Hilo ndilo chimbuko la Sinza kwa wajanja

Dar es Salaam. Sinza ni miongoni mwa maeneo maarufu na yenye pilikapilika nyingi katika Jiji la Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa Ripoti ya Sensa ya Watu na Makazi 2022, eneo hilo lina wakazi takribani 31,396, huku wanaume wakiwa 14,759 na wanawake wakiwa 16,637.

Kwa mujibu wa mkazi wa eneo hilo kwa takribani miaka 30, Mwajuma Shabani, Sinza halikuwa eneo lililochangamka na pilikapilika za hapa na pale kama ilivyo sasa.

Anasema awali eneo hilo lilikuwa pori na mashamba ambayo watu walikuwa wakilima mazao mbalimbali.

“Mfano mimi katika eneo nililojenga nyumba yangu pale Sinza Mori awali lilikuwa shamba la mpunga na nililinunua kwa Sh2,500 ya miaka hiyo na ndiyo nikajenga nyumba yangu ambayo ninaishi na familia yangu,” anasema.

Hata hivyo, anasema kadiri miaka ilivyozidi kwenda kutokana na kuendelea kukua kwa mji, watu walinunua kwa kasi maeneo na kufanya ujenzi wa nyumba za kisasa, hoteli na sehemu za starehe.

Anasema kutokana na kukua na kuwa na ongezeko la makazi ya kisasa pamoja na sehemu za starehe, ikiwemo baa, hoteli pamoja na migahawa, eneo hilo lilianza kuonekana ni eneo la watu wenye kipato cha kati na juu, baadaye kukaanza kuitwa ‘Sinza kwa wajanja’.

Hata hivyo, Yusuph Yusuph, ambaye ni mzawa wa eneo la Sinza Mori, anasema kwa upande wake anafahamu eneo hilo kuitwa ‘Sinza kwa wajanja’ kutokana na uwepo wa sehemu nyingi za starehe, hasa kipindi cha miaka ya 2000.

“Hiyo ilifanya kila mtu anayetaka kuburudisha nafsi yake kufikiria Sinza kama chaguo la kwanza, hivyo hata wasanii wengi walikuwa wakitoa burudani katika kumbi za starehe zilizopo katika maeneo hayo,” anasema.

Anaeleza kuwa kutokana na kuchangamka kwa eneo hilo na kuonekana kama ni la watu wenye kipato cha kati na juu kwa wakati huo, baadhi ya watu walianza kuliita eneo hilo kama ‘Sinza kwa wajanja’.

Akizungumza na Mwananchi, mdau wa masuala ya burudani na mzawa wa Sinza, Issa Levy anasema aliyekuza jina hilo hadi kila mahali wanalifahamu ni marehemu Ramadhani Masanja, maarufu kama Banza Stone.

Huyu alikuwa mkongwe wa muziki wa dansi aliyewahi kutamba na nyimbo kadhaa, ikiwemo Mtaji wa maskini, Elimu ya mjinga, Angurumapo simba acheza nani, Falsafa ya maisha na nyinginezo.

Dk Levy anasema, Banza Stone alitumia ‘Sinza kwa wajanja’ kama kibwagizo katika baadhi ya nyimbo zake na kufanya jina hilo kuenea, kukua na kujulikana zaidi hata na watu waliokuwa wakiishi nje ya Dar es Salaam.

Mojawapo ya nyimbo ambazo alitumia neno la ‘Sinza kwa wajanja’ kama moja ya kibwagizo chake ni pamoja na Jirani alioimba akiwa The African Stars ,Twanga Pepeta.

Moja ya mashairi katika wimbo huo alitaja baadhi ya mikoa, ikiwemo Dodoma, Shinyanga, Singida, Arusha, Bukoba na kumalizia Sinza kwa wajanja.

Sinza ina simulizi ya mahali walipoishi watu maarufu. Ukimuondoa Banza Stone na Remmy Ongala (wote sasa marehemu), Sinza ina watu maarufu kama vile wasanii wa filamu, Vicent Kigosi (Ray) na Jacob Stephen, maarufu kama JB.

Kwa sasa Sinza kama kata, ina vitongoji kadhaa maarufu, baadhi vikiwa Sinza kwa Remmy, Mori, Sinza Mapambano, Makaburini, Madukani, Kijiweni, Mugabe, Lion, Vatican, White-Inn pamoja na Darajani.

Sinza kwa Remy ni jina lililotokana na kuwapo makazi ya Remmy Ongala, mwanamuziki maarufu kutoka DRC aliyelowea Tanzania na kuasisi iliyokuwa bendi maarufu ya dansi ya Super Matimila.

Moja ya sifa kubwa za Sinza ilikuwa ni kusheheni maeneo ya burudani, lakini pia kwa sasa Sinza imechukua taswira mpya ya ujenzi wa maghorofa na maduka ya bidhaa mbalimbali.

Related Posts