MENEJA wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA),Kanda ya Ziwa, Mhandisi Imelda Salumi, amewashauri waandishi wa habari mkoani Mwanza,wawe wabunifu na kutafuta maarifa, wafikirie vitu vya pekee katika tasnia ya habari vitakavyowatofautisha na mikoa mingine.
Pia,amewapongeza wanachama wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Mwanza (MPC), kwa juhudi kubwa wanazozifanya kuhakikisha vyombo vya habari vinashirikiana na mamlaka hiyo ya udhibiti wa mawasiliano ili kufikia malengo ya pamoja.
Akifungua Mkutano Mkuu wa MPC,leo Mhandisi Imelda Salum, amesema waandishi wa habari wana nafasi kubwa ya kufikia maeneo mengi ambayo serikali haiwezi kuyafikia bila vyombo vya habari.
“Serikali inataka kuwa na uchumi wa kidijiti haitaki kumwacha mtu nyuma,tutumie teknolojia kutafuta kuyafahamu yanayoendelea duniani kwa maslahi ya jamii kwa sababu ndiko teknolojia inakotupeleka,tusaidieni kuandika habari za maendeleo, biashara na mfumko wa bei,”amesema Mhandisi Imelda.
Amesema wana habari wafikirie zaidi kuleta kitu cha kipekee kitakachoitofautisha Mwanza na mikoa mingine huku akipongeza ushirikiano uliopo baina ya mdhibitiwa (waandishi wa habari) na mdhibiti wa sekta ya mawasiliano (TCRA).
Meneja huyo wa TCRA Kanda ya Ziwa amesema ushirikiano huo unafungua njia ya maendeleo katika sekta ya habari, na kuongeza kuwa Mwanza imekuwa mfano bora wa kushirikiana na Mdhibiti wa sekta ya mawasiliano.
“MPC ina kiu ya kufika mbali kwa kushirikiana na TCRA, na hili ni jambo la kupongezwa. Ushirikiano huu ni muhimu kwa maendeleo ya tasnia yetu ya habari, nadhani Mwanza ni mfano mzuri jinsi vyombo vya habari vinavyoweza kufanya kazi kwa pamoja na mdhibiti,” amesema Mhandisi Imelda.
Meneja huyo ameeleza furaha yake kwa ongezeko la idadi ya wanachama wa MPC kuwa,ukuaji huo wa kasi, takwimu zinaonesha ni kubwa tangu klabu hiyo imeanzishwa na hilo linathibitisha waandishi wa habari wanajiendeleza na kujitahidi kuwa bora zaidi katika kazi zao.
Amewahamasisha waandishi wa habari kuendelea kujitahidi ili waweze kutoa taarifa zinazofaa na zenye manufaa kwa jamii, huku akisisitiza kuwa ni muhimu kuendana na mabadiliko ya teknolojia na ushindani wa soko la habari.
“Ninyi kama wanahabari, nafasi yenu ni kubwa sana. Rai yangu muendelee kutafuta maarifa na kubadilika kulingana na nyakati. Hizi ni zama za ushindani mkubwa, na ili kufanikiwa, ni lazima muwe wabunifu na muendelee kuleta habari zinazovutia na kuleta majibu kwa maswali ya wananchi,” ameongeza meneja.
Aidha, Mhandisi Imelda amewahimiza waandishi wa habari kuacha kutafuta ‘habari za kushtua’ ambazo hazileti ufumbuzi wa changamoto za kijamii,wazingatie umuhimu wa kutoa habari zinazojenga na kuchangia katika maendeleo ya jamii, badala ya kuandika habari zinazolenga tu kutisha, kuzua taharuki au kuwavunja moyo wananchi.
Amesisitiza umuhimu wa wanahabari kuendeleza utamaduni wa kujiongezea maarifa na kutafuta njia mpya za kuboresha kazi zao, kushirikiana katika kutatua changamoto za kiutendaji ili kufikia malengo ya pamoja.
“Changamoto ni sehemu ya kazi yetu, lakini kwa kushirikiana tutakapoweza kuzitatua na kufikia malengo yetu ya pamoja. Ni muhimu kuwa na ushirikiano mzuri katika sekta hii ili tuweze kufanikisha malengo yetu,” amesema Meneja huyo wa TCRA.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa MPC,Edwin Soko amesema ujumbe wa meneja huyo umewatia moyo na kuhamasisha waandishi wa habari kuendeleza juhudi zao za kuleta mabadiliko katika sekta ya habari, huku wakizingatia maadili na kutoa taarifa zenye tija kwa jamii.