UNAWEZA kuhisi kama ni utani lakini ndiyo uhalisia, kiungo Kelvin Nashoni na beki Israel Mwenda wanajiunga rasmi na Yanga wakitokea Singida Black Stars ikitajwa ni uhamisho wa mkopo.
Hawa wote wawili wameonekana kuwa na wakati mgumu wa kupata nafasi ya kucheza Singida Black Stars kutokana na uwepo wa nyota wa kigeni wanaofanya vizuri katika nafasi wanazocheza.
Maeneo yote mawili ambayo wanacheza, Yanga ilihitaji watu katika dirisha dogo la usajili ambalo linafunguliwa hivi karibuni na walihitaji kiungo mkabaji awe mbadala wa Khalid Aucho na beki wa pembeni ambaye anaweza kuwasaidia kina Chadrack Boka, Yao Attohoula, Nickson Kibabage na Kibwana Shomari.
Hata hivyo, kuna maswali tunayojiuliza hapa kijiweni juu ya usajili huo na tunahisi muda utatusaidia kutupatia majibu yake hivyo acha tu tuvute subira.
Tunajiuliza kama Nashoni na Mwenda wanaweza kuwa mibadala sahihi ya wachezaji wanaocheza nafasi zao kama ambavyo Yanga inategemea maana huko wanakotoka walikuwa hawapati nafasi na waliopo Yanga pale wako vizuri.
Mtihani mwingine kwa Nashoni na Mwenda ni kuweza kukabiliana na presha iliyopo Yanga kwa sasa kwani timu hiyo sasa ina malengo makubwa na muda wote mashabiki wanahitaji kuona ikipata matokeo mazuri na kinyume na hapo, wachezaji hujikuta kwenye wakati mgumu.
Singida Black Stars haina presha kama hizo na ndiyo maana unaweza kuona vijana hao wawili hawakuwa wakipata nafasi ya kucheza lakini hakukuwa na kelele zozote za mashabiki au vyombo vya habari tofauti na itakavyokuwa Yanga.
Ukiondoa hayo, suala la ugeni Yanga kwa Mwenda na Nashoni sidhani kama linaweza kuwa tatizo kwani kuna namba kubwa ya wachezaji ambao wamewahi kucheza nao hapo nyuma.
Kuna waliocheza nao wakati huo wakichezea timu ya taifa ya vijana ya Tanzania chini ya umri wa miaka 17 ‘Serengeti Boys’ na chini ya miaka 20 ‘Ngorongoro Heroes’, na kuna ambao wamewahi kucheza nao katika klabu tofauti.