Waitwa kuanzisha utalii wa utamaduni Kinapa

Moshi. Wananchi wanaoishi maeneo yanayozunguka Hifadhi ya Taifa ya Kilimanjaro (Kinapa), wametakiwa kuanzisha utalii wa kiutamaduni ili kuvutia wageni wanaopanda Mlima Kilimanjaro na kukuza kipato chao.

Wito huo umetolewa leo Jumatano Desemba 11, 2024 na Naibu Katibu Mkuu wa Maliasili na Utalii, Nkoba Mabula wakati wa mapokezi ya wapanda mlima 300 waliopanda Mlima Kilimanjaro kupitia kampeni ya Twenzetu Kileleni.

Lengo ilikuwa  kuadhimisha miaka 63 ya Uhuru wa Tanganyika, wakiongozwa na wanajeshi wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).

Mabula amesisitiza kuwa kuanzisha utalii wa kiutamaduni kutasaidia wananchi kuachana na shughuli zinazoharibu mazingira, kama vile ukataji miti kiholela na kuwasha moto hovyo, badala yake wachangie ukuaji wa uchumi. “Tunaomba wananchi wa maeneo haya watumie fursa za kiutamaduni kuimarisha kipato chao kwa kuwavutia wageni wanaopanda Mlima Kilimanjaro kutembelea maeneo yao,” amesema Mabula.

Aidha, ameonya kuhusu madhara ya moto na mabadiliko ya tabianchi, akisema athari hizo zimechangia kupungua kwa barafu kwenye kilele cha Mlima Kilimanjaro.

“Huu ni mlima wa kipekee wenye sifa duniani si kwa urefu tu bali pia kwa barafu zake, na tunapaswa kuhifadhi mazingira yake kwa faida ya vizazi vijavyo,” ameongeza.

Mabula pia amesema mwaka 2024, Mlima Kilimanjaro ulitunukiwa tuzo ya Kivutio Bora cha Utalii barani Afrika, ukishinda hifadhi maarufu za nchi nyingine duniani.

Mlima huu unachangia kwa kiasi kikubwa katika uchumi wa Mkoa wa Kilimanjaro, mikoa jirani na taifa kwa ujumla, huku ukitoa ajira zaidi ya 300,000 kila mwaka.

Kanali Deus Babuu wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), aliyewaongoza wapanda mlima hao, amewapongeza waongoza watalii kwa kazi yao kubwa na kutoa wito kwa mabalozi waliopanda mlima kuutangaza zaidi mlima huo kimataifa.

Na amesisitiza umuhimu wa kundi hilo kupewa motisha kutokana na mchango wao katika utalii wa mlima huo.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Tanapa, Jenerali mstaafu George Waitara amesema  juhudi zinaendelea kuboresha miundombinu ya malazi, barabara na huduma za uokoaji katika Mlima Kilimanjaro ili kuvutia watalii wengi zaidi.

Naibu Kamishna wa Uhifadhi na Maendeleo ya Biashara kutoka Tanapa, Massana Mwishawa amesema zaidi ya asilimia 80 ya washiriki wa kampeni hiyo wamefanikiwa kufika kileleni, jambo lililoonyesha mshikamano wa Watanzania.

Washiriki hao walitumia njia za Lemosho, Machame na Marangu, huku wakijumuisha wanajeshi wa JWTZ, mabalozi tisa, watu wenye ulemavu, na wengine kutoka taasisi mbalimbali.

Kampeni ya Twenzetu Kileleni imetoa ujumbe wa uzalendo na umuhimu wa kuimarisha uhifadhi wa Mlima Kilimanjaro kwa manufaa ya uchumi na urithi wa taifa.

Related Posts