LICHA ya kutemeshwa kibarua, aliyekuwa kocha wa Yanga, Miguel Gamondi atabaki kwenye mioyo ya Wananchi kwa kile alichokifanya akiwa na timu hiyo kutokana na rekodi nyingi za nguvu akitoa dozi za kutosha za kuanzia mabao matano katika Ligi Kuu, Kombe la FA na hata michuano ya kimataifa ya CAF.
Waswahili husema mnyonge mnyongeni, lakini haki yake mpeni. Ikiwa zimesalia siku chache kabla ya kuumaliza mwaka huu wa 2024, Yanga iliyokuwa chini ya Gamondi ndio timu ambayo imeongoza kwa kutoa dozi ya mabao kuanzia matano huku zikifuata Azam FC na JKT Tanzania katika ligi na Kombe la FA.
Ndani ya mwaka huu wa 2024 ambamo kuna sehemu ya mechi za msimu uliopita wa 2023/24 na za msimu huu 2024/25, Yanga imetoa dozi ya kuanzia mabao matano katika michezo mitatu sawa na asilimia 30 ya vipigo vikubwa kushuhudiwa katika mashindano hayo ya ndani, huku asilimia 20 ilikuwa katika Kombe la FA.
Katika orodha hiyo, Azam na JKT Tanzania nazo zimetoa dozi hizo kubwa, mmoja mara tatu na mwingine mara mbili huku wengine ikiwa ni mara moja moja tu ambao ni Simba, Ihefu na KMC.
Namna gani ilikuwa? Hivi hapa vipigo vyote 11 vya mabao kuanzia matano na kuendelea huku kwa msimu huu kuna michezo miwili tu katika orodha hiyo ambapo yamefungwa mabao kuanzia matano na yote ni upande wa Kombe la FA, katika ligi bado haijashuhudiwa mvua ya mabao ikinyesha.
Ilikuwa Januari 30, Yanga ikiwa mwenyeji wa mchezo huo kwenye Uwanja wa Azam Complex Chamazi iliikaribisha Hausung katika mechi ya Kombe la FA wakati huo likiitwa Kombe la Azam Sports Federation Cup. Ndipo mashabiki waliposhuhudia mvua ya mabao ikinyesha kwa mara ya kwanza ndani ya mwaka huu.
Mabao ya Yanga yalifungwa na Jonas Mkude (dk20), Skudu Makudubela (dk25) na Clement Mzize akimaliza na hat-trick. Bao la Hausung lilifungwa na Tonny Jailos dakika ya 70.
Kipigo hicho cha kuanzia mabao matano hakikuwa cha kwanza chini ya Gamondi. Ndani ya msimu wa 2023/24 kabla ya mwaka kugeuka, Yanga ilitoka kuwaadabisha KMC 5-0, JKT 5-0 na watani wao Simba SC 5-1.
Ni kama Yanga ilifanya kamchezo flani kwani baada ya kuwatandika Hausung ya First League mwishoni mwa Januari, iliendeleza ubabe wake kwa kuwafunga Polisi Tanzania mvua ya mabao mengine matano.
Ilikuwa Februari 20, nyota wa kimataifa wa Ivory Coast aliyesajiliwa dirisha dogo la usajili msimu uliopita, Joseph Guede ambaye kwa sasa yupo Singida Black Stars alifungia Yanga mabao mawili ikiichapa Polisi Tanzania mabao 5-0, kwenye Uwanja wa Azam Complex.
Mchezo huo wa ASFC, ulishuhudiwa Yanga ikiendeleza moto wake wa kuzichapa timu zinazokutana nazo mabao matano, ukiwa ni ushindi wa pili wa idadi hiyo ya mabao kwenye michuano hiyo baada ya awali kuifunga Hausung 5-1 kwenye mchezo wa hatua ya pili.
Guede alifunga mara mbili mabao yake ya kwanza ndani ya timu hiyo katika dakika za 13 na 45+1 yote akiyafunga kwa kichwa akitumia krosi za winga Augustine Okrah.
Winga Farid Mussa aliipa Yanga bao la pili dk32 akitumia krosi ya kiungo mshambuliaji Stephanie Aziz KI na kuifanya timu yao kwenda mapumziko ikiwa na uongozi wa mabao hayo 3-0.
Kipindi cha pili Yanga ilipata bao la nne kupitia mshambuliaji wake Clement Mzize akimalizia krosi ya beki wake wa kulia Kibwana Shomari dk82 kabla ya kiungo mshambuliaji, Shekhan Khamis kumalizia msumari wa tano kwa penalti baada ya Mzize kuangushwa.
Katika mchezo huo, Yanga ilipumzisha baadhi ya wachezaji wake wa kikosi cha kwanza kama vile, Djigui Diarra (kipa), Dickson Job, Nickson Kibabage, Mudathir Yahya, Kennedy Musonda khalid Aucho na Pacome Zouzoua.
Februari 22, matajiri wa Chamazi, Azam FC nao waliamua kujibu mapigo kwa kutinga hatua ya 16 bora wa Kombe la ASFC kwa kishindo baada ya kuitandika Green Warriors mabao 5-0.
Mabao ya Azam FC kataika mchezo huo, yalifungwa na mawinga, Iddi Suleiman ‘Nado’ dakika ya 32, Muivory Coast Kipre Junior ambaye kwa sasa yupo MC Algers dakika ya 23, beki Paul Kyabo aliyejifunga dakika ya 56 na viungo washambuliaji, Abdul Suleiman ‘Sopu’ dakika ya 65 na Ayoub Lyanga yupo Singida BS (dk 83).
Maafande wa JKT Tanzania waliwapigisha kwata TMA na kuonyesha kuwa nao wanaweza kutoa dozi ya mabao matano matano kama walivyofanya Yanga na Azam kwenye Kombe la Shirikisho.
Mara baada ya mchezo huo ambao walitinga hatua ya 16 bora, nyota wao, Shiza Ramadhan Kichuya, alisema siri ya matokeo hayo ilitokana na njaa ambayo walikuwa nayo ya kusaka matokeo ya ushindi.
“Tulihitaji kufanya vizuri hivyo tulijitahidi kila nafasi ambayo tulikuwa tukiipata kuitumia,” alisema.
Februari ilikuwa mwezi ya kushuhudia mabao mengi yakifungwa. Wekundu wa Msimbazi walifanya kweli kwa kuweka rekodi ya kufunga mabao mengi zaidi ya Yanga, Azam na JKT kwa mwaka huu kwa kuwafyatua wakusanya kodi wa Kilimanjaro mvua ya mabao 6-0.
Ilikuwa Februari 28 ambapo Simba ilitinga kibabe hatua ya 16 bora ya michuano ya ASFC baada ya kuibuka na ushindi mnono wa mabao 6-0, dhidi ya TRA ya Kilimanjaro katika mchezo uliopigwa kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamanzi.
Katika mchezo huo wa hatua ya 32 bora, shujaa wa Simba alikuwa kiungo, Sadio Kanoute ambaye kwa sasa yupo zake JS Kabylie, aliyefunga mabao matatu ‘hat-trick’ huku mengine yakifungwa na Ladaki Chasambi, Pa Omar Jobe na Freddy Michael waliofunga moja kila mmoja wao.
Machi 11, hiki ndio kilikuwa kipigo cha mwisho kikubwa kwa Yanga katika mashindano ya ndani kwa mwaka huu.
Mabao ya Yanga yalifungwa na Pacome Zouzoua, Mudathir Yahya, Stephane Aziz KI, Augustine Okrah na Max Nzengeli.
Akiongelea tano tano ambazo Yanga ilikuwa ikifunga, nyota wa zamani wa kikosi hicho, Nadir Haroub Cannavaro anasema; “Ubora wa Yanga ulikuwa mkubwa sana na hapakuwa na shaka juu ya kiwango kilichokuwa kikionyeshwa, bado wana kikosi kizuri na naamini wana uwezo wa kuendelea kufanya vizuri pamoja na changamoto wanazopitia kwa sasa.”
Mei 28, ilishuhudiwa Ihefu ikiitandika mabao 5-1 Mtibwa Sugar iliyokuwa ‘imejifia’ kabla ya kushuka daraja.
Ismail Mgunda ambaye kwa sasa anaichezea Mashujaa, alifunga mabao matatu kwenye mchezo huo huku mengine yakifungwa na Bola Lobota na Morice Chukwu.
Mara baada ya mchezo huo, Mgunda alionyesha furaha yake kwa kusema; “Haikuwa rahisi lakini nitoe shukrani zangu kwa wachezaji wenzangu maana wamekuwa msaada mkubwa kwangu katika kufanikisha hili.”
Kabla ya msimu uliopita kumalizika, Azam FC iliifunga Kagera Sugar mabao 5-1 kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi,
Mabao ya Azam FC yalifungwa na viungo Mgambia, Gibril Sillah dk50, Kipre Junior dk65, na wazawa Feisal Salum dk72 na 79 Iddi Suleiman ‘Nado’ dk90.
Agosti mwaka huu, Mcolombia, Jhonier Blanco alianza kufungua ukurasa wa mabao ndani ya kikosi hicho baada ya kufunga bao moja katika ushindi wa timu hiyo wa 5-2, dhidi ya Coastal Union.
Nyota huyo aliyesajiliwa na matajiri wa Dar es Salaam akitokea Aguilas Doradas, alifungia bao timu hiyo dk45, katika mchezo wa nusu fainali ya Ngao ya Jamii iliyopigwa kwenye Uwanja wa New Amaan Complex visiwani Zanzibar.
Mabao mengine ya Azam FC katika mchezo huo yalifungwa na Gibril Sillah dk13, Feisal Salum ‘Fei Toto’ dk39 na nyota wapya wa kikosi hicho Adam Adam aliyetokea Mashujaa akipachika la nne dk87 na Ever Meza akiweka msumari wa mwisho dk90.
Mabao ya kufuatia machozi kwa Coastal Union, yalifungwa na kiungo nyota wa kikosi hicho, Semfuko Charles dakika ya 26 na Abdallah Hassan dakika ya 86.
Desemba 6, JKT Tanzania ndio ilikuwa timu ya kwanza msimu huu kufunga mabao kuanzia matano katika Kombe la Shirikisho na kutinga hatua ya 32 bora mbele ya Igunga United kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Mstaafu Isamuhyo, Mbweni, Dar es Salaam
Mabao ya JKT Tanzania yalifungwa na Wilson Nangu dakika ya 12, Nahodha John Bocco dakika ya 14, Mohamed Bakari mawili dakika ya 16 na 30 na Danny Lyanga dakika ya 68, wakati bao pekee la Igunga United limefungwa Joel Loya dk58.
Desemba 7, KMC ilitinga hatua ya 32 bora ya Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), baada ya ushindi wa mabao 5-0 dhidi ya Black Six kwenye uwanja wake wa nyumbani wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, KMC Complex, Mwenge, Dar es Salaam.
Mabao ya KMC yalifungwa na Daruesh Saliboko mawili, dakika ya tatu na la penalti dk17, Hance Masoud dk13, Rashid Chambo dk47 na Ally Shaaban dk79.