Morogoro. Mwenyekiti wa Kitongoji cha Ngoisani Kilosa mkoani Morogoro, Lepapa Kidole amekamatwa kwa tuhuma za kuchochea vijana kutoka jamii ya wafugaji kuwashambulia kwa fimbo na virungu wakulima wa Kijiji cha Matongolo.
Tukio hilo limetokea baada ya mwenyekiti huyo kudaiwa kuwashawishi vijana wa kimaasai kuanzisha vurugu na kuwapiga wakulima wakiwazuia kulima miwa wakiotaka walime mazao ya chakula kama mahindi na mtama, ili wapate malisho ya mifugo.
Edward Malle, mmoja wa majeruhi ameeleza kuwa vurugu hizo zilitokea Desemba 11, 2024, saa 11 jioni, wakati walipokuwa shambani wakikagua baadhi ya wakulima wakiandaa mashamba yao kwa ajili ya kilimo.
“Tulipofika shambani wakaanza kujitokeza mmoja mmoja, baadaye kundi la vijana zaidi ya 30 walituzunguka wakatwambia tuzime matrekta tuondoke,” amesema Malle.
Ameongeza kuwa baada ya kuzima matrekta hayo, waliondoka eneo hilo lakini ghafla wakaona kundi hilo la vijana likiwafuata na wengine walikuwa tayari wamewazunguka, wakaanza kuwapiga na fimbo na virungu.
Ofisa Mtendaji wa Kata ya Dumila, Hamza Ally ameeleza kuwa mgogoro huo ulitatuliwa mara kadhaa na Serikali, lakini Lepapa amekuwa akiendeleza migogoro hiyo kwa masilahi ya wafugaji.
“Juzi tu ofisa tarafa aliitisha kikao, baada ya kikao hicho yakatolewa maazimio ya kuwa wakulima waachwe walime zao lenye manufaa kwao, lakini mwenyekiti huyo alitoa kauli zilizoashiria kutokubaliana na uamuzi wa kikao hicho,” amesema Ally.
Karimu Sululu, meneja wa Chama cha Wakulima wa Miwa Dumila ameiomba kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya kuwawekea ulinzi pale watakapoanza kilimo kwani wafugaji hao wamekuwa wakikiuka matamko ya Serikali kila yatolewapo.
Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Shaka Hamdu Shaka amefika katika mashamba ya wakulima hao na kueleza kuwa mgogoro huo ulishafika ofisini kwake na ulitatuliwa, lakini ushawishi wa watu wachache umekuwa ukiibua mgogoro huo mara kwa mara.
“Wananchi wa Kilosa wana tabia ya kuibua migogoro iliyotatuliwa pale tu anapokuja kiongozi mpya katika eneo husika, hili halikubaliki,” amesema Shaka.
Ameeleza kuwa kamati yake inamshikilia mwenyekiti wa kitongoji cha Ngoisan kwa mahojiano zaidi ili awataje vijana aliowatuma kutekeleza uhalifu huo.
“Sasa maagizo ya Serikali ni kwamba wakulima hawa waachwe walime zao lolote ambalo linawaingizia kipato bila bughudha yoyote,” amesema.
Aidha, amewataka wakazi wa eneo hilo kujikita katika kilimo cha miwa ili waweze kukisaidia kiwanda cha kusindika sukari cha Mkulazi.