KONGAMANO LA KUMALIZA MWAKA LA KKKT MIRERANI LAFANA

Na Mwandishi wetu, Mirerani

KONGAMANO la kumaliza mwaka la Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Mirerani Jimbo la Arusha Mashariki Dayosisi ya Kaskazini Kati, mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, limefana kwa waumini kupata chakula cha roho na kwaya mbalimbali kuhudumu.

Mchungaji kiongozi wa usharika wa Mirerani, Loishiye Godson Laizer akizungumzia kongamano hilo amesema watu wanapaswa kumshukuru Mungu kwa kuwapa uzima kwa mwaka mzima.

Mchungaji Laizer amesema ni vyema wakristo kutumia makongamano kama hayo kwa ajili ya kumshukuru Mungu kwa kumaliza salama mwaka 2024 na kuupokea mwaka mpya wa 2025.

“Kongamano limefanyika kwa muda wa siku nne, baada ya kumaliza mwaka 2024 ni vyema kumshukuru Mungu na kujiandaa kuupokea mwaka mpya wa 2025 kwa amani bila kuwepo na vurugu zozote zile,” amesema mchungaji Laizer.

Amesema katika kongamano hilo waumini wameimarishwa kwa kupewa mafundisho sahihi ili kuepuka na hujuma za imani ikiwemo udanganyifu wa visaidizi vya imani.

“Kuna baadhi ya watu kulingana na ulimwengu ulivyo hivi sasa wanadanganywa kwa kuuziwa visaidizi hivyo ikiwemo maji, chumvi na mafuta,’ amesema mchungaji Laizer.

Mratibu wa mipango na fedha, usharika wa Mirerani, Tumaini Daniel ameeleza kwamba wanamshukuru Mungu kwani kongamano hilo limekwisha kwa neema tele na baraka nyingi.

“Tunamshukuru Mungu tumepata kongamano hili kwani changamoto kwa watu kutangatanga itapatikana na kufahamu namna ya kumtumikia Mungu na namna ya kuishi katika Imani bila kuyumbishwa na imani tofauti,” amesema.

Mwinjilisti wa mtaa wa Mirerani, HappyGod Serafin Mtui amesema kongamano hilo lilikuwa zuri na limewasaidia watu kiroho kumaliza mwaka 2024 vyema na kusubiri kupokea mwaka mpya wa 2025.

“Tunamshukuru Mungu kwani mchungaji kiongozi wa usharika amefanikisha huduma hiI na waumini wamefurahi huku wakiomba tuendeleee vyema kupitia chakula cha roho,” amesema.

 

Related Posts