Makoba aaga akikumbuka sekeseke la wizara nne

Dodoma. Aliyekuwa Msemaji Mkuu wa Serikali, Thobias Makoba amesema changamoto za kushughulikia wizara nne kwa wakati mmoja zilimpa msukumo mkubwa wa kujifunza na kufanya kazi kwa bidii.

Akikabidhi ofisi kwa Msemaji Mkuu wa Serikali mpya, Greyson Msigwa leo Ijumaa Desemba 13, 2024, Makoba amesema anaondoka akiwa amejifunza mengi zaidi kuliko awali.

Amesema alipoanza kazi hiyo Juni 15, 2024, alikumbushwa na mwandishi mmoja kuwa anapaswa kuwa tayari kwa changamoto, jambo aliloliona kuwa kweli.

“Nimeondoka nikiwa nimeshughulishwa na nimeimarika, tofauti na nilivyokuwa nilipoanza,” amesema.

Ametolea mfano wa siku alipolazimika kushughulikia masuala ya wizara nne kwa wakati mmoja, akibainisha kuwa hilo lilimhitaji kutumia juhudi za hali ya juu kupata majibu ya haraka kwa maswali ya waandishi wa habari.

Desemba 8, 2024, Rais Samia Suluhu Hassan alimteua Makoba kuwa balozi, akitoka kwenye nafasi ya msemaji mkuu wa Serikali.

Makoba amewashukuru waandishi wa habari kwa uzalendo na ushirikiano wao katika kipindi chake, akisema kalamu na picha za waandishi zina uwezo wa kujenga au kubomoa jamii.

Amekumbuka tukio la janga la kuanguka kwa ghorofa la Kariakoo akisema alishirikiana kwa karibu na waandishi wa habari kwa siku tatu mfululizo kuhakikisha jamii inapata utulivu.

Kwa upande wake, Msigwa amesisitiza umuhimu wa waandishi wa habari kuhimiza umoja na utulivu wa Taifa, akitoa rai kwao kushirikiana na Serikali katika kuhakikisha taarifa sahihi na zenye manufaa zinawafikia wananchi.

Amesema sekta ya habari ni mhimili wa nne usio rasmi lakini wenye nguvu kubwa katika kuleta au kuondoa utulivu.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nicholaus Mkapa ametangaza katika hafla hiyo, kuundwa kwa Bodi ya Ithibati ambayo inasubiri kuzinduliwa.

Related Posts