Katika maisha ni kawaida kukutana na mtu ambaye pengine mwenza wake alifariki na VVU. Na huenda na yeye ameathirika, lakini akaanzisha mahusiano na mwenza mpya asiye na maambukizi.
Ikiwa unampenda mwenza huyo ni kawaida kujiuliza maswali mengi. Je, utaishije naye. Je, nimeambukizwa au niko katika hatari ya kuambukizwa? Je, tunaweza kukaa pamoja na kujamiiana bila kuambukizwa?
Hayo ni baadhi ya maswali ambayo ni kawaida kwa mwenza kujiuliza ambaye anampenda mwenza mwenye VVU na anahitaji kuishi naye. Shirika la Afya Duniani WHO, linapendekeza wanandoa wapimwe VVU na washauriwe pamoja. Lakini linawahusu pia wale wanaohitaji kuingia katika mahusiano ya kimapenzi.
Kupokea upimaji wa hiari wa VVU na ushauri nasaha kama wanandoa au wenza ina maana kwamba wapenzi wote wawili wapimwe pamoja, kupokea majibu yao, kujua hali zao na kupata msaada wa mshauri.
VVU inaenea zaidi kwa njia ya kujamiiana bila kinga. Unaweza pia kuambukizwa kama unashiriki pamoja vitu vyenye ncha kali, ikiwamo sindano na viwembe na mtu aliyeambukizwa.
Kuna uwezekano mdogo sana kupata VVU kwa kujamiiana kwa njia ya mdomo, ikiwamo kwa kumbusu. Na huwezi kupata kwa kugusana na mate, machozi au jasho.
Hatari ya maambukizi iko chini sana katika kujamiiana bila kinga na mtu mwenye VVU ambaye anatumia dawa za kufubaza makali ya VVU. Hii ni kutokana na ufanisi wake kuzuia maambukizi mpaka asilimia 99. Wakati mwenzi mmoja ameambukizwa VVU na mwingine hana lakini wanaishi pamoja hujulikana kama discordant couple, wanajulikana pia kama wenza wenye hali mchanganyiko.
Nchi za Tanzania, Kenya, Uganda, Zambia na Afrika Kusini zina wenza wa aina hii ambao wanaishi kwa zaidi ya miaka 20 pasipo mwenye VVU kumwambukiza mwenzake.
Kuishi na mwenza mwenye VVU pasipo kupata VVU kumefanikiwa kutokana na mwenza mwenye VVU kushikamana na dawa za kufubaza makali na huku akijamiiana kwa njia salama.
Msaada mkubwa kufikia lengo hili unatoka kwa madaktari pamoja na washauri nasaha wa VVU ambao wana mafunzo na huku wakizingatia miongozo ya nchi iliyo chini ya WHO. Njia salama na yenye hatari ndogo ni kujamiiana kwa njia ya uke. Hii ni kutokana na ukweli kuwa kujamiiana kinyume na maumbile kuna hatari mara 10 zaidi kupata VVU. Ni hatari zaidi wakati mwenza asiye na VVU ndiye anayepokea.
Daktari anaweza kuandikia dawa ya kurefusha maisha ili kukusaidia usipate VVU pale inapotokea umejamiiana kiholela katika hatari kubwa ya kupata maambukizi, tiba hii hujulikana kinga tiba (PEP), baada ya kuingia katika hatari ya maambukizi.
Ili PEP ifanye kazi, lazima kutumia kama ilivyoagizwa. Inaweza kupunguza hatari ya kueneza virusi kwa njia ya kujamiiana kwa asilimia 99.
Hakikisha mwenza wako anakunywa dawa, matibabu ya VVU yanaweza kumfanya awe na afya njema. Hiyo ni kwa sababu dawa za kurefusha maisha zinaweza kushusha virusi hadi viwango ambavyo haviwezi kupimwa, kitabibu huitwa kiwango cha virusi kisichoweza kutambulika.
Ikiwa mpenzi wako anatumia dawa zake na ana kiwango cha virusi kisichoweza kutambulika, basi virusi haviwezi kuambukizwa kwa kujamiiana.
Hivyo basi, kuishi na mwenza mwenye VVU unayempenda ni jambo linalowezekana na ni salama. Fika katika huduma za afya kwa ushauri na ufahamu zaidi.