Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kwa kushirikiana na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) pamoja na wadau mbalimbali wameazimisha Siku ya Maadili na Haki za Binadamu mkoani Morogoro kwa kufanya shughuli za kijamii ikiwemo usafi katika Kituo cha Afya cha Sababa, kuwafariji wagonjwa, na zoezi la upandaji miti.
Akizungumza mara baada ya zoezi la usafi katika Kituo cha Afya cha Sababa, Afisa wa TAKUKURU Mkoa wa Morogoro, Bw. Bigambo Thomas Bigambo, amesema kuwa maadhimisho hayo ni muhimu kwa kuhamasisha jamii, hasa viongozi na watumishi wa umma, kutambua jukumu lao katika kupambana na rushwa.
Ameongeza kuwa taifa haliwezi kuendelea ikiwa raia na watumishi wake watakuwa na tabia zisizokuwa na maadili. “Kila mtu anawajibika kukuza maadili katika jamii yake,” amesema.
Hendry Sawe ni Katibu Msaidizi wa Tume ya maadili kanda ya Mashariki amewataka wananchi kutoa taarifa wanapoona uvunjifu wa sheria na maadili kwa watumishi wa umma katika maeneo yao pamoja na viongozi nao kuwajibika ipasavyo katika utekelezaji wa majukumu yao
Kwa upande wake, Dr. Helen Mwayola, Kaimu Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya cha Sababa, alitoa shukrani kwa Sekretarieti ya Maadili na Viongozi wa Umma kwa kuja kutembelea kituo hicho na kushirikiana nao katika shughuli za kijamii.
“Tunafurahi sana kwa kutembelewa na sekretarieti hii. Zoezi la usafi na faraja kwa wagonjwa limekuwa la manufaa makubwa kwa jamii yetu,” alisema Dr. Mwayola.
Mrakibu Msaidizi wa Polisi, ASP Richard Mkesi, alieleza furaha yao ya kushiriki katika maadhimisho ya Siku ya Maadili. “Kama jeshi la polisi, tunawajibu wa kuwa na maadili mazuri katika utendaji wetu wa kazi.
Tunashiriki katika maadhimisho haya ili kujifunza na kuhamasisha maadili mema katika jamii,” alisema Mkesi.
Aidha, wanafunzi kutoka Taasisi ya Ufundi ya VETA walishiriki katika maadhimisho haya, akiwemo Elisha Ndimba, ambaye alisema:
“Sisi kama vijana, tumejivunia kushiriki katika maadhimisho haya kwa sababu yanatufundisha kuwa mabalozi wazuri wa maadili na wachapakazi wenye maadili katika jamii.”
Siku ya Maadili na Haki za Binadamu ni muhimu kwa kuhamasisha umma kuhusu umuhimu wa maadili katika utendaji wa kazi na katika maisha ya kila siku, ili kujenga jamii iliyo imara, yenye usawa na haki kwa wote.