono jitihada za maendeleo kwa maslahi ya pande zote mbili.
Tamko hilo limesainiwa wakati wa kuhitimisha majadiliano ya ushirikiano kati ya Tanzania na Umoja wa Ulaya yaliyofanyika tarehe 10 Desemba, 2024 katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar es Salaam chini ya uenyekiti wa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Cosato Chumi (Mb.) ambaye alimwakilisha Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb.) na Mkurugenzi Mtendaji wa Umoja wa Ulaya anayeshughulikia Kanda ya Afrika katika Kurugenzi ya Huduma za Nje ya Umoja wa Ulaya (Europeana External Action Service), Mhe. Balozi Ritha Maria Laranjinha.
Majadiliano hayo ni sehemu ya utekelezaji wa Mkataba wa Samoa, uliosainiwa mwaka 2023, ambao unaelekeza umuhimu wa kuwa na majadiliano ya mara kwa mara kati ya Umoja wa Ulaya na Nchi za Afrika, Karibiani, na Pasifiki (ACP). Tanzania, ikiwa mojawapo ya nchi wanachama wa kundi la ACP, inaendelea kutekeleza wajibu wake kwa kushiriki kikamilifu katika majadiliano haya muhimu kila mwaka kwa lengo la kuimarisha ushirikiano wa kimkakati na Umoja wa Ulaya.
Pamoja na masuala mengine majadiliano hayo yalijikita katika masuala muhimu yanayogusa maslahi ya pande zote, ikiwa ni pamoja na utawala bora, demokrasia, usalama wa baharini, biashara na uwekezaji, na ulinzi na usalama kikanda na kimataifa.
Wakiainisha masuala hayo ya ushirikiano viongozi hao wameeleza kuwa Tanzania na Umoja wa Ulaya zimedhamiria kuimarisha zaidi ushirikiano wa pande mbili chini ya Mkataba wa Samoa. Ushirikiano huu unaendana na Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2020- 2025 na Mpango wa Tatu wa Maendeleo ya Miaka Mitano. Pande zote zimekubaliana kuongeza ushirikiano ili kuhakikisha matokeo chanya na yenye manufaa kwa wananchi.