Kilosa. Zuberi Habibu (45), mkazi wa Kijiji cha Madudumizi B, Kata ya Zombo, Kilosa mkoani Morogoro, anashikiliwa na polisi kwa tuhuma za mauaji ya watu wawili, akiwemo baba yake mzazi, pamoja na kumjeruhi mwenyekiti wa kijiji hicho.
Majeruhi wa tukio hilo, ambaye ni Mwenyekiti wa Kijiji cha Madudumizi, Hamis Msabaha akizungumza na Mwananchi leo Ijumaa Desemba 13, 2024, amesema chanzo cha tukio hilo ni mgogoro wa muda mrefu wa mipaka ya mashamba, unaoendelea ndani ya familia ya mtuhumiwa.
“Marehemu ambaye ni baba wa mtuhumiwa aliniita nije kusimamia upimaji wa mipaka. Tulianza kazi hiyo, lakini baadaye Zuberi alifika na kuniambia niondoke eneo hilo,” amedai Msabaha.
Anasema hali ilibadilika ghafla walipokuwa wakijaribu kumtuliza baada ya Zuberi kunivamia na kunichoma kisu.
“Alinikata kidole na kunichoma kifuani kwa kisu. Nilidondoka chini na kupoteza fahamu. Nilipozinduka, nilijikuta niko hospitali ya wilaya,” amesimulia Msabaha.
Na amebainisha kuwa mgogoro huo ulitokana na mtuhumiwa kumzuia baba yake kukodisha mashamba, licha ya juhudi za mara kwa mara za usuluhishi.
Alisimulia chanzo cha mgogoro huo, jirani wa familia hiyo, Abdalah Atanasi amesema mgogoro kati ya mtuhumiwa na baba yake ulikuwa unaibuka mara kwa mara, mtuhumiwa akishinikiza apewe umiliki wa mashamba hayo na kumzuia baba yake kuyakodisha.
“Ugomvi mkubwa upo kwenye umiliki wa mashamba, kijana huyu hataki baba yake ayakodishe, bali yeye ndiyo afanye kazi hiyo, lakini mashamba hamiliki yeye,” amedai jirani huyo.
Juhudi za kumtafuta Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro azungumzie tukio hilo zinaendelea, lakini Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Shaka Hamdu Shaka amethibitisha kuwepo kwake.
Shaka amewataka waliouawa kuwa ni Habibu Liomite, baba mzazi wa mtuhumiwa na Hassani Khalid, mjumbe wa serikali ya mtaa.
“Baba wa mtuhumiwa alifariki wakati akipatiwa matibabu katika Zahanati ya Zombo na nimeambia sababu ya kifo alikuwa amepoteza damu nyingi sana,” amesema Shaka.
Aidha, mkuu wa wilaya amesema Mwenyekiti wa Kijiji, Msabaha bado anaendelea kupatiwa matibabu na mtuhumiwa ameshakamatwa na polisi na utaratibu mwingine wa kisheria unaendelea kabla hajafikishwa mahakamani.
“Lakini pia mamlaka zinaendelea kuchunguza chanzo cha mgogoro huo wa kifamilia,” amesema mkuu huyo wa wilaya.