Dodoma. Wadau wa mazingira nchini wametaja changamoto tano zinazowakabili washauri elekezi wa mazingira, ikiwemo upungufu wa kikanuni ambao umefanya kampuni 65 zilizosajiliwa na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) mwaka 2021 kushindwa kufanya kazi.
Kampuni hizo zimeshindwa kufanya kazi kutokana na upungufu uliopo kwenye Kanuni za usajili na utendaji kazi wa washauri Elekezi wa mazingira za mwaka 2021.
Changamoto nyingine ni uelewa mdogo wa wadau kuhusu mwongozo wa kufanya tathmini ya athari kwenye Mazingira (TAM), miradi na viwanda vingi kutoajiri wataalamu wa mazingira, namba ya mlipakodi (TIN) na ucheleweshaji wa hati za ardhi.
Hayo yamebainishwa leo Desemba 13, 2024, na Mwenyekiti wa Chama cha Washauri Elekezi wa Mazingira Tanzania (TEEA), Emmanuel Hanai, wakati wa mkutano mkuu wa sita wa chama hicho kinachoshirikisha wataalamu wa mazingira nchini.
“Mwaka 2021, NEMC ilisajili kampuni 65 za kufanya TAM lakini baada ya utekelezaji wa kanuni hii mpaka sasa hakuna kampuni inayoweza kuendelea kufanya kazi kwa takwa la kanuni hii,” amesema.
Amesema tayari TEEA, NEMC, na kampuni hizo wameanza majadiliano ya namna bora ya kuhakikisha wanaendelea kutoa huduma kwa jamii bila kuathiri wawekezaji, uwekezaji na utendaji kwa ujumla.
Amesema changamoto nyingine ambayo wameshawasilisha katika kanuni hiyo ni kuhusu kuondolewa kwa washauri elekezi ambao pia ni watumishi wa umma kufanya shughuli za TAM.
“Hiyo imeathiri taasisi kama za elimu ya juu ambapo shughuli hizo za ushauri elekezi ni moja ya majukumu yao ya kawaida na kwa mujibu wa University Charter,” amesema.
Ameitaja changamoto nyingine kuwa ni uelewa mdogo wa wadau mbalimbali kuhusu mwongozo huo ambapo baadhi ya taasisi za serikali na wadau mbalimbali bado wanatekeleza miradi bila kufanya tathmini ya athari ya mazingira.
“Sisi washauri elekezi katika utendaji wetu tunashuhudia uwepo wa miradi mingi isiyokuwa na vyeti vya TAM au kaguzi ikiendeshwa, lakini pia hata baadhi ya iliyo na TAM na kaguzi bado haitekelezi maelekezo ya usimamizi, kama ilivyotolewa kwenye ripoti za TAM na vyeti vyenyewe,” amesema.
Amesema hali hiyo imesababisha uharibifu wa mazingira, ikiwa ni pamoja na utupaji taka ovyo.
Kuhusu changamoto ya baadhi ya viwanda na miradi kutoajiri wataalamu wa mazingira, Hanai amesema changamoto hiyo huifanya tasnia ya mazingira, ambayo inatambulika katika maendeleo endelevu ya uchumi wa dunia, kuwa hatarini na kusababisha ongezeko la athari za kimazingira ikiwemo ukame, mafuriko, joto kali, na baridi kali.
Kwa upande wa changamoto ya namba ya mlipakodi (TIN), Hanai amesema washauri elekezi wanaombwa leseni na namba za TIN za biashara kama takwa la kupatiwa leseni ya utendaji kazi, jambo linalofanya maombi mengi kutofanikiwa.
Amesema hiyo ni kwa sababu mamlaka zinazotoa leseni na TIN za biashara huomba leseni za utendaji kazi ili kujiridhisha kama mwombaji wa leseni ana sifa stahiki za kupewa leseni na TIN kwa ajili ya kufanya shughuli za ushauri elekezi.
“TEEA tuliomba kufanyike marekebisho ya kanuni za usimamizi wa mazingira za mwaka 2021 kuhusu suala hili,” amesema.
Kuhusu changamoto ya ucheleweshaji wa hati, Hanai amesema hati zimekuwa zikichelewesha ukamilishaji wa TAM kwenye miradi mingi na kusababisha baadhi ya wawekezaji kughairi na kufanya kitu kingine.
Amesema hiyo inatokana na wawekezaji waliokopa wanatakiwa kuanza kurudisha mikopo na kuomba mamlaka zimpe mkurugenzi wa halmashauri mamlaka ya kuithibitishia NEMC kwamba eneo limepangwa kwa matumizi husika.
Amesema nyaraka hutoka kwa mkurugenzi lakini zinapewa uhalali na kamishna na msajili wa hati.
Akijibu hilo, Naibu Katibu Mkuu katika Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Christina Mndeme amesema amezisikia changamoto zao na kuwa Ofisi ya Makamu wa Rais itaendelea kuzifanyia kazi changamoto hizo ili kuboresha utendaji wao wa kazi.
“Ninawaahidi utendaji wenu wa kazi utakuwa wa rahisi zaidi ya jana. Kuhusu changamoto za kikanuni, natoa wito kwa TEEA na NEMC kushirikiana ili kufanya mapitio ya kanuni hizo ili kubaini maeneo yanayoleta changamoto katika utendaji wa washauri elekezi,” amesema.