Baleke anahesabu siku tu Namungo

BAADA ya kutupia bao moja akiwa na Yanga, mshambuliaji Jean Baleke inaelezwa kwa sasa anajiandaa kuondoka, huku akitajwa huenda akaibukia Namungo inayonolewa na Juma Mgunda.

Nyota huyo wa zamani wa Simba, alirejea nchini mwanzoni mwa msimu huu akitokea Libya alikokuwa kaicheza kwa mkopo kutoka klabu yake ya TP Mazembe, lakini amekuwa hana namba katika kikosi cha kwanza kuanzia kwa kocha Miguel Gamondi hadi Sead Ramovic anayeinoa timu hiyo kwa sasa.

Taarifa za ndani ya Yanga zinasema kuwa straika huyo yupo mbioni kupigwa chini katika dirisha dogo la usajili linalofunguliwa kesho, huku Namungo ikitajwa kutaka huduma yake.

Chanzo cha habari kutoka Namungo kinasema klabu hiyo kupitia Mgunda imependekeza imchukue Baleke kwani kocha huyo wa zamani wa Simba anajua makali ya mshambuliaji huyo Mkongomani.

“Mwenendo mbaya kwenye safu ya ushambuliaji ndio sababu ya kufanya usajili wa mchezaji mwingine eneo hilo kutokana na mapendekezo ya kocha na tuna imani kubwa na Baleke ataweza kutusaidia kutokana na mchezaji huyo kuwa na jicho la kuona goli,” alisema mtoa taarifa huyo aliyeomba hifadhi ya jina lake.

Related Posts