Wamachinga Soko Kuu Kingalu wapinga kuhamishwa

Morogoro. Wamachinga katika Soko Kuu la Chief Kingalu mkoani Morogoro wameeleza masikitiko yao baada ya kupewa notisi ya siku saba kuondoka katika vibanda vyao vilivyo mbele ya soko hilo.

Wamachinga hao wamedai eneo wanaloelekezwa kwenda kufanyia biashara siyo rafiki kwa biashara zao na pia hatua hiyo inakiuka mkataba wa makubaliano uliosainiwa mwaka 2021 baina yao na Halmashauri.

Kwa mujibu wa Kassim Aidan, mmoja wa wafanyabiashara hao, eneo hilo lilijengwa kwa maelekezo ya serikali baada ya Wamachinga kuondolewa barabarani.

 “Hapa tunalipa kodi kwa wakati, lakini wanapotutaka kuhamia na kutupeleka maeneo yasiyokuwa na wateja, inakuwa changamoto, wafanyabiashara sisi tunakataa kwenda huko kwa sababu hakuna biashara,” amesema Aidan.

Mary Chuwa mfanyabiashara mwingine, amelalamikia sehemu mpya waliyoelekezwa kwa kusema ni finyu na tayari ina wafanyabiashara wengine.

 “Tunapewa mikopo na benki wanapotutoa sisi wafanyabiashara hapa wanatarajia tutarudisha vipi fedha za mikopo kama biashara haifanyiki?” amehoji Chuwa.

“Tumeambiwa eneo hili linabadilishwa matumizi na kuwa maegesho ya magari, jambo ambalo walishalitatua kwani walirudisha biashara ndani ya vibanda kupisha maegesho ya magari,” amesema Chuwa.

Ameongeza kuwa hawakushirikishwa na Serikali haijawahi kukaa nao chini kujadili namna ya kuwahamisha.

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro, Lilian Henerico amethibitisha kuwa Wamachinga 94 waliopo katika eneo hilo la soko la Kingalu wameondoshwa.

Amesema hatua hiyo inalenga kupisha ujenzi wa mifumo ya kielektroniki kwa ajili ya maegesho ya kisasa na kuimarisha usalama wa taasisi za kifedha zilizopo karibu na soko hilo.

“Lakini si kweli kuwa tunawaondoa kabisa na kuwaacha wahangaije, tunawapeleka katika mabanda yaliyopo nyuma ya soko na tunaendelea kushirikiana nao kuhakikisha hakuna atakayepoteza biashara yake,” amesema Heneriko.

Mbunge wa Morogoro Mjini, Abdulaziz Abood amewataka wamachinga kuwa watulivu huku akiahidi kushughulikia suala hilo kwa niaba yao.

“Serikali inasisitiza vijana wajiajiri, lakini sasa biashara zimeshaimarika na wanataka kuwatoa bila mpango wa kueleweka hili haliwezekani, nataka uongozi wa Halmashauri uweke wazi mipango ya eneo hili wanataka kulichukua na waeleze hawa wafanyabiashara wanawapekeka wapi,” amesema Abood.

Soko la Chief Kingalu lina jumla ya Wamachinga zaidi ya 500 na uamuzi huo unawahusu rasmi Wamachinga 94 ambao mabanda yao yanatakiwa kupisha eneo hilo la mbele ya soko.

Related Posts