Wanafunzi Mkinga walia na uhaba, uchakavu wa madarasa

Mkinga. Wanafunzi wa Shule ya Msingi Mazolakilifi, iliyopo Kijiji cha Mazola wilayani Mkinga mkoani Tanga, wameomba msaada wa kuboreshewa vyumba vya madarasa yao ambavyo vipo katika hali mbaya, yakiwa yamejaa nyufa na kuhatarisha usalama wao.

Wakizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano ya matundu kumi ya vyoo yaliyojengwa na Shirika lisilo la Serikali la World Vision Tanzania jana Jumanne, Desemba 10, 2024, wanafunzi hao walitoa shukrani kwa msaada huo lakini walisisitiza kuwa bado wanakabiliwa na changamoto kubwa ya majengo ya madarasa.

Wakisoma risala yao mbele ya mgeni rasmi, Mkuu wa Wilaya ya Mkinga, Gilbert Kalima, mwanafunzi Glory Chikawe alisema uhaba wa madarasa umesababisha baadhi ya wanafunzi wa madarasa mawili tofauti kutumia chumba kimoja.

“Kwa sasa, darasa la kwanza na la pili wanasoma katika chumba kimoja na hali hiyo pia ipo kwa darasa la tano na la sita. Tatizo hili linatokana na uchache wa madarasa, tulipaswa kuwa na vyumba saba, lakini tunavyo vinne tu na kati ya hivyo, vingine vimechakaa, vina nyufa na mapaa yake yamechoka,” alisema Glory.

Aliongeza kuwa wakati wa mvua, vyumba hivyo haviwezi kutumika kwa sababu vinavuja, hali inayoongeza changamoto kwa wanafunzi na walimu.

Aidha, shule hiyo inakosa ofisi za walimu na viti vya kutosha kwa ajili ya wanafunzi.

“Tunaomba msaada wa kujengewa madarasa mapya pamoja na viti, kwani hali ya shule yetu ni mbaya sana, si kwa wanafunzi pekee bali pia kwa walimu wetu,” alihitimisha mwanafunzi huyo.

Muonekano wa baadhi ya madarasa ya Shule ya Msingi Mazolakilifi iliyopo kijiji cha Mazola wilaya ya Mkinga Tanga. Picha na Rajabu Athumani

Ofisa Elimu ya Msingi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkinga, Omari Mashaka amethibitisha kuwa Shule ya Msingi Mazolakilifi inakabiliwa na changamoto kubwa ya majengo chakavu, yanayohitaji kufanyiwa ukarabati, huku mengine yakihitaji kubomolewa kabisa kutokana na kuwa ya muda mrefu.

Mashaka alisema halmashauri ina mpango wa kutathmini majengo yanayoweza kukarabatiwa na kupanga utaratibu wa kujenga majengo mapya kufidia yale ambayo hayafai hata kukarabatiwa.

Mkuu wa Wilaya ya Mkinga, Gilbert Kalima akizungumza na wanafunzi wa shule hiyo, aliahidi kuwa serikali itashirikiana na wadau kutatua changamoto hizo kwa haraka.

Alisema tayari ameanza mazungumzo na viongozi wa Shirika la World Vision Tanzania ili kushirikiana na halmashauri kusaidia ujenzi wa madarasa.

Meneja wa Shirika la World Vision Tanzania Kanda ya Kaskazini, Juliana Charles, alisema shirika hilo limechangia ujenzi wa matundu ya vyoo baada ya kupata taarifa kuwa wanafunzi walikuwa wakijisaidia vichakani, huku wengine wakilazimika kurudi nyumbani. Vyoo hivyo, vilivyogharimu Sh86 milioni, vinajumuisha matundu matano kwa wasichana, sehemu ya wavulana, na eneo maalum kwa wasichana waliobalehe.

Charles aliongeza kuwa shirika hilo litashirikiana na serikali kutafuta njia ya kuboresha vyumba vya madarasa, lakini pia akawataka wanafunzi, walimu, na wazazi kuhakikisha vyoo hivyo vinatunzwa vizuri.

Mkazi wa Kijiji cha Mazola, Mtega Ibrahimu alisema majengo ya shule hiyo haijafanyiwa ukarabati kwa muda mrefu kutokana na changamoto mbili kubwa.

“Kwanza, ni mgogoro wa Kijiji cha Mazola na Mazola A kuhusu miradi ya maendeleo, baadhi ya wanakijiji wamegoma kuchangia ujenzi wa shule hiyo hadi miradi mingine ikamilike. Pili ni mgomo baridi wa wananchi wa kutoa michango kutokana na kutoridhishwa na matumizi ya fedha wanazozichanga kutowekwa wazi,” alidai mkazi huyo.

Hyata hivyo, alisema kutokana na mabadiliko yaliyofanyika, hivi sasa wazazi wako tayari kushirikiana na viongozi wapya kufanya kazi za maendeleo ya shule hiyo.

“Wale wa zamani hawakuhamasisha vizuri maendeleo na fedha nyingi hazikufanya kazi iliyokusudiwa,” alidai Mtega.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Mazola, Mbwana Salimu alisema kwa sasa wanajiandaa kukusanya michango ya wananchi kwa ajili ya kuanza ujenzi wa msingi wa madarasa mapya.

Aliahidi pale nguvu za wananchi zitakapofikia kikomo, wataomba msaada kutoka kwa wadau na serikali ili kukamilisha ujenzi huo.

Related Posts