Chadema Mbeya yatoa masharti kushiriki Uchaguzi Mkuu 2025

Mbeya. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Mkoa wa Mbeya kimesema hakitashiriki uchaguzi mkuu iwapo hakutakuwa na Tume huru ya uchaguzi kutokana na hujuma walizofanyiwa kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa.

Katika uchaguzi uliofanyika Novemba 27, 2024, Chadema haikushinda mtaa wowote jijini Mbeya kati ya mitaa 181 iliyopo huku kwenye vijiji kikiambilia viti 13 kati ya 533.

Akizungumza leo Desemba 13, 2024, mwenyekiti wa chama hicho Mkoa wa Mbeya, Masaga Kaloli amesema kufuatia hujuma hizo, wameazimia kutoshiriki uchaguzi mkuu wa 2025 iwapo hakutakuwa na Tume huru.

Amesema kama haitoshi, wameazimia kutotoa ushirikiano kwa wenyeviti ambao wametangazwa bila kushinda, akieleza kuwa hatua hiyo itasaidia kuwaondoa kwenye nafasi hizo.

“Tumefanyiwa hujuma sana, yapo baadhi ya maeneo ikiwamo Kyela, Rungwe na Mbeya Mjini ambapo ndio ngome ya Chadema lakini tuliambulia rafu tu, yote hii ni kutokana na kutokuwa na Tume huru badala yake CCM wanajitangaza wenyewe.

“Mwakani kwenye uchaguzi mkuu, msimamo na maazimio yetu ni kutoshiriki mchakato huo kama hakutakuwapo Tume huru, Tamisemi haina kazi katika hili,” amesema Kaloli.

Kiongozi huyo amewaomba wananchi na viongozi wengine wakiwamo wa dini kuhakikisha wanashirikiana na Chadema katika kupinga uchaguzi usio huru na haki.

Katibu wa chama hicho mkoani hapa, Hamad Mbeyale amesema namna bora ya kuondokana na hujuma katika uchaguzi ni kuwa na Katiba mpya, akieleza kuwa Chadema haitasita kudai haki hiyo.

“Matarajio yetu ilikuwa ni kupata ushindi wa zaidi ya asilimia 75 kwa maeneo yote tuliyosimamisha wagombea, lakini kwa kuwa hawana uwezo wa kushindana, wakaamua kutumia nguvu kujitangaza,” amesema Mbeyale.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la Vijana wa Chama hicho (Bavicha), Elisha Chonya amesema vijana walinyang’anywa na kunyimwa haki yao ya kuongoza na jamii kutopata haki yao.

Amesema kwa sasa inahitaji mifumo mizuri ya demokrasia ili kuweka usawa kuliko kuendelea na uchaguzi ambao unaonekana kutokuwa huru na haki.

“Tunahitaji mfumo mzuri wa kidemokrasia, tukipata katiba mpya itaweza kumaliza changamoto kama hizi, vijana wananyimwa haki zao na jamii kutopata viongozi wanaowataka,” amesema Chonya.

Related Posts