Bwalya ajiandaa kurudi Bongo | Mwanaspoti

PAMBA Jiji ipo kwenye hatua za mwisho za kumalizana na kiungo wa zamani wa Simba, Mzambia Rally Bwalya akitokea Napsa Stars FC ya Zambia.

Timu hiyo yenye maskani yake jijini Mwanza katika michezo 12 ya Ligi Kuu imeonja ushindi mara mbili, sare sita na kupoteza sita, ikiwa nafasi ya 12 ikivuna pointi 12 na kwa siku za karibuni imekuwa ikihusishwa kujiimarisha kwa kusaka nyota wapya watakaoipiga tafu ndfni ya duru la lala salama.

Ikiwa zimesalia siku mbili kabla ya dirisha dogo la usajili kufunguliwa Desemba 15 mwaka huu inaelezwa viongozi wa Pamba wameamua kuingia sokoni na kumuongeza kiungo huyo Mzambia baada ya kumkosa Najim Mussa inayesemekana yuko mbioni kujiunga na Namungo kwa mkopo akitokea Singida Black Stars ambako hakuwa akipata nafasi ya kucheza mbele ya Emmanuel Keyekeh, Josaphat Bada na Mohamed Damaro.

“Baadhi ya viongozi wamesafiri kwenda Zambia kukamilisha dili la mchezaji huyo na kwa asilimia kubwa dili hilo linaweza kukamilika kutokana na baadhi ya vitu tayari vimemalizwa bado vichache sana,” kilisema chanzo kutoka ndani ya klabu hiyo.

Hata hivyo, Mwanaspoti lilipomtafuta Ofisa Habari wa klabu hiyo, Moses William ili kujua dili hilo limefikia hatua gani, lakini alisema; “Bado dili hilo haliko rasmi, likiwepo tutatawatangazia umma juu ya usajili wote wa klabu yetu. Dirisha bado halijafunguliwa, lakini tutakiboresha kikosi chetu.”

Mbali na Bwalya, pia Pamba inadaiwa imeshamalizana na nyota wengine wazoefu wa ligi hiyo akiwamo beki wa kati wa zamani wa Simba na Yanga, Kelvin Yondani, winga Deusi Kaseke aliyewahi kutamba na Mbeya City, Yanga, Singida United na Singida Fountain Gate.

Related Posts