KLABU ya Kagera Sugar iko katika hatua za mwisho za kukamilisha uhamisho wa winga wa Singida Black Stars, Edmund John kwa mkopo wa miezi sita, baada ya nyota huyo kupitia changamoto ya kukosa nafasi ya kucheza ndani ya kikosi cha kwanza.
Nyota huyo aliyejiunga na Singida msimu huu akitokea Geita Gold iliyoshuka daraja, msimu huu pekee akiwa na kikosi hicho amecheza michezo miwili tu kati ya 12 iliyocheza timu hiyo, kabla ya ule wa jana dhidi ya ‘Walima Zabibu’, Dodoma Jiji.
Ofisa Habari na Mawasiliano wa Singida Black Stars, Hussein Massanza alisema taarifa rasmi juu ya wachezaji wote ambao wataachana nao au kuwatoa kwa mkopo kwenda sehemu nyingine wataziweka wazi, japo kwa sasa bado hawezi kuzungumzia hilo.
Wakati wa usajili huwa mambo mengi yanazungumzwa na huu ndio wakati wake na huwezi kuzungumzia kila kitu kinachoendelea mitandaoni, muda ukifika tutaweka wazi ila mashabiki zetu watambue tuna watu makini wanaofanya kazi vizuri kwenye bodi.”
Kwa upande wa Edmund akizungumza na Mwanaspoti alisema, kila kitu kitakuwa wazi muda ukifika ingawa kwa sasa ni mapema kuzungumzia hilo kwani bado hajapokea taarifa rasmi kutoka kwa viongozi, hivyo anaendelea kusubiri kujua hatima yake.
“Kama ni kweli nitatolea kwa mkopo sawa ila sijapokea taarifa yoyote kuhusu hilo, nia yangu ni kupata nafasi ya kucheza zaidi na kuonekana, ingawa haina maana kama nitaondoka nitakuwa nimekimbia ushindani uliopo hapa kikosini,” alisema.
Mwanaspoti linatambua, Kocha wa Kagera, Mmarekani Melis Medo ni shabiki mkubwa wa nyota huyo ambaye tangu msimu uliopita alifunga bao moja tu wakati akiwa Geita Gold katika ushindi wa timu hiyo wa 1-0, dhidi ya JKT Tanzania Novemba 22, 2023.