Lissu aibua mapya Chadema, Profesa Safari atia neno

Dar es Salaam. Siku moja baada ya Makamu Mwenyekiti wa Chadema (Bara), Tundu Lissu kutangaza nia ya kugombea uenyekiti  wa chama hicho, mnyukano mkali umeibuka mitandaoni miongoni mwa makada na wanaharakati, huku wachambuzi wakitaka yaliyoibuliwa na kiongozi huyo kufanyiwa kazi.

Kwa upande mwingine, aliyewahi kuwa Makamu Mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Abdallah Saffari amemtaka Lissu kujipanga na vita ya watu, aliowaita chawa watakaofanya kila linalowezekana ili asishinde.

Lissu alitangaza nia yake juzi  jijini Dar es Salaam katika mkutano uliohudhuriwa na baadhi ya viongozi na makada wa chama hicho, akisema: “Kwa msimamo wangu thabiti na usiotetereka, ninazo sifa na uwezo wa kusimamia maboresho ya chama chetu katika kipindi hiki kigumu.’’

Japo Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe bado hajatangaza nia ya kuendelea kugombea nafasi hiyo aliyoiongoza kwa miaka 20 sasa, kujitokeza kwa Lissu kunatajwa kuleta upinzani mkali unaotishia kuibuka kwa mpasuko katika chama hicho.

Hali hiyo imetahadharishwa na mchambuzi wa masuala ya siasa, Bubelwa Kaiza akisema ni wakati wa wanachama na viongozi wa chama hicho kujikita kwenye misingi ya chama.

“Kila mwanachama wa Chadema ajue kwamba Chadema ni taasisi yenye muundo, mfumo, itikadi na uongozi ambavyo vinabebwa na Katiba.

“Waachane na masuala ya kusema wanamwamini mtu. Mtu anaweza kuondoka na chama kikabaki.

Wakikivuruga chama kwa kuwa na ushabiki wa mtu, maana yake ni kwamba na wao watapotea pia,” emesema. 

Ameongeza: “Kuna msemo wa Kiswahili, asiyejua kufa atazame kaburi. Watazame vyama vilivyokuwa na nguvu kama NCCR Mageuzi, TLP, CUF, waangalie sasa viko wapi.”

Wakati hayo yakiendelea, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe anatarajiwa kuongoza kikao cha Kamati Kuu kesho Desemba 14, jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Itifaki, Uhusiano na Mambo ya Nje wa chama hicho, John Mrema, kikao hicho kitajadili na kupitisha majina ya wagombea wa nafasi mbalimbali katika Kanda ya Kaskazini na kufanya maandalizi ya mkutano mkuu.

Mtandaoni hakujatulia. Watu wa aina  mbalimbali wakiwamo makada wa chama hicho wanaonekana kunyukana kwa hoja kuhusu kinachoendelea hivi sasa.

Mmoja wa makada, Boniface Jacob, ambaye ni mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Pwani, muda mfupi baada ya mkutano wa Lissu, aliandika kwenye ukurasa wake wa X ujumbe unaotafsirika kama ni onyo kwa Lissu kutaka kugombea uenyekiti wa chama. Aliandika:

“Ndugu yako akitaka kupigana vita na wewe, mkatalie na umsihi sana asitoe upanga ndani ya ala yake. Asiposikia akataka vita zaidi, muitie ndugu wengine na wazee wa ukoo wamsihi umuhimu wa umoja wa familia.

 “Asipowasikiliza ndugu zake, wazee na majirani, muitie viongozi wa dini na wazee wamsihi madhara ya vita. Akiwakatalia wote hao, mpe anachokitaka (vita). Usimuonee huruma kabisaaaaa. Na iwe funzo kwake na ndugu wengine kuwa umoja na upendo katika familia yenu ni muhimu kuliko tamaa binafsi.”

Kauli nyingine inayoonekana pia  kumtahadharisha Lissu imetolewa na Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Shinyanga, Emmanuel Ntobi aliyeandika: “Ifahamike kuwa wajumbe wa Mkutano Mkuu Chadema Taifa ni zaidi ya 1,200. Ubwabwa wa kushiba huonekana kwenye sahani.

“Tukubaliane, ukipigwa hakuna kuhama chama wala kujiliza! Don’t hate the players, hate the game! (usiwachukie wachezaji, chukia mchezo).”

Hata hivyo, makada wengine wa Chadema hawakuonyesha kuegemea kwenye upande wowote katika maoni yao, akiwamo Martin Maranja Masese ambaye katika ukurasa wake wa X, amekisifia chama chake.

 “Chadema ni chama chenye mvuto katika jamii. Uchaguzi wa mwenyekiti unajadiliwa na kufuatiliwa na makundi rika tofauti katika jamii. Hakika, tunakwenda kuwapa uchaguzi bora wa ushindani. Siyo ….. (anakitaja jina chama fulani), mwenyekiti anagombea na kivuli. Fomu moja kama hati ya kifo,” ameandika.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Kaskazini, Godbless Lema ameandika katika mtandao huo, akitaka watu watofautishe uamuzi wa Lissu na utovu wa nidhamu.

“Kuna tofauti kubwa kati ya minyukano na utovu wa nidhamu. Jambo la msingi ni kuwa wanachama wetu wengi pengine watakuwa wanajua tofauti zake.

“Utovu wa nidhamu unaua umoja na upendo na mahusiano. Tuko katika kipindi cha kawaida sana cha kisiasa ndani ya chama chetu, isipokuwa kwa namna tunavyotazama, kufikiri, kutenda ndio linaweza kuwa tatizo au baraka,” ameandika.

Mbali na makada wa Chadema, wanaharakati kadhaa nao wametia maneno kwa uamuzi huo wa Lissu.

Ujumbe wa kuunga mkono uamuzi wa Lissu umechapishwa pia na Rais wa Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS), Boniface Mwabukusi aliyesema anahitaji wanasheria thabiti wengi zaidi kushiriki katika michakato ya kisiasa ndani ya vyama na nje.

Vijembe pia vilishuhudiwa katika mtandao huo, kikiwemo kile kilichoandikwa na Mbunge wa Ubungo (CCM), Profesa Kitila Mkumbo, “kawashika pazuri. Pale ambapo silaha inamgeukia mwenye silaha! Nimekaa paleee!”

Katika andiko lake lililosambaa mitandaoni, Askofu Emmaus Mwamakula amewataka wanachama wa Chadema kutambua kuwa kugombea nafasi yoyote ndani ya chama chao sio hisani ya baadhi ya watu au makundi na pia sio uhaini dhidi ya watu au kundi lolote.

“Kuwasema na kuwanyanyapaa watu ambao wako upande wa Lissu au Mbowe ni udikiteta na haina tofauti na vitendo vya wasiojulikana, ambao humteka na kumpoteza hata kumuua mtu aliye kinyume na mtu wao,” amesema.

Profesa Safari amng’ata sikio Lissu

Akizungumza na Mwananchi leo Desemba 13, 2024, Profesa Safari aliyewahi kuwa Makamu Mwenyekiti wa Chadema, amesema kwa uzoefu wake wa siasa za Tanzania, mara nyingi ni vigumu kuwashinda wenyeviti waliopo madarakani kwa sababu mbalimbali.

Amejitolea mfano wake alipokuwa kada wa CUF na alipoamua kumkabili mwenyekiti wa chama hicho,  katika uchaguzi wa CUF mwaka 2009, ambapo alipewa kila aina ya majina ikiwemo pandikizi.

“Lazima kuwepo na mabadiliko ya uongozi, kama nilivyowahi kusema kule CUF kwamba usultani na ufalme haufai. Kwa hiyo acha tuone vumbi litimke, tuonane sura zetu vizuri,”

“Nimefurahi sana, naona historia inajirudia kwangu mimi na Sumaye Frederick – (Waziri Mkuu mstaafu). Sioni kitu kibaya kwa Lissu kugombea, hata mimi niligombea nikiwa CUF,” amesema Profesa Safari.

Akieleza uzoefu wa yaliyomkuta akiwa CUF, Profesa Safari amesema:

“Nakumbuka sikuwa na cheo chochote, nilikuwa mshauri wa sheria, lakini nilipoamua kugombea uenyekiti CUF,  ikaanzishwa kampeni kwamba Safari pandikizi…Wakati wa uchaguzi waliwachukua wapiga kura na kuwaweka sehemu moja na kuwaeleza Safari pandikizi.

“Baadhi ya watu wa karibu pia walinigeuka kwa sababu tu nataka uenyekiti ambaye nitanyooka na kudai tume huru, wakanipiga vita. Watu wakaaminishwa kwa kulishwa matango pori, niliambulia kura sita tu,” amesema Profesa Safari.

Kwa mujibu wa Profesa Safari, aliamua kuwania uenyekiti wa CUF, ili kuleta ushindani na kuondoa mwenendo wa viongozi kukaa muda mrefu akifananisha na  kile alichokiita usultani.

 “Waliniita pandikizi, ujinga sana ule, yaani pandikizi ningefukuzwa kazi? Lissu lazima alijue hili. Lissu ana heshima kubwa, watu wanampenda, lakini ajue kuna madhila yaliyomkuta Sumaye (Frederick –waziri mkuu mstaafu),” amesema Profesa Safari.

Katika hotuba yake, Lissu aligusia umuhimu wa mabadiliko ya katiba ya chama hicho, ikiwemo ukomo wa madaraka, mfumo wa fedha na mfumo wa uchaguzi.

Kuhusu ukomo wa madaraka, Lissu ametaka uwepo kwa viongozi wote tangu tangu ngazi ya Taifa hadi ngazi ya msingi.

“Kuweka ukomo wa madaraka katika uongozi wa chama sio tu utaondoa uwezekano wa viongozi wa chama kung’ang’ania madaraka, bali pia utawezesha kujengeka kwa utamaduni wa kuandaa viongozi wapya wa chama,” alisema.

Pia, alisema umuhimu wa marekebisho ya katiba hiyo unatokana na haja ya kuwepo kwa mfumo huru wa kusimamia chaguzi za ndani ya chama hicho.

Katika hatua nyingine, Lissu alieleza umuhimu wa kuwepo utaratibu wa kutafuta, kusimamia na kutumia fedha na rasilimali nyingine za chama na iundwe idara au kitengo kitakachokuwa na jukumu la kutafuta fedha na rasilimali kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli za chama.

“Utaratibu wa kutegemea mtu mmoja kuwa mtafutaji mkuu wa fedha na rasilimali za kuendeshea shughuli za chama,  ni wa hatari na unatengeneza utegemezi usiokuwa na afya au manufaa yoyote kwa chama,” alisema.

Akijadili hoja hizo, mhadhiri wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Dk Revocatus Kabobe amesema kama hoja hizo zitashughulikiwa, zitaondoa malalamiko ya muda mrefu katika chama hicho.

Naye mchambuzi wa masuala ya siasa, Kiama Mwaimu amekubaliana na hoja ya taasisi au chama cha siasa kuwa na mihimili yake ya fedha, badala ya kumtegemea mtu.

“Kuna msemo unaosema anayekufadhili atakufanya punda. Ukimtegemea mtu inasababisha awe na nguvu ya kutengeneza utaratibu wa kufanya kila jambo atakalolitaka,” alisema.

Kuhusu mfumo huru wa uchaguzi, Dk Kabobe amesema kumekuwepo malalamiko hasa unapokuja wakati wa uchaguzi wa ndani wa chama hicho.

“Rejea chaguzi za hivi karibuni kuanzia ngazi ya chini hadi kwenye kanda. Hata Mchungaji Msigwa (Peter) alinukuliwa akilalamika juu ya kupoteza ushindi wa kanda ya Nyasa kuwa ni kukosekana kwa uwazi na haki kwenye uchaguzi,” alisema.

Suala hilo kwa mujibu wa Dk Kabobe limekuwa donda ndugu, jambo linalothibitisha kile alichodai, “Mfumo uliopo wa uchaguzi ndani ya Chadema una matundu ambayo kwa maoni yangu Lissu ndio anataka kuja na tiba yake.”

Kwa mtazamo wa Dk Kabobe, tiba ya mfumo wa uchaguzi ndani ya Chadema ianzie na viongozi wa juu hadi chini ili kutenda haki kwa wote.

Akizungumzia ukomo wa uongozi ndani ya chama hicho, Mwaimu amesema wafuasi wa vyama wana tabia ya kuuchoka uongozi hasa unapodumu kwa muda mrefu.

Alisema hilo limeshashuhudiwa kwa viongozi mbalimbali wa mataifa duniani, wameishia kuondolewa madarakani kwa nguvu kwa sababu walishachokwa.

“Hii ni dhana sahihi kwani hata Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere aliliona hilo na kuamua kung’atuka,” amesema.

Akijibu baadhi ya hoja ya upatikanaji wa fedha za chama, Mkurugenzi wa Itifaki, Uhusiano na Mambo ya Nje, John Mrema amesema Katiba ya chama hicho ibara ya 5.3, imeweka sharti kuwa ni wajibu wa kila mwanachama kutafuta rasilimali za kuendesha.

“Sasa hoja kwamba kuna mtu mmoja mwenye jukumu la kutafuta rasilimali ndani ya chama inatoka wapi?  Wakati kila mwanachama anatakiwa kuchangia chama kwa mujibu wa katiba yetu,” amesema.

Ametaja pia ibara ya 7.7.16(f) kazi za Kamati kuu ya chama, akisema ndio yenye jukumu la kuandaa na kutoa mapendekezo kwa Baraza kuu, mikakati ya kupata mahitaji ya rasilimali za kuendesha kampeni za wagombea wa chama katika chaguzi za kiserikali.

“Katiba ibara ya 7.7.12(h) inasema kazi za Baraza Kuu  ni  kuthibitisha mikakati na rasilimali za kuendesha kampeni za wagombea wa chama katika chaguzi za Serikali hususani uchaguzi mkuu na uchaguzi wa serikali za mitaa,” amesema.

Ametaja pia ibara ya 8.1 inayoeleza mapato ya chama yatatokana na ada na viingilio vya wanachama michango ya hiari ya wanachama na wafuasi wa chama.

“Tatizo ni pale watu wasipotimiza wajibu wao wa kutafuta rasilimali na kiongozi wa taasisi hawezi kuona taasisi inafeli wakati anatakiwa kuhakikisha taasisi haifi, akitimiza wajibu wake badala ya kupongezwa anabezwa na kutuhumiwa,” amesema.

Kuhusu ukomo wa madaraka, amesema: “Kuna utaratibu umewekwa na njia ya kufuatwa ili kufikia huko, mwenye hoja alete kwa utaratibu uliowekwa.”

Related Posts